Kilio cha maji miji mitatu Mbeya, Njombe kupatiwa ufumbuzi

Mbeya. Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Rujewa (Rujuwasa), imesema kero ya maji iliyopo kwa sasa katika mji huo inatarajia kuisha ifikapo Oktoba 10, 2025 kufuatia mradi mkubwa wa maji unaojengwa hivi sasa.

Mradi huo mkubwa na wa kimkakati wa miji 28 ulianza kujengwa, Machi 2023, ambapo unatarajiwa kukamilika Oktoba 10, 2025 kwa mujibu wa mkataba na hadi sasa umefikia asilimia 22.

Hata hivyo, kukamilika kwa mradi huo utanufaisha miji mitatu ikiwa ni Rujewa wilayani Mbarali mkoani Mbeya, Wanging’ombe na Makambako ya mkoani Njombe, huku wanchi jumla ya 523,554 wakifikiwa huduma hiyo.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Februari 20, 2025 Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Lestus Linda amesema kwa sasa uzalishaji wa maji ni chini ya mahitaji kwa wananchi, ambapo kiwango cha sasa ni lita 2.4 milioni, huku mahitaji yakiwa lita 15 milioni.

Amesema kutokana na kasi ya ujenzi wa mradi huo unaogharimu Sh 50 bilioni, matarajio yao ni ifikapo Oktoba 10 wakabidhi mradi huo ili wananchi waondokane na changamoto ya maji katika miji hiyo.

“Tunatarajia kabla ya kumaliza mwaka huu, tuwe na utoaji huduma kufikia asilimia 95 kutoka 44 iliyopo kwa sasa, maji yatatoka kwa saa 24, tutaendelea kupanua mradi huu ili kuwafikia wananchi wengi,” amesema.

“Mbali na mradi huu kuna kazi nyingine zinaendelea kupitia uwekezaji wa Serikali ikiwamo mradi wa ujenzi wa tenki ya lita milioni moja, usafirishaji maji wa kilomita nne volti tano, ugawaji maji wa wananchi kilomita 10 ambao tayari unaendelea,” amesema Linda.

Mkurugenzi huyo ameongeza mkakati wao ni kuhakikisha huduma hiyo inamfikia mwananchi, huku akieleza kuwa utoaji wa sasa wa huduma hiyo haujafikia malengo akiwaomba wananchi kulinda miundombinu katika mradi huo.

Redempta Husein mkazi wa Rujewa, amesema kwa sasa changamoto ya maji ni kubwa katika maeneo mengi akieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaondoa kero za kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.

“Maji ndio maisha ya mwanadamu, bila hiyo huduma hatuwezi kufanya kazi yoyote, niombe mradi huo uendelee kusimamiwa ipasavyo tuweze kupata kile Serikali imekusudia, tunaomba kasi iongezeke,” amesema Redempta.

Theophili Njavike amesema mradi huo wanautolea sana macho kuwa sehemu ya mkombozi katika kumaliza kero ya maji, akieleza kuwa kwa sasa kiu yao ni kuona huduma ya maji ikiwafikia nyumbani.

“Tunashukuru kwa mradi huo na tunauona ukiendelea, kimsingi kasi iongezeke badala ya Oktoba ikiwezekana tupate huduma hata Juni kama vifaa na fedha vipo, maji ndio msingi wa maisha kwa binadamu,” amesema Njavike.