Kilichofanya Diamond apeleke gari zake Zanzibar

Dar es Salaam. Moja ya tukio ambalo limepokea maoni mengi kutoka kwa mashabiki na mastaa katika shamra shamra za ugawaji wa tuzo za Trace ni kuhusiana na mwanamuziki Diamond kusafirisha gari (ndinga) zake kutoka Dar hadi Zanzibar.

Kutokana na tukio hilo kupata maoni mbalimbali wakati alipokuwa kwenye mahojiano kwenye ‘Blue Carpet’ kwenye usiku wa Trace Awards, Diamond aliweka wazi sababu ya kufanya hivyo ni kwa ajili ya kuiheshimisha nchi.

“Unajua hii sehemu watu wanatazama so lazima ufanye uwekezaji kwa hiyo nikaona nikifanya hivi na watu wakiona inaweza kuleta heshima kwa nchi, taifa na kwenye muziki wetu.

“Mimi kinapotokea kitu napenda kufanya kitu tofauti, nikajiuliza nifanye kitu gani so nikaona miongoni wa utofauti wacha nipeleke magari kwa sababu sio kila mtu anaweza kufanya na watu sio kama hawawezi kufanya wanaweza lakini mimi nikaona wacha nifanye kitu kipya, nimeamua kufanya hivyo na nimeshukuru watu wamelipokea kwa ukubwa kama nilivyotaka,”amesema Diamond.

Utakumbuka kupitia komenti mbalimbali katika mitandao ya kijamii mashabiki walimpongeza msanii huyo kwa kutokuwa mnyonge huku wakiandika.

“ Hakuna mnyonge wamekuja nchini kwetu lazima wanyooke,” “Ili libaba limeona lipeleke utajiri wake huko”, “Nadhani Watanzania washajua ukubwa wa Diamond kwa sasa kila mtu anamuongelea yeye na tuzo zenyewe wasanii wageni wanamtaja yeye tu,”

Mbali na mashabiki kutoa komenti zao naye mwanamuziki Harmonize alifurahishwa na kitendo hicho cha Simba kusafirisha ndinga zake huku akijiuliza kama zimepaa au zimeogelea.

“Najivunia sana wewe broskizo, nadhani nimesoma zaidi kuhusu show, nawaza zimepaa au zimeogelea. Wewe ni makini sana na kweli nataka kukutana na wewe leo,” ameandika Konde Boy.

Nyota huyo anatambulika kimataifa kupitia ngoma ya ‘Komasava’ alisafirisha ndinga zake tatu ambazo ni Simba, Simba 1 na Simba 2 ambayo haiingi risasi.