Kiongozi wa kijeshi Michel Rukunda auawa katika shambulio la ndege isio na rubani

Michel Rukunda, almaarufu Makanika, aliuawa Februari 19 katika eneo la Minembwe, katika mkoa wa Kivu Kusini. Afisa wa zamani wa cheo cha kanali katika jeshi la Kongo, aliwasilishwa kama kiongozi wa Twirwaneho, kundi lenye silaha ambao wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanakielezea kuwa na uhusiano na Muungano wa Mto Kongo (AFC), ambao M23 ni mwanachama.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na vyanzo vya habari, Michel Rukunda aliuawa siku ya Jumatano mwendo wa saa 5 mchana wakati wa shambulio la ndege isio na rubani. Shambulio hilo lililenga makao yake makuu huko Gakangala, eneo la milimani lililoko takriban kilomita kumi kutoka katikati mwa Minembwe. Kulingana na vyanzo hivi, kanali huyo wa zamani wa FARDC aliuawa katika shambulio la kuvizia , kwani hakuna mapigano yaliyoripotiwa katika eneo hilo siku mbili kabla ya shambulio hilo. Alifariki pamoja na walinzi wake kadhaa. Kundi la wapiganaji la Twirwaneho, aliloliongoza, linashutumu jeshi la Kongo kuhusika na shambulio hilo.

Mzaliwa wa Minembwe, Michel Rukunda alilfahamu vyema eneo lake. Kanali huyo wa zamani wa jeshi la Kongo alijitoa katika jeshi la Kongo, FARDC mnamo mwaka 2020 na kuamua kuanzisha kundi lake lenye silaha la kulinda kabila lake la Banyamulenge dhidi ya mashambulizi ya watu kutoka makabila mengine katika mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa DRC. Akiwa na umri wa miaka 51, amekuwa kwenye orodha ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa tangu mwaka jana. Alishutumiwa kwa kusajili watoto wenye umri kuanzia miaka 12 kupigana, kitendo kilichorekodiwa na Umoja wa Mataifa tangu mwezi Februari 2024. Jina lake pia lilionekana kwenye orodha nyeusi ya Marekani. Lakini ndani ya jamii yake, alionekana kuwa mtu aliyejitoa ili kulinda vijiji na mifugo kutokana na mivutano ya ndani.

Kifo chake kimezidisha kudorora kwa hali ya usalama. Siku ya Ijumaa, Februari 21, mapigano mapya yaliripotiwa kati ya FARDC na wapiganaji wa Twirwaneho. Kulingana na mmoja wa wapiganaji wa kundi hilo lenye silaha, jeshi la Kongo lilichukua fursa ya maombolezo hayo kuanzisha mashambulizi.