Kilio cha fidia uharibifu wa wanyama chapata jawabu

Lushoto. Kilio cha fidia kwa wananchi wanaoathiriwa na wanyamapori kimesikika, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza kanuni zake ziangaliwe upya.

Kuangaliwa upya kwa kanuni hizo kwa mujibu wa mkuu huyo wa nchi, kunalenga kuzifanya ziwezeshe utoaji fidia utakaolingana kiwango cha madhara anayosababishiwa na mwananchi.

Agizo hilo la Rais Samia, linafuta machozi ya wananchi wanaoishi maeneo yanayokaribiana na hifadhi na yale yenye wanyama waharibifu, wakiwemo tembo wanaoharibu mazao hasa mahindi.

Kilio hicho hasa kilitokana na madai kuwa, fidia zilizokuwa zinatolewa hazikuendana na ukubwa wa madhara wanayosababishiwa wananchi hao na wanyama katika mazao au mali zao.

Sambamba na agizo hilo, Rais Samia ameeleza kuwa Machi 6, mwaka huu itatangazwa zabuni ya kumpata mkandarasi atakayejenga barabara ya Soni-Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga.

Baadhi ya wananchi wa wilayani Lushoto wakimskiliza Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza katika muendelezo wa ziara yake mkoani Tanga.

Rais Samia  ameyasema hayo leo, Jumatatu Februari 24, 2025 alipowahutubia wananchi wa Lushoto katika mkutano wa hadhara ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku tisa aliyoianza jana  mkoani Tanga

Amemwagiza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana kuangalia upya kanuni za fidia ili zikitoka angalau zimlinde mwananchi kwa uharibifu atakaosababishwa na wanyama.

“Namwagiza Waziri wa Maliasili na Utalii (Dk Pindi) aone uwezekano wa kufanya mapitio ya kanuni za fidia kwa wale wanaoingiliwa kwenye mashamba yao,” amesema Rais Samia.

Mkuu huyu wa nchi, amesema kuangalia upya huko, kunalenga kuona fidia inayolipwa inalinda vipi jasho la mwananchi, baada ya kuharibiwa mazao yake.

Rais Samia ametoa agizo hilo, akimjibu Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi aliyetaja kuwepo kwa tembo ni moja ya changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo.

“Mheshimiwa Rais (Samia), tunayo tarafa ya Umba ambayo ina changamoto ya ndovu (tembo), kama ilivyo maeneo mengine, tunapambana nao kwa njia zote za kimila, lakini wametushinda tunaomba utuongezee bajeti katika eneo hilo ili angalau tuweze kukabiliana nao,” amesema Shangazi.

Samia amesema anafahamu kuwepo kwa wanyama waharibifu na kwamba Serikali imekuwa ikichukua hatua za kuwalinda wananchi kwa kuongeza askari wa wanyamapori na kutumia ‘drones’ ndegenyuki.

Amesema wataendelea kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha wananchi wanalindwa dhidi ya wanyama hao.

Ujenzi barabara

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Machi 6 mwaka huu, mchakato wa  zabuni utafunguliwa kutafuta mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 22 za barabara kuanzia Soni hadi Bumbuli kisha kilomita tisa.

Amesema barabara hiyo inajengwa baada ya kuombwa kwa muda mrefu na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba na sasa kibali cha utekelezwaji wake kimetolewa.

Sambamba na hilo, Rais Samia  amesema barabara ya Bagamoyo-Pangani-Tanga zinajengwa na hivi karibuni atakwenda kuweka jiwe la msingi, hivyo kuifungua Tanga na Pemba ili kurahisisha biashara.

Lushoto yamwagiwa sifa utunzaji mazingira

Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia ameisifu Lushoto kwa utunzaji wa mazingira, akisema ukiingia katika eneo hilo hata uvutaji wa hewa unakuwa mwepesi.

Ameitaka wilaya hiyo kuzifunza nyingine na yenyewe iendelee na juhudi hizo.

Amesema ziara yake mkoani Tanga inalenga kwanza, kuwaona na kuwasalimia wananchi, kadhalika kuangalia matumizi ya fedha zinazopelekwa kuondoa shida za wananchi.

“Sitaki nilaumu nataka niseme kwa kiasi kikubwa jana na leo, nimeona fedha zimetumika vizuri,” amesema.

Amesema dhamira ya jengo la halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli alilolizindua ni kuhakikisha huduma zote za wananchi zinatolewa katika eneo hilo.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa wilayani Lushoto katika muendelezo wa ziara yake mkoani Tanga.

Amewataka wananchi walitumie jengo kwa huduma wanazozitaka, huku akisisitiza uzuri wake uendane na ubora wa huduma watakazopewa wananchi.

Rais Samia amesema majengo ya namna hiyo 122 yamejengwa katika halmashauri mbalimbali nchini.

Pia, amezungumzia mradi wa Bwawa la Umwagiliaji  la Mkomazi, akisema  kwa muda mrefu umekuwa ukisuasua na sasa Serikali imeamua kuutekeleza.

Katika mradi huo, Rais Samia amesema bwawa kubwa linajengwa kuhakikisha maji kwa ajili ya matumizi ya wanyama na binadamu yanapatikana.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa amesema mradi wa Mkomazi ulibuniwa zaidi ya miaka 50 iliyopita ukitarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya 20,000 kutoka kata saba za Mkomazi, Mkumbara, Mazinde, Mombo, Chekelei, Makuyuni na Magila Gereza.

Mradi huo, amesema unagharimu Sh18 bilioni na utahudumia vijiji 28 katika kata saba katika wilaya ya Korogwe.

Ameongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika Agosti 2025, ukihusisha ujenzi wa tuta la udongo la kuzuia maji, barabara kuelekea eneo la mradi na ofisi ya meneja wa mradi.