
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani ametoa mwito wa kufanyika uchunguzi wa jamii ya kimataifa kuhusu “mauaji ya halaiki” ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.
Papa Francis, Kiongozi wa Wakatoliki duniani amesema kuwa, mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya ukanda wa Gaza na Lebanon ni jinai za kivita na utawala unaokalia kwa mabavu Palestina umekiuka sheria zote za vita.
Akitumia maneno kama vile “ugaidi” na “mauaji ya halaiki” ambayo wanadiplomasia wa Vatican hadi sasa wamekuwa wakijizuia kuyatamka, Papa Francis ameonyesha radiamali kali dhidi ya vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, mwezi uliopita wa Oktoba, utawala wa Kizayuni ulianzisha kampeni ya kuangamiza kabisa kila kitu ikiwa ni pamoja na wakazi wote wa kaskazini mwa Ghaza huku maelfu ya watu wakilazimika kuhama eneo hilo wakiwemo madaktari.
Hakuna chakula chochote kilichoingia kaskazini mwa Gaza tangu wakati huo huku utawala wa Kizayuni ukiendelea kuwashambulia kinyama wananchi wa Palestina ili kuwalazimisha kuhama.