
SIMBA inakwenda Misri kucheza mechi ya mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry huku ikipiga hesabu ndefu za kuvuka hatua hiyo lakini inafikiria namna ya kuvuka kikwazo kikubwa kinachoweza kuwafanya kushindwa kutoboa kucheza nusu fainali.
Kikosi hicho kilichobaki pekee kikiiwakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa ngazi ya klabu msimu huu, Jumatano ya Aprili 2 mwaka huu kitakuwa Uwanja wa Suez kupambania malengo waliyofeli mara tano nyuma kabla ya kurudi nyumbani kumaliza kazi Aprili 9 pale Benjamin Mkapa.
Hii ikiwa ni robo fainali ya sita kwa Simba katika michuano ya CAF ndani ya misimu saba kuanzia 2018/2019, hakuna hata moja ambayo Mnyama alitoboa, huku kikwazo kikubwa kikiwa ni kushindwa kuzicheza vizuri mechi za ugenini. Safari hii wataweza?
Simba katika mara tano zilizopita iliyofanya kushindwa kufuzu nusu fainali kimataifa na kuishia robo fainali pekee, ni namna ya kutozicheza vizuri mechi za ugenini.
Timu hiyo ambayo hii inakuwa mara ya pili kuanzia ugenini hatua ya robo fainali, ina kumbukumbu ya kutolewa mara mbili mfululizo kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Orlando Pirates (2021–2022) na Wydad (2022–2023) tena kwa ushindi wa kufanana penalti 4-3 kufuatia matokeo ya jumla kuwa 1-1 pia mara zote.
Katika matokeo ya mechi za kwanza wakati ikipambania kufuzu nusu fainali, imeshuhudiwa Simba mara mbili wakishinda tena zote nyumbani huku moja ikiwa suluhu na mbili ikipoteza.
Mechi ambazo Simba ilionekana inakwenda kufanya maajabu katika marudiano ni ile ya kwanza ilipotoka 0-0 nyumbani dhidi ya TP Mazembe (2018-2019) lakini ikaenda ugenini ikachapwa 4-1.
Kisha msimu wa 2021–22 nyumbani iliifunga Orlando Pirates bao 1-0, ugenini ikaruhusu kufungwa 1-0 na kupoteza kwa penalti 4-3.
Pia msimu wa 2022–2023 iliichapa Wydad bao 1-0 nyumbani, ugenini ikafungwa kwa idadi hiyo ya mabao na kuondoshwa kwa penalti 4-3.
Hata hivyo, msimu wa 2020–2021, Simba ilianzia ugenini nchini Afrika Kusini na kufungwa 4-0, ilionekana kuwa na mlima mrefu wa kuupanda ambapo mechi ya marudiano nyumbani ikashinda 3-0 na kushindwa kufuzu baada ya matokeo ya jumla kuwa 4-3.
Rekodi mbaya iliyonayo Simba ya kukwama robo fainali kunamfanya Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids kukuna kichwa zaidi huku akifichua jambo akisema: “Malengo yetu ni kucheza kwa nidhamu ugenini ili kujiwekea mazingira mazuri mechi ya nyumbani.”
Fadlu alibainisha wapinzani wao wana timu nzuri na inayobadilika mara kwa mara na hilo wamelionyesha kwa mechi walizocheza kuanzia kwao Misri na ile ya kimataifa, hivyo watapambana ili kujitengenezea mazingira mazuri mechi ya marudiano Aprili 9.
Aliongeza tangu droo ya hatua hiyo ilivyopangwa walishaanza kuwafuatilia kwa ukaribu wapinzani wao na kugundua ni timu nzuri yenye wachezaji bora kutokana na ushindani waliyoonesha mwanzoni.
“Hata hivyo hii ni hatua ngumu sana, huwezi kuangalia zaidi matokeo ya nyuma ya mpinzani wako na kile alichokifanya kwa sababu ni mechi ya hesabu tofauti na makundi, unajiuliza hata zaidi ya michezo mitatu, tumejipanga kukabiliana na hali yoyote na kufanya vizuri ugenini,” alisema Fadlu.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini anakuwa wa sita kuiongoza Simba kucheza robo fainali katika michuano ya Caf ndani ya kipindi hicho baada ya Patrick Aussems (2018/2019), Didier Gomes Da Rosa (2020–2021), Pablo Franco Martín (2021–2022), Roberto Oliveira ‘Robertinho’ (2022–2023) na Abdelhak Benchikha (2023–24).
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi amesema sasa ni muda wa kuvunja rekodi hiyo mbovu ambayo imekuwa ikwatesa Wanasimba kwa muda mrefu.
Mgosi ambaye kwa sasa yupo kwenye benchi la ufundi la Simba Queens akiwa kocha msaidizi, amesema uzoefu walionao Simba katika mashindano ya Caf, ndiyo sababu ya kuiona msimu huu inavuka hatua ya robo fainali huku akisisitiza ni lazima kufanya vizuri ugenini ili iwe rahisi kumalizia nyumbani.
“Simba si wageni katika mashindano haya, ukiangalia tayari wameshacheza robo fainali tano katika kipindi cha hivi karibuni lakini inashindwa kuvuka.
“Kushindwa kuvuka siyo sababu ya kusema msimu huu itakuwa hivyohivyo, binafsi naamini safari hii mambo yanakwenda kuwa mazuri ukizingatia kwamba Simba licha ya kuwa na kikosi cha wachezaji wengi wapya lakini huko walipotoka wamekuwa na uzoefu mkubwa hivyo watafuzu nusu fainali na ikiwezekana fainali.
“Malengo ya klabu ni kuona timu inakwenda kucheza fainali msimu huu, hivyo timu haiwezi kufika huko bila ya kuanza kuvuka robo fainali, naamini kuna mipango imewekwa ya kuhakikisha hayo yote yanafanikiwa kwani hakuna anayependa kuona timu inaishia tena hatua hiyo,” alisema Mgosi.
YANGA WALIWEZAJE?
Msimu wa 2022–2023, Yanga ilifanikiwa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilikwenda kupoteza mbele ya USM Alger kwa kanuni ya bao la ugenini kufuatia matokeo ya jumla kuwa 2-2. Katika fainali hiyo, mechi ya kwanza nyumbani Yanga ilifungwa 2-1, ugenini ikaenda kushinda 1-0.
Lakini kabla ya kufika fainali, kulikuwa na hatua ya robo fainali na nusu fainali ambapo Yanga ilizichanga vizuri karata zake kwa kushinda ugenini na kulinda matokeo hayo mazuri nyumbani.
Hatua ya robo fainali kama hii ambayo Simba imefika, Yanga nayo ilianzia ugenini dhidi ya Rivers United ya Nigeria, mchezo uliofanyika Aprili 22, 2023 kwenye Uwanja wa Godswill Akpabio International. Katika mecho huo, Yanga ilishinda 2-0 kupitia mabao ya Fiston Mayele, kisha marudiano nyumbani Aprili 30, 2023 ikatoka 0-0 na kufuzu kwa jumla ya mabao 2-0.
Nusu fainali, Mei 10, 2023 Yanga ilianzia nyumbani ikicheza dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini na kushinda 2-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kisha Mei 17, 2023 ikaenda ugenini kushinda tena 2-1 na kutinga fainali.