Dar es Salaam. Hatimaye mtangazaji Oscar Oscar ameingia rasmi kwenye tasnia ya muziki wa Hip-Hop. Huku akidai kilichofanya ajitose ni muziki huo kupoteza ladha.
Oscar ameiambia Mwananchi kilichomsukuma kuingia katika muziki ni kurejesha Hip Hop katika mstari wake, kama ulivyokuwa enzi za professor Jay, Sugu, Joh Makini na wengineo.

“Hip Hop imekosa maudhui na hasa kwenye miaka mitano ya hivi karibuni. Ukiwa unafuatilia muziki wetu huko nyuma wakati professor Jay, Sugu, Joh Makini kina Chid Benzi utagundua kwamba kulikuwa na muziki fulani hivi wenye maudhui ambao unaweza kusikiliza na ukaelewa wanazungumzia kitu gani.
“Kwahiyo nikisikiliza hasa kwenye Hip Hop siku za hivi karibuni sisikii. Nasikia staili tuu za kurap ambazo sio mbaya ni nzuri sana lakini nimeamua kuingia huku ili kurejesha maudhui kwa jamii waweze kusikia kujifunza, kuelimika, kuburudika na vitu vingine ambavyo ni kazi ya sanaa,”amesema
Oscar amesema tayari ana nyimbo 50 hadi sasa ambazo zimekamilika hivyo kila baada ya mwezi atakuwa anaachia wimbo.
“Sijawahi kushindwa kitu katika vitu vyote ambavyo nimewahi kufanya na sijawahi kujaribisha. Niwaambie mashabiki zangu hapa nimefika kweli kweli na nataka kuonesha mapinduzi makubwa ya kitu ambacho akijafanyika na hasa kwenye muziki wa Hip Hop.Hata ukiangalia wenzetu wanaofanya R&B na Bongo Fleva wamekwenda mbali sana hivyo na Hip Hop inatakiwa kubadilika, nipo hapa kuanzia kichwa, miguu mpaka mwili wote,”amesema

Utakumbuka Oscar ameachia wimbo wake wa kwanza unaoitwa ‘Mniombee’ akiwa amemshirikisha Joh Makini
“Joh Makini nilimtafuta kwa sababu ni rafiki yangu sana. Hakuwa anajua kama mimi najua kuimba na kurap. Nilikuwa nikienda naye studio mara nyingi sana wakati akitengeneza nyimbo zake au za Weusi. Siku nilipotaka kuanza muziki rasmi sikutaka ajue nilienda studio nikarekodi baada ya hapo ndio nikaja nikamtafuta baadaye tena nilikuwa nisharekodi nyimbo kama 10.
“Nilivyomtafuta nikamsikilizisha baada ya hapo akasema mwenyewe atanisapoti, kuanzia hapo nikamuomba kwenye nyimbo ya kwanza aweze kufanya verse ili aniongezee thamani wakati natoka kwa mara ya kwanza,”amesema
Licha ya hayo Oscar amesema awali aliwahi kuingiza mstari katika wimbo wa msanii Lady Jaydee.
“Hakuna nyimbo yoyote nimewahi kufanya huko nyuma huu ni wimbo wangu wa kwanza kwenye maisha yangu. Kuna remix special ya Lady Jaydee ‘Popo’ aliniomba nifanye verse nikafanya na ndiyo ilikuwa mara ya kwanza nikasikika hapo. Lakini kama Oscar hii ni ngoma ya kwanza kurekodi na kuiachia,”amemalizia Oscar

Hata hivyo licha ya kuachia wimbo huo Oscar ameitwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) leo Mei 22,2025 saa 5:00 Asubuhu. Hadi sasa bado haijafahamika sababu ya kuitwa kwake.