Mkuu wa Kanisa la Uingereza, ambaye ni kiongozi wa kiroho wa Kanisa la Kianglikana duniani anashinikizwa ajiuzulu baada ya uchunguzi kubaini kuwa alishindwa kuwajulisha polisi mara tu alipofahamu kuhusu unyanyasaji wa kimwili na udhalilishaji wa kingono uliofanywa na mfanyakazi wa kujitolea katika kambi za Kikristo za msimu wa joto.
Baadhi ya wajumbe wa Sinodi Kuu, ambalo ni Bunge la Kitaifa la Kanisa hilo, wamezindua kampeni ya ombi la kumtaka Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby ajiuzulu, wakisema “amepoteza imani ya makasisi wake”. Hadi jana Jumatatu asubuhi kwa saa za London, ombi hilo lilikuwa limeshapata saini zaidi ya 1,800 kwenye tovuti ya Change.org.
Wito wa kumtaka Welby ajiuzulu umeongezeka tangu Alkhamisi wakati Kanisa lilipotoa matokeo ya uchunguzi huru kuhusu John Smyth, ambaye aliwanyanyasa na kuwadhalilisha kingono, kisaikolojia na kimwili wavulana na vijana wapatao 30 nchini Uingereza na 85 barani Afrika kwa zaidi ya miongo mitano.
Ripoti hiyo ya kurasa 251 inatoa hitimisho kwamba, Welby alishindwa kumripoti Smyth kwa mamlaka husika alipofahamishwa kuhusu unyanyasaji huo mnamo Agosti 2013, muda mfupi baada ya kuwa Askofu Mkuu wa Canterbury.

Ripoti iliyoandaliwa kwa uongozi wa Keith Makin imesema, maafisa wa Kanisa walibaini kwa mara ya kwanza kufanyika kwa udhalilishaji huo mwaka 1982, walipopokea matokeo ya uchunguzi wa ndani kuhusu Smyth. Lakini wapokeaji wa ripoti hiyo “walifanya ubabaishaji na ufichaji” ili kuzuia matokeo ya uchunguzi kufichuliwa.
Kati ya mwaka 1984 na 2001, Smyth aliishi Zimbabwe, na kisha Afrika Kusini. Aliendelea kuwanyanyasa kingono wavulana na vijana wa kiume nchini Zimbabwe, na kuna ushahidi kwamba udhalilishaji huo uliendelea nchini Afrika Kusini hadi kifo chake Agosti 2018.
Unyanyasaji wa kingono uliofanywa na Smyth haukuwekwa wazi hadi ulipofanywa uchunguzi 2017 na Chaneli ya 4 ya mtandao wa televisheni wa Uingereza, ambao ulipelekea polisi wa Hampshire kuanzisha uchunguzi. Polisi walikuwa wakipanga kumhoji Smyth wakati wa kukaribia kifo chake na walikuwa wakijiandaa kumrudisha Uingereza.
Askofu Mkuu wa Canterbury ndiye mkuu wa Kanisa la Uingereza na anachukuliwa kuwa kiongozi wa kiroho wa Ushirika wa Anglikana, ambao una zaidi ya wanachama milioni 85 katika nchi 165 duniani…/