King Kikii kuzikwa Jumatatu makaburi ya Kinondoni

Dar es Salaam. Mwili wa msanii mkongwe wa muziki wa dansi Tanzania, Boniface Kikumbi maarufu ‘King Kikii’ unatarajiwa kupumzishwa katika nyumba yake ya milele Jumatatu Novemba 18, 2024 jijini Dar es Salaam.

Ratiba hiyo imetolewa na mtoto wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Joseph.

“Tumekaa kikao tukakubaliana tutamzika siku ya Jumatatu, lakini kukiwa na mabadiliko yoyote tutasema, tutampumzisha katika makaburi ya Kinondoni na tunafanya utaratibu aagwe viwanja vya leaders,”amesema Joseph.

King Kikii amefariki usiku wa kuamkia leo Novemba 15, 2024 nyumbani kwake Mtoni Kwa Aziz Ally jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Jesca Kikumbi ambaye ni mtoto wa marehemu amezungumzua dakika za mwisho za baba yake zilivyokuwa

“Nimemuuguza hapa kwa siku tatu za mwisho nilikuwa nampikia namlisha. Serikali imemsaidia alipelekwa India kutokana na saratani ya tezi dume kumbe saratani ilikuwa imeshapanda mpaka kwenye ini madaktari wamejitahidi sana watato wake wajitahidi sana.

“Kabla hajafariki asubuhi nilimpikia mtori mchana pia nikampikia uji akanywa sana baada ya kumaliza alikunywa maji sana kuliko kawaida nikamwambia baba leo umenifurahisha ukiendelea hivi nitakuwa na amani,” amesema Jesca

Aidha Jesca amesema kilichofanya wamtoe hospitali ni baada ya kuona anaendelea vizuri.

“Tarehe 12 mwezi huu daktari alimruhusu akataambia anaendelea vizuri na tunaweza muuguza akiwa nyumbani,”amesema Jesca

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi