Kikao cha pili cha kamati ya pande tatu za Iran, Saudi Arabia na China chafanyika Riyadh

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Saudi Arabia na China zimefanya kikao cha pili cha pande tatu huko Riyadh, Saudi Arabia kwa shabaha ya kufuatilia makubaliano yaliyofikiwa huko Beijing na kuimarisha kiwango cha ushirikiano.

Kikao hicho kilifanyika jana kikiongozwa na Walid AbdulKarim al Khereiji, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia. Ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliongozwa na Majid Takhte Ravanchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya kisiasa, na China iliwakilishwa na Deng Li Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China. 

Takhte Ravanchi katika mazungumzo na Abdul Karim al Khereiji mjini Riyadh 

Wawakilishi wa Iran na Saudi Arabia kwa mara nyingine tena wamesisitiza ahadi zao za kutekeleza kikamilifu makubaliano ya Beijing na kuendeleza juhudi za mshikamamo wa nchi hizo kwa kuzingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa, Sheria za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuheshimu mamlaka ya kujitawala, uhuru na usalama wa nchi mbalimbali. 

Kadhalika, nchi  tatu za Iran, Saudi Arabia na China zimetaka kusitishwa mara moja hujuma za Israel dhidi ya Palestina na Lebanon na kulaani kitendo cha Israel cha kushambulia na kukiuka mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi nzima ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.