Kinachoendelea kuhusu dhamana ya mwigizaji Nicole, mwenzake

Dar es Salaam. Mwigizaji,  Joyce Mbaga (32) maarufu Nicole Berry na mwenzake Rehema Mahanyu (31), mpaka sasa wanaendelea kusota mahabusu.

Msanii huyo na mwenzake walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni inayoketi Kinondoni, Jumatatu Machi 10, 2025, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, kutokana na kupokea amana (fedha) kutoka kwa umma bila kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kusota kwao mahabusi kunasababishwa na kushindwa kutekeleza masharti ya dhamana waliyopewa.

Licha ya dhamana yao kuwa wazi, lakini siku hiyo walishindwa kutekeleza masharti ya dhamana, wakapelekwa mahabusu hadi watakapoyatekeleza, lakini mpaka leo ikiwa ni siku ya nne bado wanasota mahabusu, huku hatima yao ikitarajiwa kujulikana Machi 24, 2025.

Wakili wao, Jeremiah Mtobesya alipoulizwa na Mwananchi leo Alhamisi, Machi 13, 2025 hatima ya dhamana yao, amesema kuwa hajui chochote.

“Ndio nimeingia Dar muda huu, nilikuwa Dodoma tangu juzi, hivyo sijui chochote kama ameshapata dhamana au laa,” amesema Wakili Mtobesya.

Amesema akimaliza mambo yake baadaye ndio atafuatilia kujua kama mteja wake amepata dhamana au laa.

Hata hivyo, mwendesha mashtaka wa kesi hiyo, Wakili wa Serikali Rhoda Kamungu amelieleza Mwananchi kuwa watuhumiwa hao bado wapo mahabusu kwani, hawajadhaminiwa.

Ingawa amesema baada ya siku ya kesi ndugu wa washtakiwa hao walikwenda mahakamani kesho yake kufanya taratibu za washtakiwa kufikishwa mahakamani ili kukamilisha dhamana kwa maelezo kuwa wameshatekeleza masharti ya dhamana, lakini waliwaeleza wasubiri siku ya kesi.

“Walikuja Jumanne kusema kwamba wametimiza masharti kwa mtazamo wao lakini tukawaambia waje tarehe ya kesi, maana hatujapata muda kukagua hizo document (nyaraka) zao, maana hatujaingia mahakamani, kwa hiyo mpaka tuingie mahakamani, amesema Wakili Rhoda.

Katika kesi hiyo Nicole na mwenzake wanakabiliwa na mashitaka matatu, wanayodaiwa kuyatenda kati ya Julai 2024 na Machi 2025 ndani ya mkoa wa Dar es Salaam.

Shitaka la kwanza ni la kuongoza genge la uhalifu, kwa lengo la kujipatia fedha, shitaka la pili ni la kupokea fedha kutoka kwa umma bila kuwa na leseni na shitaka la tatu ni kuendesha mfumo wa malipo bila kuwa na leseni ya malipo kutoka BoT.

Akiwasomea mashitaka hayo, katika shitaka la kwanza wakili Rhoda alidai kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo kwa lengo la kujipatia faida kwa kupokea amana au miamala kutoka kwa jamii bila kupata leseni.

Katika shitaka la pili, alidai kuwa kati ya Julai 2024 na Machi 2025 wakiwa eneo lisilofahamika ndani ya mkoa wa Dar es Salaam walipokea amana ya Sh185,515,000 (Sh185.51 milioni)  kutoka kwa jamii bila kuwa na leseni.

Katika shitaka la tatu, wakili Rhoda alidai kuwa washtakiwa waliendesha mfumo wa malipo bila kuwa na leseni ya malipo inayotolewa na BoT.

Hata hivyo hawakutakiwa kujibu chochote hadi pale upelelezi utakapokamilika na Mahakama hiyo kupewa kibali cha kusikiliza kesi hiyo ndipo watakapojibu kama ni kweli au si kweli.

Baada ya kuwasomea mashitaka, wakili Rhoda aliieleza Mahakama kwamba upelelezi bado haujakamilika pia hawana pingamizi ya dhamana ya mshtakiwa.

Wakili Jeremiah Mtobesya anayemtetea Nicole na Avelina Nelson anayemtetea Rehema waliiomba Mahakama itoe dhamana kwa wateja wao kwa sababu mashitaka wanayoshtakiwa nayo yanadhaminika.

Masharti ya dhamana

Hakimu Rugemalira, aliwataka kuwasilisha mahakamani pesa taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani sawa na nusu ya kiasi cha fedha kilichotajwa kwenye shitaka, kwa mujibu wa kifungu cha 148 (5) (e), cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Kwa mujibu wa kifungu hicho, pale shitaka linapohusisha fedha zinazozidi Sh10 milioni, kupata dhamana mshtakiwa anapaswa kuwasilisha mahakamani nusu ya kiasi hicho cha fedha au mali isiyohamishika yenye thamani sawa na nusu ya kiasi hicho cha fedha.

Hata hivyo kama washtakiwa ni zaidi ya mmoja basi watapaswa kuchangia kiasi sawa cha pesa.

Pia, Hakimu Rugemalira amewataka kuwa na wadhamini wawili kila mmoja, wenye barua za utambulisho kutoka serikali za mitaa na kama ni mwajiriwa awasilishe barua ya ofisi yake.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 24,2025 washtakiwa na  walirudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *