Kinachombeba Lazaro Coastal hiki hapa

KOCHA wa Coastal  Union, Joseph Lazaro amesema uzalendo mkubwa alionao na kuuonyesha kwa timu hiyo, umemfanya awe tegemeo la Wagosi wa Kaya huku akisema imembeba na kumtambulishwa ndani na nje ya mkoa huo, kuipenda kazi na anatamani kuona wachezaji wanazifikia ndoto zao.

Kitendo cha kuifundisha timu hiyo ambayo alikuwa sehemu ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 1988/99 akiwa na kina Juma Mgunda ambaye ni kocha wa Namungo FC inamrudia picha kama yupo uwanjani anacheza.

“Nilijiunga kuichezea Coastal mwaka 1985 nilistaafu na timu hiyo mwaka 1999 ambapo nikaanza kukaa benchi kupata uzoefu kwa makocha na wakati huo huo nilikuwa nasoma kozi za ukocha,” alisema beki huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars aliyeongeza;

“Kupitia Coastal nilionekana na Yanga ambayo niliichezea kwa msimu mmoja wa 1992-1993 ambao tulichukua ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati huko Kampala, Uganda na msimu uliyofuata nikaachwa nikajiunga na Pan Africans.”

Alisema akiitazama Coastal licha ya kupitia changamoto nyingi anapata nguvu ya kuendelea kuipambania, kuhakikisha inaendelea kuwaajili vijana wenye vipaji ambao watazisaidia familia zao kuishi.

“Nilisajiliwa kutokea mtaani, nikajiunga na African Sports kisha nikaenda Coastal ndiyo maana napata nguvu ya kuangalia mafanikio ya mbele kuliko changamoto zinazotuzunguka,” alisema.

Alizungumzia namna ambavyo msimu huu haukuwa mzuri kwa upande wao na nafasi iliyopo anaona lolote linaweza likatokea endapo wakishindwa kupata matokeo katika mechi mbili zilizosalia dhidi ya Fountain Gate na Tabora United.

“Tupo nafasi ya tisa kwa pointi 31 lazima tushindi mechi zilizobakia ili tuwe na uhakika wa kutokucheza mtoano (playoff), ndiyo maana nimesema lolote linaweza likatokea,”alisema.

Katika mechi 28 Coastal imeshinda saba, sare 10, imefungwa 11, ina mabao ya kufunga 24, mabao ya kufungwa 30 ina pointi 31.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *