Kinana alivyostaafu na rekodi ya barua za kujiuzulu CCM

Januari 18, saa 2:00 asubuhi, Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), ulishajaa. Wajumbe 1,924, wasanii, waandishi wa habari, waalikwa mbalimbali, hadi waliotoka nje ya nchi.

Weka kando chachandu za mkutano, jinsi Dodoma ilivyogeuka ya kijani, hisia ni Makamu Mwenyekiti mpya. Yalishatajwa majina mengi. Waziri Mkuu wa Tisa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda, alitajwa zaidi. Veterani wa siasa Tanzania, Stephen Wasira, aligeuka mada ya asubuhi ndani ya ukumbi. Aina ya uingiaji wake, alivyosindikizwa na vijana wenye suti nyeusi, ilisababisha ujenzi wa matarajio. Ni Wasira! Kweli akawa Wasira.

Wasira, 79, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Kanali mstaafu, Abdulrahman Kinana, 73, aliyeomba kujiuzulu, kisha Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan akaridhia ombi lake. Taarifa ya Kinana kujiuzulu ilitoka Julai 29, 2024. Barua ya Kinana kujiuzulu umakamu mwenyekiti Julai 2024, ni ya nne, zote zikiwa na maudhui yanayofanana ndani ya CCM, kutoka kwa mwanasiasa huyo mwenye historia ndefu ya utumishi. Barua hizo, kwa sehemu kubwa zinampambanua Kinana kuwa mwanasiasa wa aina gani.

Mwaka 1997, Kinana akiwa na umri wa miaka 45, alitangaza kutogombea nafasi yoyote ndani ya CCM. Kisha, alikwenda Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani, alikokwenda kujiendeleza kimasomo. Tangu mwaka 1997, Kinana hajawahi kushiriki kinyang’anyiro chochote cha uongozi.

Mwanasheria mashuhuri Afrika, Profesa PLO Lumumba, husema: “Mtumbuizaji mzuri hujua wakati wa kushuka jukwaani.” Hadithi ya Kinana ni zaidi ya mtumbuizaji bora na jukwaa. Inapambanua hulka yake ya kutopenda kukaa kwenye ofisi ya umma kwa muda mrefu.

Mwaka 2001, Kinana aliombwa kuchukua fomu ili awe Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA). Alikuwa mgombea pekee na alishinda. Hiyo inamfanya Kinana kuwa Spika wa kwanza wa Bunge la Afrika Mashariki. Nako alidumu muhula mmoja na kukabidhi kijiti.

Mtu wa misheni kubwa

Kama nitatumia neno moja kueleza sifa ya Kinana, basi ni la Kiingereza, “classy”. Yakiwa mawili ni mwanasiasa mwenye kutazamwa kama daraja la juu la ubora. Kinana ni classy, kwa maana hudumisha tabia njema, na kuonesha heshima kwa kila aliye karibu naye au anayekutana naye kwa mara ya kwanza.

Utumishi wa Kinana tangu jeshini, wakati huo wa mfumo wa chama kimoja na jeshi likiwa sehemu ya Tanu na baadaye CCM, hadi Januari 18, 2025, alipostaafu rasmi na kumpisha Wasira, ni zaidi ya miaka 50. Ni miaka ya utumishi uliotukuka, wenye kujitoa bila ubinafsi. Kinana amekuwa jabali wa misheni kubwa za Serikali na CCM. Bunge la Afrika Mashariki lilipoanzishwa na Tanzania kutakiwa kutoa spika, Kinana alikuwa jawabu la kila kitendawili. Upande wa CCM, Kinana ni tingatinga. Alisawazisha magugu, akageuza makorongo kuwa tambarare. Uchaguzi Mkuu 1995, ambao ulikuwa wa kwanza kushirikisha vyama vingi tangu nchi ipate uhuru, Kinana alikuwa kiongozi wa kampeni za CCM, kuhakikisha mgombea urais, Benjamin Mkapa, anashinda.

Kinana aliongoza pia kampeni za CCM, Uchaguzi Mkuu 2000, 2005, 2010 na 2015, alikuwa ndiye Katibu Mkuu CCM. CCM baada ya kupepesuka kwenye Uchaguzi Mkuu 2010, aliyekuwa Mwenyekiti, Jakaya Kikwete, alipata shida kujenga chama kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015. Mgawanyiko ndani ya CCM ulikuwa mkubwa. Makundi ya urais yalikizidi nguvu chama. Aprili 2011, Kikwete aliunda sekretarieti mpya iliyoongozwa na Wilson Mukama.

Ndani ya mwaka mmoja, ilionekana CCM bado haijapona. Kikwete aliijua suluhu ya CCM ni Kinana, ila kila alipomshirikisha amteue kuwa Katibu Mkuu, alimkatalia. Ilibidi Kikwete awashirikishe wazee, Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi na Mkapa, ambao walifanikiwa kumshawishi Kinana, akakubali.

Kazi ambayo Kinana aliifanya kati ya mwaka 2012 na 2015, iliwezesha kurejesha uhai wa CCM. Aliifanya CCM kuwa sauti ya wananchi na kuwashughulikia mawaziri ambao walionekana hawawajibiki ipasavyo.

Juhudi hizo ziliiwezesha CCM kuvuka salama kipindi ambacho ushindani wa kisiasa ulikuwa mkali, kuliko wakati wowote ule katika historia ya Tanzania. Vita ya urais iliipa majeraha makubwa CCM, lakini chama kilivuka. Kinana alikuwa daraja la uvukaji huo.

Nimepata kuisoma barua iliyoandikwa na Mkapa, kwenda kwa Kinana, ya Juni 4, 2018, ikiwa na kumbukumbu namba FP. III/12. Mkapa, Rais wa Tatu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tatu wa CCM, aliandika barua hiyo kumshukuru Kinana kwa uongozi wake uliowezesha kurejesha uhai wa chama hicho. Sehemu kubwa ya barua hiyo, Mkapa alitambua jinsi Kinana alivyowezesha CCM kuvuka salama Uchaguzi Mkuu 2015, ambao ulikuwa mgumu, na ugumu ukiwa ulisababishwa na minyukano ya ndani ya chama.

Barua ya Mkapa, ilikuwa hati ya kutambua utumishi bora wa Kinana, baada ya kuwa amejiuzulu ukatibu mkuu, Mei 28, 2018. Hivyo, Mkapa aliandika barua kwenda kwa Kinana, siku saba tangu alipojiuzulu ukatibu mkuu CCM. Maudhui ndani ya barua ya Mkapa ni uthibitisho kuwa Kinana ni mtu wa misheni kubwa.

Barua za kujiuzulu

Julai 2016, kuelekea mkutano mkuu maalumu wa CCM, uliomchagua Magufuli kuwa Mwenyekiti wa chama, Kinana alitokeza na kutangaza kusudio lake la kuachia ngazi. Alisema kuwa hata nafasi yenyewe aliishika kwa ombi la wazee, ila hayakuwa mapenzi yake. Wakati wa mkutano mkuu, Dk Magufuli aliikataa barua ya Kinana na kumtaka aendelee kushika nafasi ya katibu mkuu. Kinana alipokuwa akielezea alivyoafiki kuendelea na nafasi hiyo, alisema alipokea kijiti cha ukatibu mkuu kutoka kwa mtangulizi wake, Wilson Mukama baada ya kuombwa mara nyingi na Rais mstaafu, Kikwete.

Kwa maneno yake mwenyewe, Kinana alisema: “Niliona si heshima kumkatalia Rais wa nchi.”

Mwaka 2017, Kinana aliandika barua ya pili ya kuomba kujiuzulu ukatibu mkuu, nayo ilikataliwa. Mei 2018, Kinana aliandika barua ya tatu, ambayo safari hiyo, Dk Magufuli aliikubali na kumteua Dk Bashiru Ally, kushika wadhifa huo.

Aprili Mosi, 2022, Kinana alirejea CCM kama Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara. Haikuwa rahisi, bali kwa nguvu kubwa ya ushawishi kama kawaida yake. Kinana hakuwa akitaka kurejea kwenye safu ya uongozi CCM, lakini alikubali baada ya kuombwa.

Barua ya Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec) CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, Julai 29, 2024, ilimkariri Rais Samia kuwa Kinana aliomba muda mrefu kujiuzulu, kwamba hata wakati anamwomba awe Makamu Mwenyekiti, alimwahidi ingekuwa kwa muda mfupi.

Maneno hayo ni kuonesha kwamba Kinana aliombwa kushika nafasi kwa sharti la kukaa muda mfupi. Pili, aliomba kujiuzulu. Hivyo, barua ya Kinana kuomba kuachia ngazi nafasi ya umakamu mwenyekiti ni ya nne.

Kuhusu kuombwa kushika wadhifa kisha kujiuzulu, Kikwete alipata kuelezea safari ya kumshawishi Kinana kuwa Katibu Mkuu wa CCM, kwamba kila mara alipomwomba alikataa. Kabla ya Yusuf Makamba kuwa katibu mkuu, alipeleka ombi kwa Kinana akakataa. Mwaka 2012 baada ya Mukama, Kikwete alisema, alimwambia Kinana kuwa safari hiyo hakuwa na namna zaidi ya kukubali ili kukiokoa chama.

Hata wakati wa uongozi wa Rais Mwinyi na Rais Mkapa, kwa nyakati tofauti, kila mmoja akiwa Mwenyekiti CCM, alitamani kufanya kazi na Kinana kwa nafasi ya ukatibu mkuu. Kipindi hicho, Kinana alipmba asipewe nafasi hiyo kwa sababu alikuwa bado kijana. Mwinyi na Mkapa walimwelewa.

Inaleta mantiki kuwa Kinana ni hazina ya CCM, inayotumainiwa mno kipindi chama kinapopitia nyakati ngumu. Hukubali pale ambapo huona hana budi kukubali. Huitenda kazi yake, halafu yeye mwenyewe kuomba kuondoka.

Mtu wa misingi

Utumishi wake wa muda mrefu, jinsi ambavyo amekuwa akijiweka na namna anavyotambulika kijamii, kwa Kiingereza anatosheleza kuitwa “statesman”, yaani kiongozi wa kijamii mwenye uzoefu, maarifa makubwa na anayeheshimika.

Kikubwa, Kinana ni mtu wa misingi. Anapoona kuna jaribio au mpango wa kuchafua jina lake, huwa hasiti kutoka kupigania heshima yake, aliyoijenga kwa miaka mingi. Mfano ni kipindi alipojiuzulu ukatibu mkuu CCM, yalianzishwa mashambulizi dhidi yake.

Mtu aliyejitambulisha kama mwanaharakati huru, Cyprian Musiba, ambaye alijipa jukumu la kumtetea Rais Magufuli, alianza mashambulizi dhidi ya Kinana na viongozi wa kada mbalimbali, aliodai wanamhujumu Magufuli.

Ukimya wa CCM kipindi ambacho Musiba anataja majina ya viongozi katika sura ya uchonganishi, ulisababisha Kinana na Makamba, waandike waraka ambao ulitetemesha nchi. Waraka huo ulisambaa Desemba 2019.

Dhahiri, Kinana, ambaye amestaafu rasmi siasa, licha kuahidi kusaidia chama chake pale atakapohotajika, pamoja na sifa nyingi za uungwana zinazosemwa kuwa anazo, ila ni mtu wa misingi. Huwa haachi mambo yapite pale anapoona jina lake au heshima yake inachezewa.