Kijiji kidogo cha India kinachodai Kamala Harris ni ‘wao’

.

Chanzo cha picha, Janarthanan/BBC

Maelezo ya picha, Bango la picha ya Kamala Harris katika kijiji cha India cha Thulasendhrapuram

Thulasendhrapuram, kijiji kidogo kilichopo karibu kilomita 300 kutoka mji wa kusini wa India wa Chennai (zamani Madras) na kilomita 14,000 kutoka Washington DC, ndipo mababu wa Kamala Harris walikotoka.

Eneo la katikati ya kijiji hicho kwa sasa limewekwa picha kubwa ya Bi Harris, 59.

Maombi maalum yanatolewa kwa mungu wa eneo hilo kwa ajili ya mafanikio yake – Bi Harris na majina ya babu zake yapo kwenye orodha ya wafadhili wa hekalu la kijiji – na pipi zinasambazwa.

Wanakijiji wamekuwa wakifuatilia kwa karibu kinyang’anyiro cha urais wa Marekani kufuatia kujiondoa kwa Joe Biden na kuibuka kwa Bi Harris kama mgombea anayeweza kuteuliwa.

“Si jambo rahisi kufika mahali ambapo amefikia katika nchi yenye nguvu zaidi duniani,” anasema Krishnamurthi, meneja wa benki aliyestaafu.

“Kwa kweli tunajivunia. Wakati Wahindi walipokuwa wakitawaliwa na wageni, sasa Wahindi wanaongoza mataifa yenye nguvu.”

Pia kuna hisia za majivuno, hasa kati ya wanawake. Wanamwona Bibi Harris kama mmoja wao, ishara ya kile kinachowezekana kwa wanawake kila mahali.

“Kila mtu anamjua, hata watoto. ‘dada yangu, mama yangu’ – hivyo ndivyo wanavyomuita,” alisema Arulmozhi Sudhakar, mwakilishi wa halmashauri ya kijiji.

“Tunafurahi kwamba hajasahau asili yake na tunaelezea furaha yetu.”

Msisimko na tamasha ni ukumbusho wa jinsi wanakijiji waliingia mitaani kwa fataki, na kubeba mabango wakati Bi Harris alipokuwa makamu wa rais.

Kulikuwa na karamu ya jumuiya ambapo mamia walifurahia vyakula vya kitamaduni vya Wahindi wa kusini kama vile sambar na idli, ambavyo kulingana na mmoja wa jamaa za Bi Harris, ni miongoni mwa vyakula anavyopenda sana kula.

Asili ya India

.

Chanzo cha picha, Janarthanan/BBC

Maelezo ya picha, Wanakijiji wanatumai maombi yao yatamsaidia Bi Harris kushinda uchaguzi huo

Bi Harris ni binti wa Shyamala Gopalan, mtafiti wa saratani ya matiti, ambaye alitoka jimbo la kusini la Tamil Nadu, kabla ya kuhamia Marekani mwaka wa 1958. Wazazi wa Gopalan walikuwa wanatoka Thulasendhrapuram.

“Mama yangu, Shyamala, alikuja Marekani kutoka India peke yake akiwa na umri wa miaka 19. Alikuwa mwanasayansi, mwanaharakati wa haki za kiraia, na mama ambaye mabinti zake wawili walijivunia ,” Bi Harris alisema katika mtandao wa kijamii mwaka jana.

Bi Harris alitembelea Chennai pamoja na dadake Maya baada ya mama yao kufariki, na kuzamisha majivu yake baharini kulingana na mila za Kihindu, kulingana na ripoti hii katika gazeti la The Hindu.

Bi Harris anatoka katika familia yenye watu waliofanikiwa kwa kiwango cha juu. Mjomba wake mama Gopalan Balachandran ni msomi. Babu yake PV Gopalan, aliinuka na kuwa afisa wa serikali ya India, na alikuwa mtaalam wa uhamishaji wa wakimbizi.

Pia aliwahi kuwa mshauri wa rais wa kwanza wa Zambia katika miaka ya 1960.

.

Chanzo cha picha, Janarthanan/BBC

Maelezo ya picha, Kijiji cha Thulasendhrapuram kiko takriban kilomita 300 kutoka Chennai

“Yeye (Kamala) amekuwa mtu maarufu kwa muda mrefu sasa. Sio kitu kikubwa cha kushangaza. Mpango huu ulikuwa ukiendelea kwa miaka mingi,” alisema R Rajaraman, profesa mstaafu wa fizikia ya kinadharia katika Chuo Kikuu cha Delhi cha Jawaharlal Nehru na mwanafunzi mwenza wa mama yake Bi. Harris.

Prof Rajaraman anasema alipoteza mawasiliano na Shyamala lakini alikutana naye tena katikati ya miaka ya 1970 aliposafiri hadi Marekani na kukutana na Bi Gopalan huko Berkeley.

Shyamala alikuwepo. Alinipa kikombe cha chai. Watoto hawa wawili (Kamala na dada yake Maya) walikuwepo. Hawakushughulika” alikumbuka.

“Wote wawili walikuwa wajasiriamali. Mama yake alikuwa na tabia ya kupenda maendeleo , ambayo pia kama yuko nayo.

Huko Thulasenhrapuram, wanakijiji wanatarajia kutangazwa kwa ugombeaji wake hivi karibuni.

“Chithi wa Kamala (dada mdogo wa mama) Sarala hutembelea hekalu hili mara kwa mara. Mnamo 2014 alitoa rupia 5,000 ($60; £46) kwa niaba ya Kamala Harris,” alisema Natarajan, kuhani wa hekalu.

Natarajan ana imani kuwa maombi yao yatamsaidia Bi Harris kushinda uchaguzi huo.

Wanakijiji wanasema wanaweza kuwa maelfu ya maili kutoka Marekani, lakini wanahisi kushikamana na safari yake. Wanatumaini angewatembelea siku moja au kijiji chao kingepata kutajwa katika hotuba yake.

Imetafsiriwa na kuchapishwa na Seif Abdalla