MCHEZO wa fainali ya mkondo wa kwanza Kombe la Shirikisho Afrika baina ya RS Berkane dhidi ya Simba umemalizika nchini Morocco kwa wenyeji kushinda 2-0, hivyo kwa sasa ni kuuendea wa marudiano utakaochezwa Tanzania, Jumapili ijayo huku yakibainika mambo matatu yaliyoigharimu timu hiyo.
Simba inayosaka ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza, imeshuhudiwa ikipoteza mchezo wa ugenini kutokana na safu ya ulinzi kushindwa kuwa makini katika kuokoa hatari.
Hiyo ilibainika katika mabao mawili iliyoruhusu ambapo la kwanza dakika ya nane mfungaji Mamadou Camara aliruka mwenyewe kushambulia kona iliyopigwa na kuuweka mpira kimiani.
Bao la pili dakika ya 14, mfungaji Oussama Lamlaoui akiwa mbele ya walinzi watatu wa Simba, alifunga kirahisi.
Jambo la tatu wachezaji wa Simba kwa ujumla hawakuwa na uharaka katika kufika kwenye maeneo kulinganisha na ilivyokuwa kwa RS Berkane ambao wanapopoteza mpira, walikuwa wanaurudisha mapema kwenye himaya yao.
Wakati Simba ikiwa kwenye mawazo ya nini kinapaswa kufanyika mechi ya marudiano ili kubeba ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza, kuna nondo tatu za kufanikisha jambo hilo.
Kwanza Simba inabebwa na rekodi ya uwanja wa nyumbani katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu ambapo imeshinda zote sita, lakini inapaswa kuwa makini kwani Berkane mechi za ugenini za CAF ilizocheza msimu huu, imeshinda nne, sare moja na kupoteza moja, hivyo ipo vizuri nje ya nyumbani kwao.

Pia baada ya mchezo kudaiwa utachezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Simba kwao si wageni huku ikiwa na rekodi nzuri inapocheza hapo ambapo mara ya mwisho iliutumia vizuri kufuzu fainali ya michuano hiyo kwa ya kwanza ikiichapa Stellenbosch ya Afrika Kusini bao 1-0, ilipoenda ugenini ikatoka 0-0 ikawa faida kwao.
Ishu ya tatu, ni rekodi ya kuichapa RS Berkane mara ya mwisho ilipokuja Tanzania Machi 13, 2022 ambapo timu hizo zilikutana hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ikishinda 1-0 kupitia bao la Pape Ousmane Sakho, hata hivyo inapaswa kuongeza idadi ya mabao kwani wakati huo pia ilifungwa na RS Berkane idadi hiyo ya mabao ugenini. Ikienda na upepo huo wa mara ya mwisho kushinda nyumbani dhidi ya wapinzani wao hao, inaweza kuwabeba.
Mbali na hayo, wakongwe waliowahi kucheza Simba na kufundisha, wameipa Simba mbinu ya kufanya ikiwemo kucheza kwa umoja na kutumia vizuri nafasi wanazotengeneza.
Abadallah Kibadeni maarufu “King Kibadeni” ambaye wakati Simba inacheza fainali ya Kombe la CAF 1993 alikuwa kocha wa kikosi hicho, alisema ili Simba ifanye vizuri mchezo wa marudiano, wachezaji wanapaswa kutambua kiu waliyonayo Watanzania kushinda ubingwa huu.
“Kikubwa ninachokiomba kwamba wachezaji wajue Watanzania hasa wapenzi wa Simba tunahitaji kitu gani, viongozi, kocha na wachezaji wajue tuna kiu kubwa tunataka kushinda, watengeneze mipango yao yote watakayoweza kupanga kuhakikisha tunataka tusheherekee kikombe hapa nyumbani,” alisema Kibadeni.

Kibadeni ambaye mbali na kuwa kocha wa Simba, pia amewahi kuichezea timu hiyo ambapo ameendelea kwa kusema kikosi alivyokiona kipo vizuri.
“Sasa hivi ukitazama utaona timu iko vizuri, upande wa nyuma kwa kipa na walinzi wake wanaocheza wako vizuri.
“Nawaona kabisa wanacheza mpira mzuri halafu wanakwenda kushambulia na nafasi zinapatikana, tunaweza kushinda.
“Wachezaji wasinyimane nafasi za kufunga, ikitokea mmoja hayupo sehemu nzuri amuachie mwenzie afunge jambo liwe rahisi,” alisema.
Naye mshambuliaji wa zamani wa Simba, Malota Soma ambaye alicheza fainali ya Kombe la CAF 1993, alisema: “Simba kocha anacholalamika kila siku ni kutokutumia nafasi, wanapata nafasi 10 wanatumia mbili, ukiangalia ni mashindano ya kutaka kufunga, wakiacha ubinafsi watavunja historia yetu.”
Beki wa zamani wa Simba, George Masatu, alisema: “Kitu pekee ambacho safu ya ulinzi ya Simba inatakiwa kuwa nacho ni kuongea, sijui shida yao hasa ni nini kwani huwa hawana mawasiliano jambo linalowagharimu.
“Kipa anatakiwa kuongea na mabeki ili kuwajulisha na wengine kuhusu mbinu za wapinzani, kwa sababu wao ndio wanaowaona jinsi wanavyowashambulia na kusogea langoni.”

Rekodi ya Simba uwanja wa nyumbani msimu huu katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika zinaonyesha ilianza kwa kuichapa Al Ahli Tripoli mabao 3-1 hatua ya pili na kufuzu makundi.
Baada ya hapo, kwenye makundi ilishinda dhidi ya Bravos ya Angola kwa bao 1-0, kisha kuikanda CS Sfaxien ya Tunisia kwa mabao 2-1 na kuilaza CS Constantine kwa mabao 2-0.
Robo fainali ikaifunga Al Masry mabao 2-0 ikafanya matokeo ya jumla kuwa 2-2 baada ya kupoteza ugenini 2-0, kisha kupigiana penalti na kushinda 4-1 huku nusu fainali ikiichapa Stellenbosch 1-0.