Dar es Salaam. Kiu ya wananchi kuhusu nyongeza ya mabasi yaendayo haraka katika Barabara ya Morogoro, inatarajiwa kukatwa miezi mitatu ijayo.
Hiyo ni baada ya Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) kuweka wazi kuwa, baada ya miezi hiyo mabasi yote 100 yaliyoagizwa yatakuwa nchini tayari kutoa huduma.
Taarifa hiyo inakuja katika kipindi ambacho, huduma za usafiri katika mradi huo zimekuwa zikilalamikiwa kwa uchache wa mabasi.

Kwa sababu ya hilo, abiria wamekuwa wakisongamana vituoni kwa muda mrefu bila kuhudumiwa, lakini hata mabasi yenyewe yanapakia idadi kubwa ya abiria kiasi cha kurundikana.
Katika kukabiliana na adha hiyo, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Mei 2024 ilitangaza kuruhusu kurejeshwa kwa daladala 20, ambazo kila moja ilipaswa kuwa na uwezo wa kubeba abiria 40, katika njia hiyo.
Matarajio ya mradi ilikuwa wananchi kukaa vituoni dakika chache, lakini imekuwa tofauti, kwani abiria husubiri mabasi kwa nusu saa au zaidi.
Taarifa ya ujio wa mabasi hayo miezi mitatu ijayo, imetolewa leo, Jumapili Machi 23, 2025 na Msemaji wa Udart, Gabriel Katanga akieleza kampuni hiyo inajiandaa kupokea mabasi hayo.
Baada ya taarifa yake hiyo, Katanga ameiambia Mwananchi kuwa, ujio wa mabasi hayo yatakayotumia nishati ya gesi (CNG), utatanguliwa na basi la mfano litakalowasili Aprili mwaka huu.
Amesema miezi mitatu baada ya sasa yatafuatia mengine 99 kukamilisha idadi kamili ya mabasi 100 yaliyoagizwa.
“Kwa sababu basi moja la mfano litaingia Aprili, katika 100 yatakuwa yamebaki 99 ambayo baada ya miezi mitatu yatawasili nchini,” amesema.
Amesema mabasi hayo ni kwa ajili ya kuboresha huduma za usafiri katika awamu ya kwanza ya mradi huo, inayohusisha barabara ya Morogoro na yote yatatumia mfumo wa gesi.

Awamu ya kwanza ya mradi inajumuisha barabara za Morogoro kutoka Kimara hadi Kivukoni, Kimara Gerezani na Kimara-Morocco na ilianza kutoa huduma mwaka 2016 baada ya kuzinduliwa na Rais wa wakati huo, John Magufuli.
Sambamba na hilo, Katanga amesema katika mabasi hayo mapya, kasoro iliyokuwa ikisumbua awali katika injini imetatuliwa.
“Yale ya awali kwa kuwa injini zilikuwa nyuma zilisumbua kwa sababu ya kuingia uchafu, lakini haya yanayokuja yameboreshwa, hakutakuwa na hilo tatizo, ingawa injini zake zipo nyuma,” amesema.
Alipoulizwa ni lini yataingia mengine kwa ajili ya awamu ya pili, amesema bado hana taarifa za kina kuhusu awamu hiyo kwa sababu kwa sasa wamejikita na huduma katika awamu ya kwanza.
Hata hivyo, katika taarifa yake kwa umma, amesema kuwasili kwa mabasi hayo ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma, kuondoa msongamano wa abiria na kuchangia katika uhifadhi wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya mafuta ya dizeli.
“Hatua hiyo ya kuingiza mabasi mapya inalenga kuyaondoa kwa awamu machakavu na ambayo muda wake wa kutoa huduma umekwisha, likiwemo moja ambalo hivi karibuni limeonekana kwenye mitandao ya kijamii likipitisha maji sehemu yake ya kupitishia hewa,” amesema.
Amesema hatua hiyo ya kuagizwa mabasi mapya inatekelezwa baada ya kuwepo kwa changamoto iliyosababishwa na uchakavu wa mabasi ya awali.
Katanga amesema muda wa matazamio ya kihuduma katika mabasi hayo kulingana na taarifa za mzalishaji ni miaka minane hadi 10. Mabasi ya awali yaliingizwa nchini mara ya kwanza kati ya mwaka 2015-2016.
“Tunataka kuhakikisha kuwa teknolojia ya mabasi yanayotumia gesi asilia inakidhi mahitaji ya wakazi wa Dar es Salaam, kabla ya kuanza operesheni rasmi za mabasi mapya mwaka huu,” amesema Katanga.
Walichokisema wananchi
Mkazi wa Kimara, Mariam Juma, akizungumza na Mwananchi amesema: “Sisi wananchi kwa kweli tumechoka na ahadi za kila uchwao, tunachokitaka ni kuona magari, kama kweli yanakuja yatasaidia kutupunguzia adha ya usafiri.”
“Nakumbuka tuliambiwa unakaa kituoni dakika tano tu gari imefika, lakini kwa sasa unaweza kukaa kituoni hata saa nzima, sasa hakuna maana tena ya mwendokasi,” amesema Mariam.
Mkazi wa Mbezi, Christina Mollel, hana matumaini kuhusu ujio wa mabasi hayo kutokana na kile alichoeleza, ahadi nyingi zilishatolewa lakini mabasi hayakuonekana.
Ingawa amekosa matumaini, amesema iwapo yataletwa yatasaidia kupunguza msongamano vituoni na mrundikano ndani ya mabasi unaosababishwa na uhaba wa vyombo vya usafiri.
“Kituoni unakaa nusu saa hadi saa kusubiri basi na linapita likiwa limejaa kiasi cha kukosa pa kuingia, mabasi machache abiria wengi, angalau yakiongezeka yatakidhi mahitaji,” amesema.
Mussa Salum anayeishi Ubungo, amesema angalau mabasi hayo yatapunguza adha ya usafiri kwa watumiaji wa barabara ya Morogoro.
“Tulidhani mabasi yaendayo haraka yangetuepusha na msongamano wa magari na kuchelewa kazini, lakini hali iliyopo sasa yamekuwa chanzo cha kuchelewa kazini kwa sababu hayapiti vituoni kwa wakati na hata yanayopita huwa yamejaa,” amesema.
Kwa mujibu wa Mussa, ndani ya basi moja huwa na abiria zaidi ya 200 na wakati mwingine inakosekana hewa.