Kilio cha X-Ray Mji wa Himo chamalizika, wananchi wasema…

Moshi. Wananchi wa mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro waliokuwa wakitembea umbali mrefu na kutumia gharama kubwa kufuata huduma ya X-Ray sasa imemalizika baada ya Serikali kupeleka mashine hiyo.

Mashine hiyo, yenye thamani ya zaidi ya Sh200 milioni, ilizinduliwa rasmi Machi 5, 2025 na inatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa huduma za X-ray kwa wananchi wa Himo na maeneo jirani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, wananchi hao wameishukuru Serikali kwa kutoa msaada wa Mashine hiyo ambayo itawasaidia kupata huduma hiyo kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

Aidha, wamesema awali walikuwa wakisafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo na kutumia gharama kubwa ya usafiri pamoja na za matibabu.

Edward Temu, mkazi wa Himo amesema mashine hiyo imeleta unafuu mkubwa kwa wananchi ambao awali walilazimika kusafiri kwenda hospitali za mbali na binafsi kwa ajili ya vipimo vya X-ray kwa gharama ya Sh20,000, lakini kwa sasa wataipata huduma hiyo kwa Sh10,000.

“Naishukuru Serikali kwa msaada huu mkubwa, huduma zinazotolewa hapa ni nafuu kuliko hospitali nyingine. Pia kuna mashine ya kutibu matatizo ya kinywa, lakini bado tunakabiliwa na changamoto ya wodi za wagonjwa. Tunaomba tuongezewe majengo ili huduma ziwe bora zaidi,” amesema Temu.

Rahma Msabaha, mkazi wa Lotima amesema mashine hiyo imeokoa muda na gharama za kusafiri, huku akiipongeza Serikali kwa kuhakikisha huduma hiyo inapatikana karibu na wananchi.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk Ahmed Ulimwengu amesema ujio wa mashine hiyo umeongeza idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma katika hospitali hiyo, wakiwemo wananchi kutoka wilaya za jirani zikiwamo za Rombo, Mwanga na hata nchi jirani ya Kenya.

“Kwa sasa tunahudumia wastani wa wagonjwa 10 kwa siku, lakini tunategemea idadi itaongezeka kadri wananchi wanavyoendelea kufahamu uwepo wa huduma hii. Changamoto tuliyonayo sasa ni ongezeko la wagonjwa, tunahitaji nyongeza ya wafanyakazi na miundombinu ili huduma ziendelee kuwa bora zaidi,” amesema Dk Ulimwengu.

Naye, Mbunge wa Vunjo (CCM), Dk Charles Kimei amesema mashine hiyo yenye thamani ya zaidi ya Sh200 milioni ni miongoni mwa chache zilizotolewa na Serikali katika awamu ya kwanza.

“Kituo hiki ni cha kipekee kwa sababu kinatoa huduma za kisasa ambazo si rahisi kupatikana hata katika hospitali kubwa. Tunafurahi kuona wananchi wananufaika na huduma hizi, lakini tunaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha tunapanua miundombinu ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa wanaoongezeka,” amesema Dk Kimei.