Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduuzi ya Kiislamu, Jumamosi ya jana alihutubia kikao cha maelfu ya wanafunzi na wasomi wa vyuo vikuu akieleza sababu za kimsingi za mapambano ya takriban miaka 70 ya taifa la Iran dhidi ya dhulma na sera za kupenda makuu na kujitanua za Marekani.
Amesema: Mapambano ya Kiislamu, kitaifa, ya busara na kibinadamu ya taifa la Iran dhidi ya ubeberu wa Marekani ambayo yanaoana na sheria za kimataifa yataendelea kwa kufuata ramani sahihi ya njia na bila kupuuza au kuzembea.
Ayatullah Khamenei ameashiria nukta kadhaa muhimu katika hotuba hiyo ambayo imetolewa kwa mnasaba wa kuadhimisha kumbukumbu ya kutekwa pango la ujasusi la Marekani (ubalozi wa Marekani mjini Tehran) uliotwaliwa na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Iran tarehe 4 Novemba 1979, inayojulikana kama Siku ya Kitaifa ya Mapambano dhidi ya Ubeberu wa Kimataifa:
1. Hatua ya kimantiki kwa mujibu wa dini na sheria.
Nukta ya kwanza ni kwamba, kwa mtazamo wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, mapambano ya taifa la Iran dhidi ya ubeberu wa Marekani yana msingi wa kimantiki na kidini. Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, kumkufuru na kumkana Taghuti ni miongoni mwa masharti muhimu ya imani ya Mwislamu. Imam Ali Khamenei anaitambua Marekani kuwa kielelezo cha Taghuti na anasema kwamba: “Harakati jumla ya taifa na viongozi katika kukabiliana na ubeberu wa kimataifa na chombo cha kihalifu kinachotawala mfumo wa sasa wa dunia ni hatua ya kimantiki inayooana na Sharia, maadili na kanuni za kimataifa, na taifa na viongozi hawatazembea hata kidogo katika suala hili.”
2. Mapambano yanatokana na utawala dhalimu wa Marekani
Jambo lingine ni kwamba kwa mtazamo wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, mapambano ya taifa la Iran dhidi ya Marekani yanatokana na “ukandamizaji na uonevu wa kikatili wa serikali ya Marekani kwa taifa pendwa la Iran. Hapana shaka kwamba, Marekani inazikandamiza nchi zinazoendelea, hasa nchi zenye utajiri wa mafuta za eneo la Asia Magharibi, na hairuhusu nchi hizo kuwa huru na kujitawala. Moja ya sababu kuu za uadui na uhasama wa kupindukia wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni sera za Iran za kutaka kujitawala katika mfumo wa dunia na upinzani wake dhidi ya ubeberu wa Marekani. Kwa sababu hiyo, serikali ya Marekani imechukua hatua za kidhalimu na kikatili dhidi ya taifa la Iran katika kipindi cha miaka 45 iliyopita katika sura mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuitwisha vita, kuiwekea vikwazo vya pande zote vya kiuchumi, kusaidia makundi ya kigaidi, na kuanzisha kampeni ya kuchafua jina la Iran au Iranophobia katika eneo la Asia Magharibi. Katika suala hili, Imam Ali Khamenei amekutaja kutekwa Pango la Ujasusi la Marekani baada ya kubainisha dhati na hakika ya kazi za ubalozi Marekani mjini Tehran kuwa ni nukta muhimu sana na tukio la kihistoria ambalo haliwezi kusahaulika, na kusema kuwa: Ni kwa sababu hii ndiyo maana, kutokana na muono wake wa mbali, Imam Khomeini akauunga mkkono harakati hiyo ya wanafunzi wa vyuo vikuu.

3. Mapambano dhidi ya Marekani yanawiana na mantiki ya kimataifa
Sababu ya tatu ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu ulazima wa kuendeleza mapambano dhidi ya Marekani inahusiana na mantiki ya kimataifa ya mapambano haya. Marekani ndiyo muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika jinai zisizo na kifani zinazofanywa dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza. Takriban watu 50,000 wameuawa shahidi na Wazayuni katika kipindi cha miezi 13 iliyopita, na jinai hizi za kinyama, kama anavyosema Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, “zinatekelezwa kwa misaada ya kijeshi na kisiasa na ushiriki wa waziwazi wa Marekani.”
Kwa mujibu wa sababu hizi zilizotajwa, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu anasisitiza mambo mawili muhimu kuhusu mapambano dhidi ya Marekani.
Nukta ya kwanza ni kwamba ni kosa kubwa kufungamanisha mwanzo wa mapambano ya taifa la Iran dhidi ya Marekani na kutekwa ubalozi wa nchi hiyo mjini Tehran, na kwa mujibu wa matamshi ya Kiongozi wa Mapinduzi, huo ni upotoshaji wa historia. Mwanzo wa uadui wa Iran na Marekani unarudi nyuma miaka mingi iliyopita, na kwa mtazamo wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamuu, unarejea kwenye mapinduzi ya Agosti 19, 1953 (Mordad 28, 1332).

Nukta ya pili ni kwamba, mapambano dhidi ya Marekani si jambo la muda na la kupita bali kwa mujibu wa matamshi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu; “Mapambano ya taifa la Iran dhidi ya ubeberu wa Marekani ni jambo la kudumu, endelevu na katika muktadha wa maisha ya taifa.
Nukta ya tatu ni kwamba baadhi ya watu na mirengo ya ndani na nje ya nchi inajaribu kutakasa na kusafisha sura ya kibeberu ya Marekani. Hata hivyo, jinai kubwa zilizofanywa na Marekani dhidi ya taifa la Iran na baadhi ya mataifa katika eneo la Magharibi mwa Asia, hususan taifa la Palestina, zinawafanya washindwe kufikia lengo la kutakasa sura chafu ya Marekani.