ILI kutinga nusu fainali Simba inahitaji ushindi wa tofauti ya mabao matatu Kwa Mkapa Jumatano ijayo baada ya kufungwa 2-0 ugenini dhidi ya Al Masry katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa usiku wa Jumatano hii.
Mashabiki wa Simba wamesema “tutakutana kwa Mkapa” huku kiwango cha mechi yao iliyopita ambayo licha ya kufungwa 2-0 kiliwapa matumaini kwa jinsi timu ilivyotawala mchezo kwa takwimu zote, huku jambo moja pekee ambalo halikwenda vyema ilikuwa ni kuutumbukiza mpira nyavuni tu.
Wanamsimbazi wanaamini katika mechi ya Dar es Salaam, jambo hilo halitaachwa lijitokeze tena nyumbani kwa sababu “Kwa Mkapa Hatoki Mtu.”
Kiujumla Simba ilipiga mashuti 18 kwa saba ya wenyeji Al Masry na kutawala mpira kwa asilimia 51 kwa 49 za wenyeji ambao walipata bao la pili la dakika za jiooni liliamuliwa kwa VAR.

SIMBA ILIKOSEA HAPA
Kitu cha kwanza ni kushindwa kuwa makini zaidi katika zile dakika 20 za kwanza ambazo Mwanaspoti ilikujuza mapema kwamba ndizo zinaweza kuamua mchezo na kweli ikawa hivyo kufuatia wenyeji Al Masry kufunga bao la kwanza dakika ya 16.
Bao hilo lililofungwa na kiungo mshambuliaji raia wa Algeria, Abderrahim Deghmoum dakika ya 16, mfungaji alitumia udhaifu wa wachezaji wa Simba waliojisahau katika kukaba na kuachia shuti kali la mguu wa kushoto nje ya 18 akitumia pasi ya Youssef Ismail Omar El Farouk El Gohary, kipa Moussa Camara akashindwa kudaka licha ya kuugusa mpira huo uliodunda mbele yake kabla ya kujaa nyavuni.
Katika kuonyesha Al Masry walikuwa makini sana na nguvu kubwa kwenye dakika 20 za kwanza, walipiga mashuti matatu moja likilenga lango na kuwa bao, huku Simba ikipiga shuti moja pekee ambalo lilitoka nje. Kwa upande wa umiliki wa mpira, Al Masry walikuwa na asilimia 53 dhidi ya 47 za Simba huku Waarabu hao wakiotea mara moja wakionyesha njaa ya kwenda kushambulia lakini hawakuwa na kona, Simba wakiwa hawajaotea na kupata kona moja ndani ya muda huo.
Baada ya hapo, Simba ikaamka na kujibu mashabulizi ambayo hata hivyo dakika 45 zilimalizika Al Masry ikiendelea mapumziko kwa kuongoza bao 1-0.
Katika dakika hizo 45 za kwanza, Al Masry ilitawala mchezo kwa asilimia 51 dhidi ya 49 za Simba, lakini Simba ikaongoza kwa mashuti ikipiga 6 na mawili yakilenga lango wakati Al Masry ikipiga matatu na moja likizaa bao. Hata hivyo, John Okoye Ebuka aliyeingia kipindi cha pili, aliongeza bao la pili dakika ya 90+2.

Jambo la pili lililoiangusha Simba ni namna ambavyo Al Masry waliingia na mfumo wa 3-5-2 ambao uliwapa nguvu kubwa ya kufanya mashambulizi ambayo yalizaa bao lao kwani nyuma iliwaweka mabeki watatu ikiwatumia Khaled Sobhi na Baher El Mohamady ambao kiasili ni eneo lao, akaongezwa Mahmoud Hamada ambaye yeye ni kiungo mkabaji aliyechezeshwa beki.
Mbele yao kulikuwa na wachezaji watano wakiwemo mabeki wa pembeni Ahmed Eid (kulia) na Amr Saadawy Salem Ismail (kushoto) waliokuwa na jukumu la kuongeza namba wakienda kushambulia na kufanya hivyo wakiwa wanashambuliwa, huku Mohamed Makhlouf na Youssef Ismail Omar El Farouk El Gohary wakicheza kiungo cha kati.
Idadi ya wachezaji hao watano wa katikati, iliwafanya Al Masry wakienda kushambulia wanakuwa saba, na wakirudi kukaba wanakuwa nane wakiwanyima Simba utulivu mkubwa, wakafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Mshambuliaji wao kinara, Fakhereedine Ben Youssef alisimama juu na Salah Mohsen ambao walikuwa pia na jukumu la kuutanua uwanja na kuwafanya wachezaji wa Simba eneo la ulinzi kuvutika na kuacha nafasi kubwa kati.
Hata bao walilofungwa, mpira uliokuwa pembeni, uliwafanya wachezaji wa Simba kuvutika upande mmoja, haraka El Gohary akaurudisha kati kwa mfungaji Deghmoum ambaye hakuchelewa kufanya uamuzi.
Mfumo wa 3-5-2 unatoa faida ya kumiliki eneo la kiungo na msingi thabiti wa ulinzi wenye mabeki watatu, na uwezo wa kushambulia kupitia mabeki wa pembeni.
Hata hivyo, Simba walishindwa kutumia udhaifu wa mfumo huo kwani hawakuwa na wachezaji wengi wenye uwezo wa kufanya uamuzi wa haraka zaidi ya Kibu Denis na Elie Mpanzu, lakini kama wangekuwa na nyota wengi wenye uwezo huo, wangewapa shida Al Masry kwani wakati mabeki wao wa pembeni wakiwa wamepanda, wao wangeanzisha mashambulizi ya haraka.
Lakini Simba nao walioingia na mfumo wa 4-5-1, Kocha Fadlu Davids alitaka kujilinda kwanza, kisha kushambulia lakini mfumo huo ulimfanya mshambuliaji Leonel Ateba kuwa na kazi kubwa sana akizungukwa na mabeki watatu, huku eneo la kiungo pia idadi ikilingana hivyo kuwanyima Simba kuandaa mashambulizi mengi ya maana kipindi cha kwanza.
Wakati kipindi cha kwanza Al Masry wakitumia vizuri kupata bao moja, Simba ilishindwa kutumia cha pili kwani walifanya mashambulizi mengi hatari langoni mwa wapinzani wao.
Kipindi hicho cha pili, rekodi zinaonesha Al Masry hawapo vizuri sana kwani tangu hatua ya makundi walishindwa kucheza kwa kiwango kikubwa.
Udhaifu wao huo katika kipindi cha pili, uliwafanya Al Masry kubadili mbinu kwa kucheza kwa kujilinda zaidi wakikumbuka kwamba wakizubaa tu wapinzani wao watasawazisha, hata hivyo, mashambulizi machache yakawapa bao la pili.

Al Masry ambayo hadi inafika hatua ya robo fainali, ilikuwa imefunga mabao saba kwenye makundi ambapo sita yote yalipatikana kipindi cha kwanza na moja cha pili, huku mabao manne waliyoruhusu, yalitokea kipindi cha pili ambacho Simba ilishindwa kukitumia vizuri licha ya wao rekodi kuwa nzuri kwao.
Baada ya mchezo huu, marudiano ni Aprili 9 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar ambapo mshindi wa jumla atacheza nusu fainali dhidi ya Zamalek au Stellenbosch ambao mechi ya kwanza wametoka 0-0.
KIKOSI SIMBA: Camara, Kapombe, Mohamed Hussein, Karaboue, Hamza, Ngoma, Kagoma, Denis, Ahoua, Elie Mpanzu na Leonel Ateba.