Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu: Utawala wa Kizayuni umefanya makosa ya kimahesabu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamefanya mahesabu potofu kuhusu Jamhuri ya Kiislamu kwa sababu hawawafahamu vijana na wananchi wa Iran na bado hawajaweza kuelewa ipasavyo nguvu, uwezo, uvumbuzi na irada ya taifa hili.

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo Jumapili katika kikao chake na maelfu ya familia za mashahidi wa usalama ameashiria uhalifu wa kivita unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ghaza na Lebanon na kutoa wito wa kuundwa “muungano wa kimataifa” dhidi ya utawala huu muovu.

Ayatullah Khamenei amesema kuhusu hatua ya shari ya utawala wa Kizayuni siku ya Jumamosi (26 Oktoba) kwamba: ‘Kuhusu kosa hili walilofanya, wanajikuza kwa malengo maalumu, lakini pia ni makosa kulidogesha tukio hilo na kusema kwamba halikuwa chochote wala si jambo muhimu.’

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: ‘Bila shaka viongozi wanapaswa kainisha kwa usahihi ubora wa kazi hiyo na kufanya yale ambayo yana maslahi kwa nchi na taifa, ili Wazayuni waelewe taifa la Iran ni nani na vijana wake wako vipi.’

Akiashiria jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza zikiwemo za kuuliwa shahidi watoto elfu kumi na zaidi ya wanawake elfu kumi, jambo ambalo ni kielelezo cha jinai za kikatili zaidi za kivita, Ayatullah Khamenei amekosoa kushindwa kukubwa kwa nchi na jamii ya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa kukabiliana na vitendo vya utawala huo huko Gaza na Lebanon. Amesema: ‘Vita vina sheria, kanuni na mipaka, na sio kama kwamba mipaka yote inakiukwa katika vita, lakini genge la wahalifu linalotawala maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina limevunja na kukanyaga mipaka na sheria zote.’

Kiongozi Muadhamu alipokutana na familia za Mashahidi wa Usalama

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa ni muhimu kwa serikali hususan za Kiislamu kusimama kidete dhidi ya utawala huo katili na kuunda muungano wa kimataifa dhidi yake na kuongeza kuwa: ‘Kusimama kidete hakumaanishi kukata misaada ya kiuchumi kwa sababu ni wazi kuwa kuusaidia kiuchumi utawala ghasibu ni mojawapo ya dhambi mbaya na kubwa zaidi, bali kusimama kidete kunamaanisha kuunda muungano wa kimataifa wa kisiasa, kiuchumi na ikibidi, wa kijeshi dhidi ya utawala huu habithi unaofanya jinai za kikatili zaidi za kivita.’

Vile vile amezihutubu familia tukufu za mashahidi wa usalama na kuwataja mashahidi hao kuwa miongoni mwa mashahidi bora wa njia ya haki na huku akiashiria umuhimu wa miundomsingi ya usalama katika masuala yote ya jamii na nyanja mbalimbali za maisha ya watu, amesisitiza kuwa: ‘Ni Iran yeye nguvu tu ndiyo inayoweza kudhamini usalama na maendeleo ya nchi na taifa. Kwa hivyo, Iran inapasa kuimarika zaidi siku baada ya siku katika nyanja zote za kiuchumi-kisayansi-kisiasa na kiulinzi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja nguvu ya kitaifa kuwa ndiyo njia pekee ya kuwa salama Iran na kuongeza kuwa: ‘Ili kuilinda nchi, jamii na maendeleo, Iran inapaswa kuwa na nguvu katika nyanja zote za kiuchumi, kisayansi, kiulinzi, kisiasa na kiutawala na nyanja nyinginezo.’