Kijiji cha kihistoria cha Esfahak, kilicho katika mkoa wa Khorasan Kusini mwa Iran, kimetambuliwa kimataifa kwa kutajwa na Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa kuwa mojawapo ya Vijiji Bora vya Utalii mwaka 2024.
Hadhi hiyo imeangazia mabadiliko ya ajabu ya Esfahak kutoka eneo lililoharibiwa na tetemeko la ardhi la 1978 hadi eneo linalostawi la kitamaduni na utalii wa mazingira ambalo ni mfano wa maendeleo endelevu na turathi.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Waziri wa Utalii nchini Iran, Seyyed Reza Salehi-Amiri, amesema ustahimilivu wa Esfahak na kujitolea kuhifadhi urithi wake wa kitamaduni ni mfano wa kuigwa. Salehi-Amiri amepongeza maendeleo ya kijiji hicho na kukumbatia kwake utalii endelevu.
Kijiji cha kihistoria cha Esfahak kiliharibiwa vibaya na tetemeko la ardhi la 1978 katika eneo la Tabas. Wakati huo kijiji hicho kiloenekana kama sehemu isiyoweza kuishika tena. Hata hivyo wakaazi walikijenga upya kijiji hicho na kuendelea na maisha yao ya kawaida.

Kwa kujitolea katika maendeleo endelevu na kulinda turathi za kitamaduni, wanakijiji walijenga nyumba za kulala wageni na kurejesha nyumba za kitamaduni zilizokuwepo kwa karne nyingi.
Mabadiliko ya Esfahak kuwa kivutio cha kitamaduni na utalii wa kiikolojia yamepelekea kijiji hicho kupata Tuzo ya kifahari ya Usanifu wa Asia. Leo, kijiji hicho kinavutia watalii kutoka kote ulimwenguni kutokana na usanifu majengo wa kuvutia ambao umehifadhi utambulisho wa kitamaduni.