Kilichoiangusha Simba sasa kimehamia Yanga.

Ubao unaweza kupinduka. Namba za mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga zinashuka siku hadi siku tofauti na Simba inayoimarika kulinganisha na misimu mitatu nyuma.

Yanga wanaopambana kutetea taji lao, namba msimu huu zinawakataa ukilinganisha na watani zao Simba wanaohitaji kurudisha furaha iliyopotea kwa takribani misimu mitatu sasa. Msimu huu ni jino kwa jino kwa timu zote mbili.

YAN 02

SABABU ZA KUYUMBA

Yanga licha kushinda mechi 15 kama ilivyokuwa msimu uliopita, lakini bado rekodi zinawakataa kutokana na kushindwa kufikia kiwango walichoonesha msimu uliopita wakati kama huu, huku sababu kubwa ya hayo yote ni mabadiliko ya mara kwa mara ya benchi la ufundi.

Kinachoiangusha Yanga msimu huu hata watani zao Simba ambao wamekwama kwa misimu mitatu mfululizo wamekipitia ambapo kubwa zaidi ni kuachana na makocha ndani ya kipindi cha muda mfupi.

Yanga msimu huu wakiwa wamecheza mechi 18 za ligi na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo, imenolewa na makocha watatu. Alianza Miguel Gamondi ambaye alishindwa kuendelea baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo kati ya kumi alizoiongoza timu hiyo ambapo nane alishinda.

Kuondoka kwa Gamondi, mikoba akakabidhiwa Sead Ramovic ambaye amehudumu kikosini hapo kwa siku 81 akiongoza kwenye mechi sita na kushinda zote.

Mabingwa hao watetezi wamemsaini Miloud Hamdi, hadi sasa ameiongoza Yanga kwenye mchezo mmoja akiambulia suluhu mbele ya JKT Tanzania.

Katika hizo mechi 18, moja alisimamia kwa muda Mkurugenzi wa ufundi, Abdihamid Moallin dhidi ya Ken Gold na kushinda mabao 6-1.

YAN 01 (1)

Kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya benchi la ufundi wataalam wanatafsiri kuwa ni sababu mojawapo ya timu hiyo kuyumba na kushindwa kufikia baadhi ya rekodi zao kama walivyofanya msimu uliopita kwenye mechi 18 za kwanza.

Mabadiliko ya benchi la ufundi yanachangia kila kocha anayekuja kuingiza mifumo yake hivyo inawapa wakati mgumu wachezaji kuishika kwa haraka.

Kutokana na hilo, kocha wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Charles Boniface Mkwasa, amesema: “Kuna madhara ya kubadili benchi la ufundi, hiyo inawaondoa wachezaji kwenye ushindani kutokana na kubadili mifumo mara kwa mara lakini Yanga tayari ina wachezaji wakomavu ambao wanafahamiana kwa misimu zaidi ya mitatu.

“Mabadiliko waliyoyafanya Yanga ni eneo moja lakini kikosi ni kilekile licha ya kuongeza wachezaji wachache wapya sioni hilo likiwaondoa kwenye mbio za ubingwa kama wataendelea kupambana.”

Yanga katika misimu mitatu ya kilele chao cha furaha, imefundishwa na makocha wawili pekee ambao ni Nasreddine Nabi na Miguel Gamondi. Nabi aliyetua Yanga Aprili 20, 2021 na kuondoka Juni 15, 2023, alishinda mataji mawili ya ligi kuu, huku Gamondi akishinda taji moja la ligi akikaa Yanga kuanzia Julai 11, 2023 hadi Novemba 15, 2025.

Rekodi zinaonyesha kuwa, msimu wa 2023/24, Yanga kwenye mechi 18 walizocheza chini ya Kocha Gamondi walifanikiwa kukusanya pointi 47 wakati msimu huu wana 46 wakifundishwa na makocha watatu tofauti.

Msimu uliopita walishinda mechi 15 sawa na msimu huu, sare mbili wakati msimu huu wana moja, walipoteza mechi moja na sasa wamepoteza mbili.

Wakati katika ukusanyaji pointi ukiwaangusha, lakini upande wa mabao walifunga 42 sawa na sasa, katika kuruhusu msimu uliopita walifungwa tisa na sasa ni saba.

Msimu uliopita walicheza mechi 11 bila kuruhusu bao, msimu huu imepanda wakicheza mechi 14 bila nyavu zao kutikiswa.

Hapa tatizo la Yanga si katika kufunga mabao wala kuzuia, bali ishu kubwa ni kusaka ushindi.

YAN 03

Yanga haina mabadiliko mengi kwenye kikosi chake ndani ya misimu mitatu ukiondoa kuvunjwa kwa benchi la ufundi mara kwa mara eneo la wachezaji halijafanyiwa maboresho makubwa.

Kwa asilimia kubwa wachezaji waliotwaa mataji yote matatu ni walewale, wameondoka wachache na wameingiza idadi ndogo.

Baadhi ya nyota waliokuwa kikosi cha kwanza ambao wameondoka ni Fiston Mayele, Jesus Moloko, Djuma Shaban, Yanick Bangala, Joyce Lomalisa, huku wakiingia Prince Dube, Jean Baleke, Nickson Kibabage, Duke Abuya, Israel Mwenda, Clatous Chama, Kouassi Attohoula, Khomeiny Abubakar.

Katika kikosi cha Yanga, kuna asilimia kubwa ya wachezaji waliotumika misimu mitatu ya mafanikio ambao ni Aziz Ki, Pacome, Djigui Diarra, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Clement Mzize, Khalid Aucho ambao wanaonekana hawana mbadala sahihi wanapokosekana.

Licha ya kwamba wapo wengine wapya wamejiunga na timu hiyo akiwemo Clatous Chama, Israel Mwenda, Prince Dube na Chadrack Boka walioingia kikosi cha kwanza, wengine wanajitafuta na kutoa nafasi kwa walewale kucheza.

Hali hiyo inawafanya wachezaji kuwa na uchovu kutokana na kucheza muda mwingi kitu kilichotajwa kinawaangusha pia.

Uchovu huo wa wachezaji umekuwa ukijitokeza zaidi muda mfupi kila yanapofanyika mabadiliko ya benchi la ufundi, ilianza wakati Ramovic amekabidhiwa timu, baadaye akaiweka sawa kisha mchezo wa kwanza wa Hamdi, jambo hilo likaibuka tena.

YAN 05

UIMARA WA SIMBA

Ubora wa Simba hauwezi kuuweka kando na kushuka kwa Yanga, hii inachangiwa na namna ambavyo timu hizo zimekuwa zikishindana zaidi kwa muda mrefu kwenye ligi.

Ukiangalia kipindi cha misimu kumi sasa kuanzia 2014-2015, timu hizo mbili pekee ndizo zimebadlishana taji la ligi, Simba ikichukua mara nne na Yanga sita.

Katika msimu ambao Yanga imekuwa bingwa, ni wazi Simba haikufanya vizuri na kinyume chake ipo hivyo.

Baada ya mateso kwenye misimu mitatu mfululizo Simba msimu huu ni kama wamejipata kutokana na timu hiyo kuimarika tofauti na hapo awali.

Ukiachana na ubora walionao Simba, pia wametibu changamoto ya kubadili benchi la ufundi mara kwa mara jambo lililokuwa likiwarudisha nyuma na kujikuta wanashindwa kufikia malengo.

Simba iliyobeba ubingwa mara ya mwisho ilikuwa ikifundishwa na Kocha Didier Gomes Da Rosa ambapo hadi sasa tayari wamepita makocha wanne ambao ni Pablo Franco, Zoran Maki, Roberto Oliveira ‘Robertinho na Abdelhak Benchikha huku Fadlu Davids akipewa jukumu la kurudisha furaha.

Rekodi zinaonyesha, Simba katika mechi 18 za msimu wa 2020-2021 kama ambazo imecheza hivi sasa, ilikusanya pointi 42 zilizotokana na kushinda mechi 13, sare 3 na kupoteza mbili huku ikimaliza msimu na pointi 83.

Katika misimu mitatu ya mateso ya Simba kulipambania taji la Ligi Kuu Bara ambalo mara zote limebebwa na Yanga, timu hiyo ilikuwa haijavuka pointi 42 baada ya mechi 18 za kwanza, huku msimu uliopita ikimaliza nafasi ya tatu baada ya hapo awali misimu miwili mfululizo kuwa ya pili.

Kumaliza kwao nafasi ya tatu msimu uliopita baada ya kukusanya pointi 69, ni wazi ulikuwa msimu mbaya zaidi kwao katika kipindi cha misimu mitatu ya kutesekea ubingwa wa ligi. Hata hivyo, pointi hizo zilikuwa nyingi zaidi ya ilivyokuwa msimu wa kwanza kukosa ubingwa kwa maana ya 2021-2022 kutokana na kumaliza ligi na pointi 61 nafasi ya pili.

Katika msimu wa 2021-2022 ambao Simba iliingia kama bingwa mtetezi, mechi 18 za kwanza ilikusanya pointi 42 baada ya kushinda mechi 13, sare 3 na kupoteza 2. Mechi 12 zilizobaki baada ya hapo ikakusanya pointi 19 na kumaliza msimu ikiwa nazo 61 kwenye nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Yanga waliopata pointi 74.

Pia msimu wa 2022-2023, Simba ilimaliza ligi na pointi 73 katika nafasi ya pili, huku mechi 18 za kwanza ikikusanya pointi 41 baada ya kushinda mechi 12, sare 5 na kupoteza 1. Vigingi ilivyokuwa navyo katika mechi 12 zilizobaki iliambulia pointi 32.

Ukija msimu wa 2023-2024 ambao Simba ilimaliza nafasi ya tatu na pointi 69 sawa na Azam zikipishana mabao ya kufunga na kufungwa, mechi 18 za kwanza ilikusanya pointi 42 kutokana na kushinda mechi 13, sare 3 na kupoteza 2, kisha mechi 12 zilizofuatia ikapata pointi 27.

Wakati Simba inajitafuta, ukiondoa mabadiliko ya benchi la ufundi pia kwenye usajili misimu mitatu iliyopita waliokosa ubingwa wamesajili wachezaji wengi walioshindwa kuingia kwenye mfumo na baadae kuamua kuachana nao.

Sio wachezaji wa kigeni pekee hadi wazawa pia Simba ilipambana nao na kujikuta ikifanya uamuzi wa kuwatoa kwa mkopo huku wengine wakivunja nao mikataba, baadhi ya wachezaji ni pamoja na Nassoro Kapama, Shaban Chilunda, Abdallah Hamis, hawa ni upande wa wazawa.

Nyota wa kigeni kulikuwa na Freddy Michael, Pa Omar Jobe, Ismael Sawadogo, Babacar Sarr, Willy Onana na wengine wengi ambao waliachana nao.

YAN 04

WATATOBOA?

Kwenye mechi 12 za Yanga zilizobaki, tano nyumbani na saba ugenini hivyo wana kibarua kigumu kuhakikisha wanapindua meza dhidi ya Simba ambayo inataka kulinda rekodi yao ya kutwaa mataji mara nne mfululizo.

Michezo ya Yanga iliyobaki ni dhidi ya KMC ugenini baada ya nyumbani kushinda 1-0, Singida Black Stars (nyumbani) wakati ugenini ilishinda 1-0, Mashujaa (ugenini) huku nyumbani ikishinda mabao 3-2, Pamba Jiji (ugenini) nyumbani ilishinda mabao 4-0.

Zingine ni Simba (nyumbani) ugenini ilishinda 1-0, Tabora United (ugenini) ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza nyumbani mabao 3-1, Coastal Union (nyumbani) ikishinda ugenini 2-0.

Pia dhidi ya Azam FC (ugenini) ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 nyumbani, Fountain Gate (ugenini) ikishinda 5-0 nyumbani, Namungo (nyumbani) ina kumbukumbu ya kushinda 2-0 ugenini, Tanzania Prisons (ugenini) ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mabao 4-0 nyumbani, itamaliza na Dodoma Jiji nyumbani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mabao 4-0 ugenini.

Hata hivyo, Yanga bado haipo mbali kwenye kurekebisha pale walipoteleza kwani mechi 12 zilizobaki zenye jumla ya pointi 36, lolote linaweza kutokea ukizingatia kwamba kuna mchezo utawakutanisha na watani zao Simba, Machi 8 mwaka huu.

WASIKIE WATAALAMU

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ alisifu ushindani wa ligi, huku akiisifu Yanga kuendeleza ushindani ndani ya misimu minne licha ya msimu huu kuvunja benchi la ufundi mara kwa mara lakini bado imekuwa sehemu ya timu zinazowania taji.

“Ni kweli wamefundishwa na makocha watatu ndani ya msimu mmoja, kipi unaona kimepungua na kama wameshuka kiwango kwa kiasi kikubwa basi wangekuwa nafasi ya nne au tatu, binafsi naona bado wamepambana na wameachwa kwa pointi moja na kinara ambaye bado wana mchezo naye na michezo mingine, haipaswi kuitoa timu hii kwenye kutetea ubingwa, nafasi wanayo.

“Ninafurahi kuona wachezaji wazawa hasa washambuliaji wanafanya vizuri kwa sasa na kuzisaidia timu zao. Binafsi nawasihi waendelee kujituma na kuwa na nidhamu ili waendelee kufanya vizuri zaidi kwenye klabu zao na timu ya taifa,” alisema Mmachinga.

Kocha na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibaden alisema ushindani uliojitokeza mzunguko wa pili, unaweza kuchochea ugumu zaidi na atakayechanga karata zake vizuri kati ya Simba na Yanga atatwaa taji.

“Ligi ni ngumu, ubora wa Simba unaongeza chachu ya ushindani kwa Yanga ambayo inahitaji kufikia rekodi ya Simba kutwaa taji mara nne mfululizo, suala la ubora wa Yanga kupungua hilo silioni kwasababu inapambana na hiyo timu inayotajwa kwa ubora kwa kuachana pointi moja sio rahisi kama inavyochukuliwa, timu zote zinatakiwa kupambana, nafasi bado ipo wazi,” alisema Kibaden.