Kikundi cha masheikh chafungua kesi kupinga kuwa chini ya Bakwata

Dar es Salaam. Kikundi cha Masheikh na Walimu wa Dini ya Uislam nchini kimefungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam kupinga sharti la kuwa chini ya usimamizi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), katika uendeshaji wa shughuli zao.

Kesi hiyo imefunguliwa na Sheikh Ayoub Salim Muinge, Sheikh Profesa Hamza Mustafa Njozi, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzao wengine tisa wakiwamo waalimu (maustaadhi) wa dini hiyo, akiwemo mwanamke pekee, Riziki Shahari Ngwali.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Msajili wa Jumuiya, Kabidhi Wasihi Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Wadhamini waliosajiliwa na Bakwata na Wadhamini wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania.

Katika hati ya madai, wadai wanapinga kitendo cha Msajili wa Jumuiya na Kabidhi Wasihi Mkuu kuwalazimisha kuwa na barua inayowatambulisha kutoka Bakwata katika kusajili taasisi yoyote.

Wakili wao Juma Nassoro amesema sharti hilo linawalazimisha wateja wake kuwa chini ya Bakwata wakati hakuna sheria inayowalazimisha waislamu wote kuwa chini ya Bakwata, ambayo yenyewe pia imesajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani na katika Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita).

Wakili Nassoro amesema kwa kuwa Bakwata imesajiliwa kama taasisi nyingine zilizosajiliwa, haina usajili wa kuwa taasisi ya kuwawakilisha waislamu wote nchini na kwamba hata Katiba yake (Bakwata) hakuna kipingele kinachobainisha ni nani mwanachama wa Bakwata.

“Kwa hiyo kuwalazimisha waislamu wote kuwa chini ya Bakwata ni kinyume na Katiba (ya Nchi). Waislamu waachwe wenyewe waamue kuwa wanataka kuwa chini ya taasisi gani, na wanapotaka kusajili taasisi yoyote ya kidini wasilazimishwe kwamba watambuliwe na Bakwata,” amesema Nassoro.

Amesema wanapaswa waulizwe wao wenyewe na kwamba kama ni lazima walete barua ya taasisi iliyosajiliwa ya Kiislamu inayowatambua, waulizwe wao wenyewe wanaotaka kusajili taasisi yao kuwa wanataka taasisi gani iwatambue.

“Lakini siyo kuwalazimisha kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa uhuru wa mtu yeyote kujiunga na jumuiya yoyote anayoitaka. Sasa huwezi kuwalazimisha wote wawe chini ya Bakwata, hiyo ni kuvunja Katiba,” amesema Nassoro.

“Kwa hiyo wamevunja Katiba, lakini pili hakuna sheria yoyote inayowataka Rita au Msajili wa Vyama vya Kijamii kuwaelekeza waislamu waende Bakwata wakalete barua.”

Hata hivyo, Nassoro amefafanua ingawa wanaowalazimisha Waislam kuwa chini ya Bakwata ni Msajili wa Jumuiya na Kabidhi Wasihi Mkuu, lakini wamewaunganisha Bakwata ili nao wapate haki ya kusikilizwa.

Pia amesema Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nalo limeunganishwa ili nalo lipate haki ya kusikilizwa kwa kuwa nalo ni tasisi yenye hadhi sawa na Bakwata.

Kesi hiyo iliyopangwa kusikilizwa na Jaji Anold Kirekiano imetajwa kwa mara ya kwanza leo Novemba 13, 2024 kwa ajili ya kuangalia kama pande zote hususan wadaiwa wameshapewa na wadai nyaraka za kesi.

Hata hivyo wakati ilipotajwa, upande wa wadaiwa waliofika mahakamani ni Bakwata na Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, lakini Msajili wa Jumuiya, Kabidhi Wasihi Mkuu na AG hawakuwepo wala wawakilishi wao.

Wakili Nassoro amesema wadaiwa wote walipewa hati za wito wa kufika mahakamani Novemba 11, 2024.

Jaji Kirekiano ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 26, 2024 itakapotajwa tena kwa ajili ya kuangalia kama wadaiwa watakuwa wameshawasilisha majibu yao ya maandishi na viapo kinzani kabla ya kupanga tarehe ya usikilizwaji kama taratibu zitakuwa zimekamilika.

Vilevile amewaelekeza wadai kuwasilisha mahakamani hapo ushahidi kuwa wadaiwa walishapatiwa nyaraka za kesi leo.