Dar es Salaam. Juzi kati wakati nipo kwenye harakati za mtu mweusi nikazama chimbo moja hivi ninalopenda kutembelea mara kwa mara.
Nikaagiza maji ya baridi, ile natupia fundo la kwanza kooni nikipepesa macho huku na kule, ghafla nikamuona nyota mmoja mkubwa wa muziki wa Hip-Hop hapa nchini akiwa amekaa pekeyake akitumia kimiminika kama ninachotumia mimi, isipokuwa kwenye meza yake kulipambwa na miwani kubwa nyeusi (wanaziita miwani za jua).
Ile narusha macho taratibu kutazama vizuri kama ninayemuona ndiye, nikagundua hata yeye alikuwa akinitazama. Mara ghafla akachukua miwani iliyokuwa juu ya meza akaivaa. Mkasa huo ukanikumbusha staa mmoja wa Bongo Fleva aliyegoma kupiga picha na mashabiki hadi apatiwe miwani aliyokuwa ameiacha kwenye gari ili aivae.

Niliyoyaona nikayapuuzia. Wakati naendelea kugonga kimiminika nilichoagiza kwa pesa yangu niliyoipata kwa mbinde, huku nikiperuzi na kudadisi kwenye mitandao ya kijamii, nikajikuta nimezama kwenye ukurasa wa Instagram wa Diamond Platnumz ambako nako niligundua kitu kingine.
Kwenye ukurasa wa nyota huyo niliona kumechapishwa jumla ya maudhui 8576, lakini nikatupa jicho haraka nikagundua kati ya picha ishirini za juu alizochapisha, 15 alipiga akiwa amevaa miwani huku tano tu ndiyo akiwa ameachia macho yake.
Ndipo akili ikanicheza nikafanya kama mchezo nikazama kwenye kurasa mbalimbali nyingine za mastaa nikagundua wengi wao wamekabidhi macho yao kwenye miwani hasa ya rangi nyeusi bila kujali wapo katika mazingira gani.
Wakati natafakari hilo ndipo likaja swali kichwani mwangu kwanini watu maarufu hupendelea zaidi kuvaa miwani.
Akizungumza na Mwananchi, mtayarishaji wa muziki nchini, S2kizzy anasema kuna nguo ambazo huwalazimisha kuvaa miwani ili kwenda na fasheni.

“Ingawa zipo ambazo hata usipovaa miwani zinapendeza. Miwani inasaidia kwenye confidence (kujiamini). Unajua siyo kila mtu anataka kumuangalia mtu sura au macho, unaweza kuwa unaangalia kitu au unamuangalia mtu na asijue kama unaangalia.
“Inakufanya baadhi ya vitu uvifanye kwa kujiamini na kuwa huru kufanya kitu bila mtu kugundua. Unaweza kuona miwani kama ya jua kumbe ndiyo fasheni yake,” anasema.
Anasema katika dunia ya sasa watu wengi hupendelea kuvaa miwani ili wapate mwonekano bomba na kuzuia aibu.
Mbali na mkali huyo aliyehusika katika uzalishaji wa ngoma kali kama Komasava ya Diamond, naye mbunifu wa mavazi Ally Remtullah anasema zamani miwani nyeusi zilikuwa zinavaliwa kwa lengo la kulinda macho dhidi ya jua lakini kwa sasa imekuwa tofauti.

“Sasa miwani za jua zimekuja tofauti zinavaliwa kama fasheni. Unakuta mtu anataka mwonekano wake uwe tofauti na wengine, kwa hiyo mara nyingi watu wanavaa miwani hata usiku kulingana na mwonekano.
“Kuhusu kuvaa miwani kwa sababu ya kujiamini ni kama msichana akivaa high heels (viatu virefu), akitembea jukwani confidence (kujiamini) yake inakuwa juu kwa sababu anajiona mkubwa kuliko wenzake. Sasa miwani ya jua ni urembo,” anasema.
Ally anasema watu wengi maarufu wanavaa miwani kwa lengo la kujibadilisha ili waonekane tofauti.
“Mtu anapotaka kununua miwani anatakiwa azingatie umbo la sura yake kwani kuna aina nyingi. Mtu akiwa na sura ndogo hatakiwi kuvaa miwani kubwa kuficha sura nzima. Na mtu akiwa na sura pana hawezi kuvaa miwani ndogo inayokuwa imetokeza puani, kila sura ina shape yake na size ya miwani.
“Sasa hivi naona wasanii wetu wanajitahidi sana kupendeza, kuonekana tofauti lakini mara nyingi celebrities (watu maarufu) wa Tanzania wanadhani wakivaa vitu vingi ndiyo wanaonekana tofauti. Wakati saa nyingine kitu simpo huwafanya waonekane wa kipekee,” anasema Ally.

Kwa upande wa mwanamuziki Dully Sykes anasema miwani zipo za aina nyingi kama vile za jua, tiba na hata za fasheni.
“Wengine hupendelea kuvaa miwani, mtu kama Chid Benz yeye hupendelea na mimi pia huwa napenda miwani. Lakini napenda za fasheni, inaweza ikawa nyeusi ya laa lakini navaa wakati wa kwenda kupafomu, wakati mwingine navaa kwa sababu ya kumechisha na mavazi.
“Kwa watu wengine miwani inawatoa aibu lakini kwa mimi hapana, kwa sababu muziki ni kazi yangu kwa hiyo siwezi kusema naona aibu kufanya kazi yangu, kwa kuvaa miwani nijifiche kutoona watu sitofanya kazi kwa weledi,” anasema.
Anasema anapotaka kununua miwani kuna vitu anazingatia.
“Lazima niangalie yenye fremu nzuri, kioo kizuri kama inaweza kuwa na rangi mbili au moja maana siku hizi kuna miwani ambayo tunaweza kuvaa mpaka usiku.
“Unaweza kuiona nyeusi lakini kumbe sio. Sisi sehemu ambazo tunapenda kwenda zina mataa mengi. Unajua taa za kwenye shoo zinaweza kuathiri mpaka ubongo kwa hiyo kuvaa miwani nyeusi kwa wasanii husaidia kuepuka matatizo kama hayo,” anasema Dully.

Hata hivyo tovuti ya Carfia imetaja sababu nyingine za watu maarufu kupendelea kuvaa ikiwemo kujificha kwa lengo la kutotambulika. Wanataja njia hiyo kuwa bora zaidi kwa kujikinga dhidi ya macho ya watu wengi hasa katika maeneo ya umma.
Kutokana na watu hao kuandamwa na kamera katika maeneo mengi wanayokatiza, miwani hizo zinatajwa kugeuka kinga dhidi ya mwanga wa kamera.
Licha ya hayo safari za mara kwa mara na kufanya kazi kwa muda mrefu ambao huweza kusababisha uchovu, miwani nyeusi hutumika kusaidia kuficha nyuso za uchovu kwa mastaa hao.

Utakumbuka mtindo huo siyo kwa wasanii wa Bongo tu kwani hata mwanamuziki wa Uingereza, Elton John ambaye mara zote huonekana akiwa amevalia miwani amewahi kueleza kuwa alianza kuvaa miwani alipokuwa na umri wa miaka 13 ili kujifananisha na Buddy Holly. Lakini baada ya miezi 18, aligundua kuwa hawezi kuona bila miwani.
Pia mwanamuziki Rihanna amewahi kusema anapenda kuvaa miwani kama mtindo wake na inamsaidia kuficha baadhi ya mambo yake binafsi, kama vile hisia za uchovu au kukosa mood ya kukutana na paparazi. Kwa Rihanna, miwani ya jua ni kama sehemu ya kujikinga na usumbufu wa umaarufu.