
MSHAMBULIAJI kinda wa Tanzania, Mourice Sichone anayekipiga katika timu ya Trident FC ya Zambia amesema anatamani aisaidie timu hiyo kuipandisha Ligi Kuu msimu huu.
Msimu uliopita Trident ilishuka daraja na kushiriki Ligi Daraja la Kwanza baada ya kumaliza mkiani na pointi 26.
Kinda huyo (18) alisajiliwa dirisha dogo akitokea Mpulungu Harbour FC ya nchini humo akicheza mechi 12 na kufunga mabao manne na asisti tano.
Akizungumza na Mwanaspoti, Sichone alisema anatamani kuisaidia timu yake kushinda kila mchezo kwa kutupia ili irejee Ligi Kuu msimu ujao.
“Natamani sana tufanye vizuri na timu yangu turejee Ligi Kuu, hatujaanza vibaya lakini hadi sasa nimecheza mechi moja nyingine ni za kirafiki,” alisema Sichone
Nyota huyo kabla ya kujiunga na timu za Zambia alitokea kwenye akademi ya Mabibo, pia aliwahi kucheza Simba na Azam za vijana.