Kinachojadiliwa Kamati Kuu Chadema hiki hapa

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), inakutana katika kikao maalumu kikiwa na ajenda mbalimbali, ikiwemo uteuzi wa wakurugenzi, makatibu wa kanda, na taarifa ya utekelezaji wa ‘No Reforms No Election’.

Ajenda hizo zimeanza kujadiliwa katika kikao hicho kilichoanza leo Jumatatu, Machi 10, 2025 na kinatarajiwa kuhitimishwa kesho Jumanne, makao makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kimeanza kwa kuongozwa na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Mzee Said, hadi alasiri alipoingia Mwenyekiti, Tundu Lissu, akitokea kushiriki mazishi ya Profesa Philemon Sarungi.

Lissu aliambatana na Makamu wake -Bara, John Heche, kushiriki hafla ya kuaga mwili wa kiongozi huyo iliyofanyika  katika viwanja vya Karimjee, kisha maziko kufanyika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Taarifa za kikao hicho, imetolewa asubuhi ya leo Jumatatu na Msaidizi wa Kurugenzi ya Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, Apolinary Margwe, ikisema kikao hicho kitafanyikia makao makuu, Mikocheni.

Taarifa hiyo ilieelza pamoja na mambo mengine, kitajadili masuala mbalimbali, ikiwemo usaili wa wagombea katika kanda ya Unguja. Kanda hiyo ni sehemu ya kanda 10 za Chadema, ambazo nyingine tisa zimeshamaliza uchaguzi wake.

Licha ya taarifa hiyo kuishia hapo, taarifa ambazo Mwananchi limezipata kutoka miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu, ajenda inayosubiriwa kwa hamu ni uteuzi wa wajumbe wa sekretarieti, ambao ni wakurugenzi wa idara.

Hii inatokana na wajumbe waliokuwapo baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa ndani Januari 21, 2025 kujiweka kando na wengine walijiuzulu. Hiyo inaelezwa uongozi mpya wa Lissu unataka kusafisha utawala wa mtangulizi wake, Freeman Mbowe kwa kuingiza sura mpya.

Katika kurugenzi tano za Chadema, tayari imeshajazwa nafasi moja ya uchumi na fedha, huku kurugenzi nyingine za sheria na haki za binadamu, mawasiliano, itifaki na mambo ya nje, uchaguzi, na ile ya ufuatiliaji na tathmini zikiwa wazi.

Wakurugenzi hao wanapatikana kwa Lissu kushauriana na Katibu Mkuu, John Mnyika, kuwasilisha majina wanayoona yanafaa ili Kamati Kuu iweze kuwateua.

Kumekuwa na mvutano kati ya kambi ya Lissu na Mbowe. Wapo wanaotaka iwe mseto, kwa maana ya mchanganyiko, kutokana na kambi hizo zote kuhitajiana kuliko kambi nyingine kuwekwa kando, hali inayoweza kusababisha kurudi nyuma hasa ikiwa kambi fulani itaachwa.

Mbali na hilo, Mwananchi limedokezwa ajenda nyingine ni uteuzi wa makatibu wa kanda. Chadema ina kanda 10 na uteuzi huo ni mwendelezo wa mabadiliko ya uongozi ulioanzia ngazi ya Taifa kwa Lissu kushika usukani, hivyo inaelezwa ana panga-pangua.

Kikao hicho pia kinakwenda kujadili utekelezaji wa sasa wa kampeni yao ya ‘No Reform No Election’, kwamba kama hakutakuwa na mabadiliko ya kimfumo, hakutakuwa na uchaguzi. Lissu amekuwa akisistiza hilo wanakwenda kulitekeleza kwa kuwaomba wananchi kuwaunga mkono ili kuwa na chaguzi huru na za haki.

Aidha, kikao hicho kitapokea taarifa za kampeni yao ya kuchangisha fedha kutoka kwa wananchi ‘tone tone’ ili kuendesha shughuli za chama, hususan mikutano ya hadhara. Pia, watajadili kauli mbiu ya ‘Strong Together’ yenye lengo la kutibu majeraha yaliyotokana na minyukano ya uchaguzi.

Lissu, katika mahojiano na Mwananchi hivi karibuni, alisema jukumu hilo la kutibu majeraha limepewa Baraza la Wazee la chama hicho (Bazecha). Mwenyekiti wa baraza hilo, Susan Lyimo, alipozungumza na Mwananchi alisema wameshaanza kulifanyia kazi.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa kikao hicho kitajadili rasimu ya sera ya jinsia na ujumuishaji na mkakati wa wanawake ndani ya chama hicho.

Mwisho wa kikao hicho, kesho Jumanne, kutatua fursa kwa wajumbe wa Kamati Kuu kushiriki mafunzo kwa siku mbili, kuanzisha Machi 11-12, 2025 yatakayofanyikia makao makuu ya chama hicho, yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kiuongozi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *