Geita. Abrahaman Habiye, mkazi wa Mtaa wa Uwanja, Kata ya Nyankumbu mjini Geita anadaiwa kutoweka tangu Machi Mosi, 2025 alipochukuliwa na watu wasiojulikana.
Habiye (24), aliyekuwa akiuza duka la nguo la mama yake, inadaiwa alifuatwa na watu walioshuka kwenye gari jeupe aina ya Toyota Land Cruiser lenye vioo vyeusi waliojifanya wateja.
Jeshi la Polisi limethibitisha kutoweka kwa kijana huyo likisema watu wanne wanashikiliwa kuhusu tukio hilo na linaendelea na uchunguzi.

Abrahaman Habiye muuza duka la nguo anaedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana katika mtaa wa Uwanja kata ya Nyankumbu mjini Geita.
Inadaiwa watu hao walikuwa wakichagua nguo lakini ghafla walianza kumpekua kijana huyo, wakatoa simu na pochi yake, wakamfunga pingu kisha kuondoka naye.
Mariam Juma, mama mzazi wa kijana huyo akizungumza na Mwananchi amedai mchana wa Machi Mosi, 2025 akiwa safarini alipigiwa simu na mfanyakazi wake, Joseph Fabian akamweleza watu wasiojulikana wamemchukua mwanaye na kuondoka naye.
Amedai aliwasiliana na mkuu wa kituo cha polisi Nyankumbu aliyemshauri arudi Geita afungue jalada la uchunguzi.

Mariam Juma mama wa Abrahaman akiwa amesimama nje ya duka alilokua akiuza mwanae kabla ya kuchukuliwa na wasiojulikana .
Mariam amedai Machi 3, 2025 alifika na kufungua jalada kituo kikuu cha Polisi Geita.
“Mwanangu sina mawasiliano naye ni siku 10 sasa, sijui alipo. Nimezunguka vituo vyote vya polisi sijampata, naomba Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama mnisaidie nimpate mwanangu, nisaidieni nimpate hata kama ameuawa niuone mwili wake,” amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo akithibitisha tukio hilo amesema watu wanne wanashikiliwa kwa uchunguzi.
Amesema polisi wanaendelea kuchunguza ili kijana huyo apatikane.
Aliwahi kupewa vitisho

Abrahaman Habiye muuza duka la nguo anaedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana katika mtaa wa Uwanja kata ya Nyankumbu mjini Geita.
Mama wa kijana huyo amedai Desemba 15, 2024 akiwa jijini Dar es Salaam alipigiwa simu baada ya mtu (anamtaja jina) kufika dukani kwake na kudai kijana (anamtaja) ana mahusiano ya kimapenzi na mkewe na kwamba ametishia kuchoma moto duka hilo.
“Nilipopata simu hiyo niliomba nipewe namba ya huyo (anamtaja) nilitumiwa nikampigia na kumuomba asifanye chochote dukani awe na subira ili nifike tuzungumze. Nilianza safari kurudi Geita nikampigia simu akaja dukani na vijana sita wenye visu na kudai yupo tayari kumpoteza (anamtaja) kwa kuwa anatembea na mkewe.
“Vijana aliokuja nao walikuwa wamevaa makoti meusi, mmoja akinoa kisu chini akidai ametumwa kumtoa roho … na bwana … akaniambia ananipa miezi mitatu nihamishe duka au nimpoteze …” amedai.
Mama huyo amedai baada ya kupewa taarifa hiyo alimuomba ampe muda kwa kuwa ulikuwa msimu wa biashara, hivyo mtu huyo aliridhia kwa kumpa miezi mitatu akimtaka auze mali aondoke au la atachoma duka lake moto.
Amedai baadaye mtu huyo alirejea na kumtaka aseme bei ya vitu vilivyomo dukani ili amlipe aondoke akamwambia thamani yake ni Sh18 milioni.
Alimtaka asubiri mthamini wa Serikali ili afanye tathimini akitaka ampe Sh13 milioni kitendo ambacho mama huyo anasema hakuridhia.
Amedai alimtaka msimamizi wa duka lake lingine lililopo Mwanza kwenda Geita kwa ajili ya usalama.
Mariam amesema kutokana na vitisho hivyo alitoa taarifa polisi lakini hakuna aliyekamatwa wala hatua zilizochukuliwa.
Kauli ya shuhuda
Anastazia Isaka, mkazi wa Uwanja, Kata ya Nyankumbu amedai siku ya tukio akiwa dukani hapo na Abdul (mtoto wa mama huyo) alifika mteja aliyetaka suruali akaanza kuchagua lakini ghafla lilifika gari, akashuka mwanamume mrefu mweupe aliyeingia dukani kuchagua nguo.
Amedai akiwa anachagua nguo, alishuka mwingine mweusi wakaungana kuchagua lakini ghafla mmoja alianza kumpekua Abdul na kutoa simu na pochi, kisha akamfunga pingu pamoja na mteja aliyekutwa akichagua suruali dukani.
Amedai watu hao walimtaka atulie na asinyanyuke hali iliyompa mshtuko.