Kilio wananchi, madereva kero ya foleni Dar

Kilio wananchi, madereva kero ya foleni Dar

Dar es Salaam. Ukiacha wingi wa mishemishe, starehe, biashara na vituko vinavyotokana na idadi kubwa ya watu katika Jiji la Dar es Salaam, msongamano wa magari barabarani ni moja ya karaha yenye maumivu yanayogusa sekta nyingi.

Mbali na kuwa kikwazo cha kuwahi kazini, msongamano wa magari unadhoofisha uzalishaji wa nchi, unaongeza gharama za usafiri na kuathiri mazingira, kama inavyofafanuliwa na wataalamu na wadau wa sekta hizo.

Ripoti ya Traffic Time Index (TTI) ya Machi 2025 katika jiji hilo, inathibitisha msongamano wa magari ulivyo kikwazo kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za kiuchumi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, safari inayopaswa kufanywa kwa dakika 30, itafanywa kwa dakika 65 hadi 70 ndani ya Dar es Salaam kutokana na msongamano.

Ripoti hiyo imekwenda mbali zaidi na kueleza, wafanyakazi hupoteza wastani wa saa 2.5 kila siku za kazi katika msongamano. Kwa kipindi cha siku 10 za kazi, karibu siku tatu zimetumika kupigania nafasi barabarani badala ya kazi.

Siyo hivyo tu, msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam mwaka 2021, ulisababisha hasara ya Sh4 bilioni kwa siku na Sh1.44 trilioni kwa mwaka kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Mwanza-Isaka Juni 2021.

Hata hivyo, akizungumzia changamoto hiyo ya foleni, Naibu Waziri wa Ujenzi, Geofrey Kasekenya amesema tangu kuanza kwa vikao vya Bunge Dodoma mwezi uliopita hajafika jijini Dar es Salaam: “Lakini ninachojua kuna ujenzi unaendelea maeneo mengi katika Jiji la Dar es Salaam na hilo linaweza kuwa sababu.”

“Najua kuna foleni Dar es Salaam lakini sijajua kwa ukubwa gani lakini sababu zinaweza kuwa zinatofautiana, kama nilivyosema ni shughuli za ujenzi zinazoendelea maeneo mbalimbali,” amesema Kasekenya.

Aidha amesema, licha ya ujenzi kuendelea kuna namna ya kupangilia foleni ili zisiathiri shughuli za wananchi.

Hivi karibuni, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akikagua maendeleo ya ujenzi wa miradi ya barabara za mwendo jijini humo alisema kukamilika kwake kutapunguza foleni ambayo imekuwa tatizo kwa wakazi Jiji hilo.

Ilichoshuhudia Mwananchi

Sambamba na kilichoelezwa na ripoti hiyo, Mwananchi lilipita katika barabara tano za Dar es Salaam kwa nyakati tofauti, kushuhudia hali halisi ya kero ya msongamano. barabara hizo ni Nelson Mandela, Morogoro, Bagamoyo, Kilwa na Kawawa.

Katika barabara ya Nelson Mandela kutoka eneo la Uhasibu hadi Ubungo liliko Daraja la Kijazi, Mwandishi alitumia saa 2 kwa usafiri wa gari binafsi, badala ya dakika 30.

Wakati wa safari hiyo, kulishuhudiwa maeneo manne unakotekea msongamano. Upo ulioanzia mwanzoni mwa eneo la Serengeti hadi karibu na Vetenari. Kisha ukafuata katika eneo la Tazara hadi lilipo daraja la waenda kwa miguu Buguruni.

Msongamano mwingine ulishuhudiwa kuanzia eneo la Tabata Gereji, hadi External, kisha foleni iliyoanzia Mabibo Hosteli hadi Riverside.

Safari iliyoanza saa 5:07 asubuhi kutoka Uhasibu, ilifika saa 7:12 mchana Kijazi Interchange Tazara, eneo ambalo dereva wa gari hilo, Said Hamis anasema kama siyo msongamano angetumia dakika 30 au 20.

“Kutoka pale Uhasibu hadi Kijazi Interchange Tazara kwa mwendo wa kawaida wa gari binafsi haizidi dakika 15, tumetumia saa 2 kwa sababu ya msongamano,” anasema.

Ukiacha muda uliopotea, Said anasema hata kiwango cha mafuta kinachotumika kwenye safari inayohusisha msongamano huwa ni kikubwa ukilinganisha na safari isiyo na msongamano.

Hata hivyo, anaeleza msongamano katika barabara hiyo hutegemea na muda, mara nyingi nyakati za asubuhi inakuwepo kuelekea Ubungo na jioni inakuwepo kuelekea Uhasibu.

Baada ya safari hiyo, mwandishi aliifuata Barabara ya Morogoro kutoka Magomeni Usalama hadi Kimara Mwisho, safari iliyochukua saa 3 na dakika 17 kwa muda wa jioni. Hata hivyo, umbali huo iwapo kusingekuwa na hakuna foleni unaweza kutumia wastani wa dakika 15 kutoka Magomeni hadi Kimara Mwisho.

Katika barabara hiyo, kulikuwa na vipande vitano unakutana na msongamano, upo ulioanzia Magomeni Kagera hadi Manzese, kisha Urafiki hadi Shekilango, Ubungo Maji hadi Kibo, Kibo hadi Kimara Baruti na kuanzia Baruti hadi Kimara Mwisho.

Safari hiyo katika Barabara ya Morogoro, ilianza saa 12:02 jioni kutoka Magomeni Usalama na kufika saa 2:08 usiku, jambo ambalo Said anasema kuna wakati hali huwa mbaya zaidi.

Kwa mujibu wa Said, msongamano katika barabara hiyo unachochewa na wingi wa malori ambayo wakati mwingine huharibika katikati ya barabara na kuwazuia watumiaji wengine.

“Hata kutembea kwake, lori huwezi kufananisha na gari zingine, inatuumiza sisi zaidi,” anasema Said.

Kama ilivyoshuhudiwa katika barabara hizo, hali ilikuwa mbaya hata katika barabara nyingine na msongamano hasa huwa nyakati za asubuhi na jioni.

Daladala: Ni maumivu

Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema anataja matengenezo ya barabara nyingi yanayoendelea ndiyo chanzo cha tatizo.

“Mashimo ni mengi na yanaumiza zaidi magari yetu, unakuta njia inayotengenezwa ni moja na mnayopita ni hiyohiyo, inakuwa vurugu mfano barabara zenye shida Mbagala kwenda Mbezi kuanzia sokata unakuta malori yamejipanga muda wote,” anasema.

Lema anasema hali inakuwa ngumu hasa pale wanapojaribu kutumia barabara za mchepuko angalau kuwahi kufanya safari ili kutengeneza faida, lakini Polisi wanawakamata.

Kulingana na Lema, wingi wa malori ya mizigo mathalani katika Barabara ya Mandera ni sababu nyingine ya foleni. Katika barabara hiyo anasema kuna wakati huwa na mengi na mwendo wake ni mdogo.

“Hali hiyo inaleta changamoto ya foleni ilitakiwa mamlaka ziangalie namna ya kuweka sawa ikiwezekana malori yakae upande wa kulia au kushoto ili zile gari zinazotembea haraka zipewe nafasi ya kwenda,” anasema Lema.

Malori kutembea pamoja na magari yanayoweza kutembea haraka Lema anasema ni changamoto nyingine inayoathiri vipato vyao, kwani gari zinatumia mafuta mengi kwa kuwa zinaguruma muda mrefu.

“Kipindi cha mvua tunakuwa kwenye wakati mgumu zaidi hasa katikati ya mji kuna mashimo mengi na maji yakuwa yametuama inakulazimu utembee taratibu kuhofia usalama wa chombo,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, anasema ilitakiwa Serikali iruhusu watu kutumia hata njia za mchepuko zenye upenyo wa kutoka na kufika sehemu wanayokwenda bila kuathiri safari.

“Tatizo limekuwa kubwa kama ulitarajia kwa siku ufanye safari saba au sita kama kuna foleni unajikuta umefanya kwa siku safari nne na unashindwa kutimiza malengo unakuta unatoka Buguruni kwenda Mnazi Mmoja unaweza kutumia hata masaa matatu,” anasema.

Anasema kuna kipande chenye changamoto kuanzia mataa yanayotokea Vingunguti hadi Rozana unakuta makatapila yanachimba na daladala zinatakiwa kupita hapohapo.

“Siyo hivyo unakuta wafanyabiashara nao wanaendelea na shughuli zao eneo hilohilo na unakuta njia zimezuiwa kupita watu unakuta wanapanda na imekuwa ikileta shida. Huu ujenzi unaoendelea ilitakiwa itafutwe namna kuangalia njia zingine za kuzitumia,” anasema.

Anasema ujenzi unaendelea lakini hakuna barabara zinazoruhusu magari kupita na kuna baadhi ya maeneo wanaweza kupita baada ya dakika kadhaa panakuwa pamefungwa.

“Ukifika pamefungwa unaambiwa urudi tena ulikotoka, siyo siri foleni inaathiri unapotumia kuanzia saa tatu barabarani wakati ulitakiwa kutumia dakika 15. Tunashindwa kufuata ratiba kwa gari kufika kwa muda uliokusudiwa,” anasema.

Simon Devis ambaye ni kondakta wa daladala jijini Dar es Salaam, anasema pamoja na kuwepo foleni mabosi zao hawaelewi hilo, wanachokitaka ni kukabidhiwa hesabu kamili.

“Bosi wangu hesabu yake ni Sh100,000 kila siku, hata kama kuna foleni nimekosa kiasi hicho cha fedha hanielewi. Kwa hiyo tunashirikiana na dereva wangu kutafuta tunakojua sisi, wakati mwingine tunakopa ilimradi usiharibu kazi,” anasema.

Msongamano unawaathiri hata madereva wa maguta, wanaosema wanalazimika kufanya kazi chache za kupeleka mizigo kwa wateja kwa sababu ya foleni, kama anavyoeleza Hassan Hassan anayeendesha guta Dar es Salaam.

“Kukiwa na foleni utabeba mizigo awamu tatu au mbili, kwa hiyo hupati fedha nyingi, kama barabara haina foleni kwa siku unapeleka hata mara tano. Mara nyingi siku za wikiendi barabara zinafunguka,” anaeleza.

Athari kwa uzalishaji, uchumi

Msongamano unasababisha kupungua kwa ufanisi wa utendaji wa mtu mmoja mmoja kama inavyoelezwa na Mtaalamu wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Hamisi Mwinyimvua.

Kupungua kwa ufanisi huko, kwa mujibu wa mwanazuoni huyo, kunakwaza uzalishaji kwa kiwango kinachostahili na matokeo ya hilo hayaishii kwa mtu mmoja, bali Taifa kwa ujumla.

Katika ufafanuzi wake, anaeleza kunapokuwa na msongamano kama ni mfanyakazi, badala ya kutumia saa moja kutoka nyumbani hadi kufika kazini, atatumia zaidi ya muda huo.

Kitendo cha kutumia saa zaidi ya ile ambayo aghalabu huitumia kwenda kazini, muda wake wa kufanya kazi unapungua.

“Badala ya kufika kazini saa 2 asubuhi mathalan, atafika saa 4 asubuhi, maana yake atafanya kazi kwa saa chache kuliko angefika mapema.

“Kama atafanya kazi kwa saa chache maana yake uzalishaji wake utakuwa mdogo pia. Uzalishaji ambao angeufanya iwapo angefika kazini mapema hauwezi kulingana na ule atakaoufanya kwa kuchelewa,” anasema.

Msongamano pia unawaathiri wafanyabiashara ya usafirishaji wa umma kwa kuwa hawatafanya safari nyingi, ukilinganisha na ambazo wangefanya iwapo kusingekuwa na msongamano.

Dk Mwinyimvua anasema hata gharama za usafiri kwa wenye magari binafsi zinaongezeka, kwa kuwa badala ya kiasi cha mafuta ambacho angekitumia kutoka safari moja kwenda nyingine, atalazimika kutumia zaidi kwa kuwa atakuwa kwenye msongamano.

Mkazi wa Mbagala, Mariam Abdallah anasema foleni imekuwa inasababisha gharama za usafiri zinaongezeka: “Kwa sababu inakulazimu kutumia bodaboda na kuharibu bajeti. Sehemu ya kwenda Sh1,000 kwa daladala unatumia Sh3,000 au Sh5,000 hili linaathiri bajeti ya mtu kwa ujumla wake.”

Ni hatari kwa mazingira

Mtaalamu Mwandamizi wa Uchechemuzi wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Msololo Onditi anasema msongamano unaongeza uzalishaji wa gesijoto unaotokana na mafuta yanayotumiwa kwenye magari.

“Gari likisimama dakika 15 maana yake mafuta ambayo yangetumika katika safari yanakuwa yametumika eneo hilo na gesijoto nyingi inazalishwa hapo kwenye msongamano,” anasema.

Athari nyingine, anasema watu waliopo ndani ya magari kwa sababu hayatembei wanaweza kulazimika kutupa taka katika maeneo yasiyo sahihi na wakati mwingine hata kujisaidia haja ndogo.

Athari nyingine anasema, “Mfano kuna gari la taka linataka kwenda Pugu lakini limekuta foleni, linasimama taka zinanuka, nzi watasambaa, katika eneo hilo unakuta kunauzwa chakula, tayari hewa inaharibika na hatari kwa afya za watu inaongezeka,” anasema.

Hakuna njia moja kudhibiti foleni

Mbobezi wa Usafiri na Usafirishaji wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji (NIT), Dk Prosper Nyaki anasema hakuna njia moja ya kudhibiti msongamano hasa katika maeneo ya mijini.

Hilo linatokana na kile alichofafanua, msongamano huongezeka kwa kadri uchumi na idadi ya watu inavyoongezeka katika mji husika.

Katika mazingira hayo, Dk Nyaki anasema njia mbalimbali zinaweza kutumika angalau kuleta nafuu ya hali hiyo ikiwemo kuruhusu mbinu tofauti za usafirishaji wa umma.

“Kwa Dar es Salaam ilivyo sasa, kinachotakiwa kifanyike ni kuboresha usafiri wa umma, tusiangalie magari tu, tubuni njia mbalimbali za kuhakikisha watu wanatoka eneo moja kwenda lingine,” anasema.

Katika ufafanuzi wake, mwanazuoni huyo anasema Serikali inapaswa kuhakikisha siyo barabara kuu pekee ndizo zinazomfikisha mtu anakotaka, hata zile za mitaa ziwe na uwezo huo.

“Leo hii mtu akitaka kwenda katikati ya mji, isiwe lazima afike kwenye barabara kuu, zile barabara za mitaa nazo ziboreshwe kiasi cha kumfikisha mtu popote,” anasema.

Kufanya hivyo, anaeleza kutapunguza utegemezi wa njia moja kwa watu wengi, jambo linalochangia kuwepo magari mengi barabarani na hatimaye msongamano.

Kwa mujibu wa Dk Nyaki, foleni inasababishwa na wingi wa magari hasa binafsi, kukosekana kwa usafiri wa umma imara na aina ya miundombinu husika.

“Katika usafiri wa umma, ili kupunguza foleni, lazima kuhakikisha kila njia hata zile za mitaani zina usafiri wa umma wa kutosha na mtu anaweza kwenda popote, lakini barabarani tuweke taa kwenye barabara kuu, watu wakiongezeka zijengwe barabara za mzunguko kwenye makutano na zaidi hata kuongeza barabara za juu,” anasema.

Dk Nyaki anasema hayo yote yanapaswa kufanywa kwa pamoja, ili kupunguza au kumaliza msongamano.

“Dar es Salaam ina Kariakoo moja, hivyo mtu akitaka kitu fulani analazimika kwenda Kariakoo, watu wanalazimika kusongamana kwenda katikati ya Mji kufuata huduma,” anasema.

Wakati hayo yanafanyika, anasema ni muhimu kuimarisha barabara za mitaa, ili barabara kuu zisiwe njia pekee za kuwafikisha watu katika eneo fulani.

Mbali na Dk Nyaki, Dk Mwinyimvua anasema hatua za ujenzi wa miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka inaweza kuwa suluhu ya kudumu ya changamoto ya msongamano iwapo mradi huo utaendeshwa kwa ufanisi.

Anasema mabasi hayo iwapo yataendeshwa kwa ufanisi, yatapunguza idadi ya magari barabarani kwa watu kupanda mwendokasi kwenda na kurudi kutoka kazini. Magari yakipungua hakutakuwa na msongamano.

“Kama mwendokasi zote zitafanya kazi vizuri, watu hawatapoteza muda njiani, mafuta mengi na litakuwa suluhisho zuri zaidi. Barabara zikimalizika na uendeshaji wa mwendokasi ukienda vema mji utabadilika,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *