Dar es Salaam. Kwa miaka mingi msanii Afande Sele anajulikana kwa uwezo wake wa kuandika na kuchana. Anajua kupanga hoja na kutengeneza picha kubwa kwa hadhira kwa kile anachozungumza katika nyimbo zake, jambo lililompatia mashabiki wengi.
Huyu ni mwasisi wa makundi ya Ghetto Boyz na Watu Pori ambayo yamewatoa vijana wengi kimuziki. Ametoa albamu, ameshinda tuzo huku akishikwa mkono na Mr II ‘Sugu’ katika safari yake ya muziki. Fahamu zaidi.

Mwishoni mwa miaka ya 1990 akiwa jeshini ndipo alipopata jina hilo la Afande Sele, hivyo ni kweli yeye ni afande kama anavyojiita. Hiyo ni tofauti na wasanii kama Inspector Haroun, Profesa Jay na kadhalika.
Wakati Mheshimiwa Temba akiondolewa JKT mwaka 2005 kutokana na kuchora tattoo mwilini, Afande Sele ni msanii mwingine Bongo aliyewahi kuondolewa jeshini kwa sababu za kinidhamu, na baadaye Temba akaja kumchana katika wimbo wake, Mwaka wa Shetani.
Wasanii wa Reggae kwa kiasi kikubwa walimvutia Afande Sele hadi kupenda muziki na hata kuiga mtindo wao wa maisha kama kufuga rasta. Miongoni mwa wasanii hao ni Bob Marley, Peter Tosh na Culture.

Vilevile aliamua kufuga rasta kutokana na kumpenda mnyama Simba na kuwa shabiki mkubwa wa Simba SC na ndio sababu ya hata kutoa wimbo wake, Simba Dume.
Kwa mara ya kwanza Afande Sele alikutana na John Dilinga ‘DJ JD’ nje ya Bongo Records na kumuomba amsimamie kimuziki. DJ JD alisita, ila baada ya kuona usumbufu wa Afande ni mkubwa akakubali na ukizingatia wanatoka mkoa mmoja, Morogoro.
Na DJ JD ndiye alimpa Profesa Jay jina hilo baada ya hapo awali kutumia jina la Nigga J tangu anajiunga na kundi la Hard Blasters Crew (HBC) mwaka 1995 akiwa kidato cha tano.
Pale Bongo Records, rapa Soggy Doggy alihusika kurekodi wimbo wa Afande Sele ‘Darubini Kali’ ambao ulifanya vizuri. Pia Soggy amehusika kutengeneza nyimbo za Ngwea ‘She Got A Gwan’ na ‘Mikasi’ akishirikiana na Mzungu Kichaa na Profesa Ludigo.

Afande Sele ndiye ni msanii wa kwanza Bongo kuujaza Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, wakati wa uzinduzi wa albamu yake ya kwanza, Mkuki Moyoni (2003). Hiyo ni sawa na Juma Nature ambaye ndiye msanii wa kwanza kuujaza ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam katika uzinduzi wa albamu yake ya pili, Ugali (2003) chini ya Bongo Records.
Kwa asilimia 90 alichoimba Afande Sele katika wimbo wake ‘Mkuki Moyoni’ ni kweli. Ni kweli baba yake alifariki dunia akiwa katika umri mdogo na mama yake akaondoka nyumbani kuanza maisha mengine jambo lililomuumiza Sele hadi kuandika wimbo huo.
Profesa Jay akiwa anashuka uwanja wa ndege akitokea katika shoo Bukoba akapokea simu ya P-Funk Majani akimuita studio ili kurekodi ngoma, Mtazamo, kufika studio akakuta Afande Sele na Solo Thang wamesharekodi sehemu yao. Basi Profesa Jay akaandika vesi yake papo hapo na kurekodi. Baada ya kumaliza Majani akamtaka tena Jay aandike kiitikio na kurekodi. Akafanya hivyo na kitu kikatoka vizuri. Awali kina Afande walimuaachia Majani jukumu hilo.
Afande Sele anaamini alishinda taji la Mkali wa Rhymes 2004 sio kwa sababu ni msanii bora wa muda wote, bali wakati huo alikuwa na ngoma kali kuliko washindani wake. Afande alikuwa anatamba na ngoma mbili, Darubini Kali na Mtazamo.

Daz Baba alisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ili kumuomba Afande Sele ashiriki katika wimbo wake ‘Elimu Dunia’ ambao ndio ulibeba jina la albamu yake ya kwanza, Elimu Dunia (2004). Sele alikubali na kazi ikatoka kali.
Ikumbukwe Daz Baba yupo katika kundi la Daz Nundaz lililoanza na wasanii watano ila baadaye walikuja kuongezeka wengine ambao waliunda makundi yao chini ya Daz Nundaz na kuwa kama familia moja. Makundi hayo ni Sewa Side na Scout Jentaz.