
Dar es Salaam. Wadau wa masuala ya miundombinu nchini wametaja sababu za makandarasi wa kigeni kutokamilisha miradi wanayopewa ikiwamo kutumia muda mrefu kutafuta wasaidizi wa bei nafuu.
Jambo lingine ni makandarasi hao kutuma fedha zote za mradi kwao baada ya kukamilishiwa malipo, hatua ambayo huongeza mchakato wa malipo ya makandarasi wasaidizi na mafundi kwenye mradi husika.
Wadau wameeleza hayo, baada ya jana Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega kulalamikia makandarasi wa barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam kuwa nje ya mkataba, akiagiza viongozi wa kampuni za China zinazotekeleza mradi huo kufika nchini kabla ya mwisho wa Machi.
“Hata mtu asiyefundi anaona hakuna muujiza wowote kukamilisha kazi hii, hawa wanatuchezea, nimewaelekeza wawaite viongozi wao kabla ya mwezi wa tatu, nitafuata utaratibu wa kidiplomasia pia kuwaandikia barua waje hapa nchini hiki kinachofanyika hakikubaliki,”amesema.
Akizungumza leo Alhamisi Machi 6, 2025, Profesa wa miundombinu, John Bura ambaye ni Rais wa Kampuni ya BQ Construction amesema baadhi ya makandarasi wanachelewesha miradi kutokana na kutumia mafundi wa kawaida kwenye miradi hiyo na kubana matumizi.
“Hao makandarasi wa kigeni tulishindwana nao, kwa sababu wanatafuta huduma ya gharama rahisi, tuliposhindwana walikwenda kuwatafuta mafundi wa kawaida na hapo walipoteza kama miezi mitatu wakati wa mchakato huo.
“Pili, wanapolipwa fedha wanazituma kwao zote, sasa mchakato wa kuzirudisha kulipa makandarasi wasaidizi na wafanyakazi wengine ni mgumu ndio maana unakuta wanaanza kuzozana na makandarasi wasaidizi kuhusu malipo mradi hauendi,”amesema.
Hoja hii iliibuliwa pia na Waziri Ulega akisema makandarasi wamekuwa na utaratibu wa kutuma fedha zote nyumbani huku kazi walizopewa zikisuasua.
Mbali na sababu hizo, Bura amesema hata mikataba inayohusisha ujenzi wa miundombinu hiyo ilisainiwa kwa presha bila kufuata taratibu zinazohitajika.
Mtaalamu huyo amesema sababu ya mkandarasi kudai joto ndio kikwazo cha kuwa nyuma ya mradi si kweli kwa kuwa, mkandarasi anapoona changamoto moja hutafuta mbinu mbadala ya kushughulikia.
“Kama kazi imeongezeka anaweza kuomba nyongeza ya muda, kama mvua kali ndio inazuia utekelezaji wa mradi anaweza kuomba muda,”amesema.
Mtaalamu mwingine wa uchumi wa biashara, Dk Donath Olomi amesema: “Lile ni jambo la kimkataba linashangaza waziri kumgombeza hadharani mkandarasi jambo hilo lilipaswa kushughulikiwa kisheria.”
Dk Olomi amesema mkataba unapochelewa lazima hasara itakuwepo hasa kuongezeka kwa gharama.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude amesema kilichofanywa na Waziri wa Ujenzi kuhoji utekelezaji wa mradi wa mwendokasi ni kwa niaba ya wananchi.
“Nafikiri waziri ameuliza kwa niaba ya Watanzania wengi wanaotamani kujua mradi wa BRT unaendeleaje. Inawezekana yeye na wataalamu wa wizarani wanafahamu haya yote, lakini wananchi hawajui.
“Hivyo kwenda kuwauliza kuhusu mradi ni ‘style’ tu ya kufikisha ujumbe kwa wanacchi juu ya nini kinacho endelea kwenye mradi,”amesema.
Alipoulizwa Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Dar es Salaam, Alinanuswe Kyamba kama walikuwa wakiona mwenendo wa kusuasua wa mkandarasi wakati wa majukumu yake, amesema wanafanya kazi kulingana na mkataba.
“Hatua hatuchukui tu ghafla tuna makubaliano ya kimkataba mkandarasi ameomba muda wa nyongeza ambao msimamizi wa mradi aataangalia hoja zake alafu zitapelekwa kwenye bodi na bodi ijiridhishe na kutoa maamuzi ya hatua zitakazofuata,” amesema.
Kyamba amesema mikataba ni mchakato mpana hadi kufanyika maamuzi ya kuachana na mkandarasi si jambo la siku moja.