Kikao cha dharura cha Baraza la Usalama; Israel yabebeshwa lawama

Kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambacho kimeitishwa kwa ombi la Iran kwa ajili ya kujadili uchokozi wa hivi karibuni wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Tehran, kimefanyika huku Israel ikibebeshwa lawama za hali tete iliyopo hivi sasa katika eneo la Asia Magharibi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, katika kikao hicho, mwakilishi wa Algeria amelaani vikali shambulio la Israel dhidi ya Iran na kusema kuwa ni uvunjaji wa sheria za kimataifa na limehatarisha amani ya dunia nzima. 

Amesema, amani ya kweli haiwezi kupatikana duniani bila ya kuheshimiwa sheria za Umoja wa Mataifa. Lawama zote zinakwenda kwa wanajeshi vamizi wa Israel. Leo hii tunakabiliwa na vita vya eneo zima ambavyo matokeo yake hayatabiriki. 

Kwa upande wake, mwakilishi wa China amesema katika kikao hicho cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa cha kujadili mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran kwamba, Beijing inapinga shambulio lolote ambano linahatarisha amani na usalama wa kieneo. Hali Mashariki ya Kati ni tete na pande zote zinapaswa kusimamisha mapigano. Suala la kusimamishwa vita Ghaza bado liko mbali. Maazimio ya Baraza la Usalama yanapuuzwa.

Naye mwakilishi wa Russia ameshangazwa na madai ya Marekani kuwa eti haikushiriki katika shambulio la Israel dhidi ya Iran na kusema kuwa, wakati Marekani imeupa utawala wa Kizayuni taarifa zote za kijasusi; suala ambalo ni uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa, vipi hivi sasa inadai kuwa haikushiriki kwenye shambulio hilo? Hakuna jambo lolote muhimu hivi sasa kuliko kusimamishwa vita, kuanchiliwa huru mateka na kufikishiwa misaada watu wa Ghaza.