Kilichoiponza Kirumba chatajwa, Mtanda atoa siku saba

Baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuufungia Uwanja wa CCM Kirumba uliopo jijini Mwanza kutumika kwa mechi mbalimbali, imebaibishwa kuwa eneo la kuchezea (pitch), kukosekana kwa maji, huduma ya vyoo, kiyoyozi na upungufu wa mabenchi katika vyumba vya wachezaji (dressing room) ndiyo chanzo cha adhabu hiyo.

Hayo yameelezwa leo Machi 11, 2025 na Mratibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kituo cha Mwanza, Goodluck Nyamhandi wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alipokagua uwanja huo leo Jumanne na kujionea mapungufu yaliyopo.

Jana Jumatatu Machi 10, 2025, TFF ilivifungia viwanja vya Jamhuri (Dodoma), Kirumba (Mwanza) na Liti (Singida) kutumika kwa michezo ya Ligi kwa kukosa vigezo vya kikanuni na Sheria za mpira wa miguu kutokana na miundombinu ya viwanja hivyo kutokidhi matakwa ya kanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya leseni za klabu.

MWAN 01
MWAN 01

Nyamhandi amesema kwa mujibu wa TFF, katika vyumba vya wachezaji kuna upungufu wa mabenchi matano ya kukalia wachezaji, hakukuwa na huduma ya maji katika mchezo wa Tabora United dhidi ya JKT Tanzania, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vijana (U-20) kati ya Pamba Jiji na Azam FC mvua ilinyesha na maji kuingia eneo la vyumba vya wachezaji.

Ameongeza kuwa, katika mchezo wa Pamba Jiji dhidi ya Yanga maji yalichelewa kufunguliwa na kusababisha walinzi wa Yanga kwenda kusomba maji nje ya uwanja ili kusafisha chumba cha timu yao, huku Azam FC wakilazimika kutumia feni zao walizokuja nazo katika mchezo dhidi ya Pamba Jiji kutokana na feni za vyumbani hapo kuwa na kasi ya chini.

MWAN 02

“Azam walitumia feni zao wakidai feni za hapa hazifanyi kazi vizuri, eneo la kuchezea kuna baadhi ya maeneo siyo mazuri hasa eneo la kupigia penalti na sehemu ya makipa kuna upungufu wa nyasi. Pia eneo la jukwaa kuu (VVIP) kuna ngazi ziliondolewa wakati wa sherehe za Mwenge wa Uhuru na kusababisha watu kulazimika kusimamia kwa sababu wakikaa hawaoni,” amesema Nyamhandi.

Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi na kujionea maeneo yenye changamoto, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amewataka wamiliki wa uwanja huo kutumia siku saba kurekebisha kasoro zilizobinishwa ikiwemo kutengeneza mabenchi 10 ya vyumba vya wachezaji ili kukidhi mahitaji.

MWAN 03
MWAN 03

Mtanda amesema ni jambo la kushangaza wamiliki wa uwanja huo (CCM) kuingiza Sh10 milioni katika mchezo wa Pamba Jiji na Yanga na Sh8 milioni dhidi ya Simba lakini wanashindwa kutengeneza mabenchi na kulazimika kuwa wanaazima viti kwenye michezo mbalimbali ya ligi.

“Kwa sababu ligi imesimama wekeni nguvu zenu, kimsingi hakuna hoja kubwa labda ni kurekebisha tu madhaifu machache lakini tumepokea changamoto tutazifanyia kazi. Nawapeni siku saba kutengeneza mabenchi 10 katika vyumba vya kubadilishia nguo baada ya hapo tutakuja tena kufanya ukaguzi,” amesema Mtanda na kuongeza.

MWAN 04

“Nashukuru nimezunguka na kuona maeneo yote ya uwanja huu, nimeona kazi kubwa ambayo inafanyika, kwahiyo Meneja endelea kufanyia kazi usafi wa mazingira, nafikiri wenzetu wa Shirikisho (TFF) wameamua tu kutukumbusha.

“TFF wanapotupa maagizo hatuyakaidi, tunayatekeleza, baada ya wiki moja watakuja wakaguzi, na mimi nawahakikishia Wana Mwanza uwanja huu hauna tatizo kubwa, tutaendelea kuhakikisha unatumika.”

MWAN 05

Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba, Hassan Ally amesema: “Tumezipokea changamoto zote zilizoonekana kwenye uwanja wetu tunazifanyia kazi ili urudi katika hali nzuri zaidi. Wananchi watulie tunafanya kazi uwanja utarudi na kuendelea kutumia.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *