Kiongozi maarufu wa upinzani Tanzania na wenzake waachiliwa huru kwa dhamana

Freeman Mbowe, kiongozi wa chama cha upinzani cha Chadema nchini Tanzania jana aliachiliwa huru kwa dhamana baada ya kukamatwa siku ya Ijumaa yaani siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa wa Novemba 27 nchini humo.

Mashirika mbalimbali ya habari ya ndani na nje ya Tanzania likiwemo la Africa News yametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, chama cha Chadema kilitangaza kuachiwa huru Mbowe jana Jumamosi kupitia mtandao wa kijamii wa X. Taarifa hiyo ya Chadema imesema: “Mwenyekiti Freeman Mbowe (…) na viongozi wengine waliokuwa wanashikiliwa katika kituo cha polisi cha Vwawa wameachiwa huru kwa dhamana.”

Uchaguzi wa serikali za mitaa wa Novemba 27 nchini Tanzania unafuatiliwa kwa karibu kama mtihani muhimu wa hali ya kisiasa ya nchi hiyo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba 2025.

Shirika la habari la Africa News limeandika: “Tangu ashike madaraka mwaka 2021, Rais Samia Suluhu Hassan amechukua baadhi ya hatua za kulegeza vikwazo vya vyombo vya habari na upinzani; hata hivyo, watetezi wa haki za binadamu wanadai kwamba kuwekwa kizuizini kiholela kunaendelea.”

Pia limeandika: “Wakati wa uongozi wa Magufuli, mikusanyiko ya upinzani ilikandamizwa na polisi, na mara nyingi viongozi wao walikamatwa. Vigogo wa Chadema, Mbowe na naibu wake Tundu Lissu, walishambuliwa na watu wasiojulikana, huku wote wakidai kuwa hujuma hizo zilitokana na misimamo yao ya kisiasa.”

Lakini wakati wa urais wa Samia Suluhu Hassan, harakati za vyama vya siasa vikiwemo vya upinzani zimereshwa ikiwa na maana ya kuweko msukumo upya wa uwazi wa kisiasa na mageuzi nchini Tanzania.