Kikao cha Taoussi, Blanco chaanza kujibu

KOCHA wa Azam FC, Rachid Taoussi, amefichua kwamba kikao alichofanya na mshambuliaji Jhonier Blanco juu ya kutathimini kiwango chake kisha kuanza kufanya mazoezi binafsi, kimeanza kuleta matumaini huku akikiri kuwa amechelewa kufanya hivyo.

Blanco huu ni msimu wake wa kwanza akiitumikia Azam aliyojiunga nayo akitokea Rionegro Aguila ya kwao Colombia. Hadi sasa amefunga mabao matatu kwenye ligi na asisti moja. 

Bao lake dhidi ya Kagera Sugar Jumamosi iliyopita, alilifunga baada ya kukaa siku 143 sawa na miezi minne na siku 23 kwani mara ya mwisho kucheka na nyavu ilikuwa Novemba 28, 2024, Azam iliposhinda 2-1 dhidi ya Singida Black Stars.

Akizungumza na Mwanaspoti, Taoussi alisema, kwa sasa anamuona mshambuliaji huyo kiwango kinaanza kukua tofauti na ilivyokuwa mwanzo huku akisema sababu ya hayo yote ni makubaliano waliyofikia katika kikao cha hivi karibuni.

“Kwa bahati mbaya sana ameanza kuonyesha makali kwenye mechi za mwisho, ila kwa upande mwingine kama ataendelea hivi basi msimu ujao unaweza kuwa bora kwake.” alisema Taoussi na kuongeza: “Alinifuata na kuniambia anataka kufanya kitu tofauti kuthibitisha ubora wake, hivyo akawa anafanya mazoezi mengi binafsi tofauti na yale ya timu.

“Blanco anajua kufunga, kama ataweza kuwa na muendelezo wa kiwango chake ataisaidia timu hii kwani kukiwa na washambuliaji wazuri wanakifanya kikosi kuwa na nguvu zaidi katika ushindani.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *