Dar es Salaam. Mshumaa umezimika. Hivi ndivyo tunaweza kusema baada ya mwili wa msanii mkongwe wa muziki wa dansi Tanzania, Boniface Kikumbi maarufu ‘King Kikii’ kupumzishwa leo Novemba 18, 2024 katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

King Kikii ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 15, 2024 nyumbani kwake Mtoni Kwa Aziz Ally jijini Dar es Salaam kwa maradhi ya saratani ya ini alifariki akiwa na miaka 77.
Wakati akisoma wasifu wa baba yake katika Viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam, Joseph Kikumbi ambaye ni mtoto wa marehemu amesema mwanamuziki huyo nguli wa miondoko ya dansi ameacha watoto 11 ambao kati yao wawili wamefariki dunia.

Ikumbukwe kuwa King Kikii katika moja ya mahojiano aliyowahi kufanya na Mwananchi alisema kipindi akiwa na umri wa miaka sita akisoma shule ya awali mwaka 1952 alifurahishwa na kuvutiwa na kundi la muziki kutoka nchini Afrika Kusini ambalo mwanamuziki mahiri Miriamu Makeba alikuwa akifanyia kazi.

“Nimezunguka nchi nyingi kufanya muziki na nimeona shoo nyingi za kimataifa hakuna aliyewahi kuvunja rekodi ya kile nilichokiona siku hiyo, waliimba kwa ustadi mkubwa, walicheza kama hawana mifupa kwenye miguu na mwili kwa ujumla, Makeba alikuwa ni kinara wa kuimba,”alisema King Kikii enzi za uhai wake.