
Dar es Salaam. Upelelezi katika kesi ya kughushi wosia wa mama yao mzazi inayomkabili Nargis Omar(70) na mdogo wake Mohamed Omar(64), umekamilika.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Neema Moshi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Machi 7, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Nargis na Mohamed wanakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kughushi wosia na kuwasilisha nyaraka za uongo mahakamani na kisha kujipatia nyumba kinyume cha sheria.
Neema ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Franco Kiswaga anayesikiliza kesi hiyo.
“Kesi hii imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake umeshakamilika hivyo tunaomba Mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali (PH)” alisema Wakili Moshi.
Baada ya kueleza hayo, hakimu Kiswaga aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 22, 2025 kwa ajili ya PH.
Hata hivyo mshtakiwa Nargis, hakuwepo mahakamani hapo kutokana na kuwa mgonjwa.
Taarifa ya ugonjwa imetolewa na wakili wa washtakiwa hao, Steven Mosha.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kughushi wosia, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Julai 29, 1997 na Oktoba 28, 1998 katika Jiji la Dar es Salaam.
Alidai washtakiwa katika kipindi hicho, kwa lengo la kudanganya walighushi wosia kuwa uliandikwa na marehemu Rukia Ahmed Omar, maarufu kama Rukia Sheikh Ali, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Shitaka la pili ni kuwasilisha nyaraka ya uongo mahakamani, tukio wanalodaiwa kulitenda katika tarehe hizo jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, Nargis na dada yake huku wakijua kuwa wanadanganya, waliwasilisha wosia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakionyesha kuwa marehemu mama yao, Rukia Ahmed Omar alitoa nyumba moja kwa Nargis iliyopo kiwanja namba 35, eneo la Kariakoo na pia alitoa nyumba kwa Mohamed iliyopo kiwanja namba 60 kitalu M, eneo la Magomeni, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Washtakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana.