
Ujumbe huo unalenga kushughulikia mvutano uliozuka mwezi uliopita wakati Juba ilipomnyima ruhusa Mkongo aliyefukuzwa, Makula Kintu, ambaye pia anajulikana kama Nimeri Garang, ambaye alithibitishwa kimakosa kuwa raia wa Sudani Kusini.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Serikali ya Sudani Kusini itatuma ujumbe wa ngazi ya juu mjini Washington, D.C., ili kuharakisha kuwarejesha nyumbani raia 137 wa Sudani Kusini na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia huku kukiwa na mzozo wa hivi majuzi.
Ujumbe huo unalenga kushughulikia mvutano uliozuka mwezi uliopita wakati Juba ilipomnyima ruhusa Mkongo aliyefukuzwa, Makula Kintu, ambaye pia anajulikana kama Nimeri Garang, ambaye alithibitishwa kimakosa kuwa raia wa Sudani Kusini. Tukio hili lilipelekea utawala wa Trump kubatilisha viza zote za wenye hati za kusafiria za Sudani Kusini, na kutishia kuchukuwa hatua zaidi.
Ujumbe huo ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Marial Dongrin Ater, unajumuisha Gavana wa Benki Kuu Bw. Jonny Ohisa na Mkurugenzi Mkuu wa Usajili wa Raia, kutoa Uraia, Pasipoti na Uhamiaji, Jenerali Elia Kosta. Watashirikiana na mamlaka za Marekani ili kuhakikisha mchakato wa kuwarejesha watu makwao kwa utaratibu, kisheria na wenye heshima.
“Serikali ya Jamhuri ya Sudani Kusini inatangaza kwamba itatuma ujumbe wa ngazi ya juu huko Washington, D.C. katika siku zijazo ili kuwasiliana moja kwa moja na maafisa wa Serikali ya Marekani kuhusu suala la dharura la kuwarejesha nyumbani takriban raia 137 wa Sudani Kusini ambao kwa sasa wameagizwa kufukuzwa kutoka Marekani,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
“Ujumbe huu utafanya kazi kwa uratibu wa karibu na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani na Wizara ya Usalama wa Taifa ili kuwezesha mchakato wa kurejea kwa utaratibu, kisheria na wenye heshima,” taarifa hiyo imeongeza.
Uamuzi huo umekosolewa na baadhi ya raia wa Sudan Kusini wanaounga mkono mpango huo lakini wanahoji ni kwa nini Waziri wa Mambo ya Nje hakujumuishwa kuongoza ujumbe huo na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia. Utawala wa Kiir ulisisitiza kujitolea kwake kusuluhisha suala hilo mara moja.
“Kwa hiyo, tukio lililohusisha Bw. Kintu Makula/Nemeri Garang lilikuwa la kusikitisha, na hatua za ndani zimechukuliwa tangu wakati huo kuzuia kujirudia kwa matukio hayo ya kusikitisha,” amesema Dk. Benjamin Bol Mel, Makamu wa Rais wa shirika la Economic Cluster.
“Serikali ya Sudani Kusini inapenda kutoa heshima na shukrani kwa Rais Donald J. Trump na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio kwa uongozi wao na kuendelea kujitolea kutekeleza sera ya uhamiaji ya Marekani,” ameongeza.
Sudani Kusini imeomba radhi kwa usumbufu wowote uliosababishwa na Marekani na kueleza nia yake ya kutatua suala hilo haraka na kwa ushirikiano.
“Sudani Kusini inajivunia kusimama na Marekani kama mshirika katika kupata ufikiaji wa rasilimali za kimkakati muhimu kwa Sudani Kusini na uchumi wa Marekani na usalama wa taifa,” Dk. Bol Mel amesema.
Rais Salva Kiir bado amejitolea kukuza ushirikiano mzuri na Marekani katika nyanja kama vile biashara, uwekezaji, usalama wa kikanda, uzalishaji wa mafuta, na ushirikiano wa kimkakati kwenye madini muhimu.
Hata hivyo wafanyabiashara wa Marekani na watu binafsi wameonywa dhidi ya kufanya biashara nchini Sudani Kusini kutokana na wimbi la vikwazo vilivyowekwa dhidi ya maafisa wake wakuu wa serikali akiwemo Mel ambaye ofisi yake imetoa taarifa hiyo.