Dar es Salaam. Udhaifu wa usimamizi wa sheria, rushwa kwa baadhi ya watendaji wa Serikali, ukosefu wa teknolojia ya kisasa ya ufuatiliaji, na mazingira magumu ya kiuchumi kwa wananchi waishio pwani katika mikoa ya Dar es Salaam na Lindi, vinatajwa kuwa vyanzo vya uwepo wa bandari bubu.
Si hayo pekee, viwango vikubwa vya ushuru wa bidhaa pia vinaelezwa kuchochea wafanyabiashara kuvikwepa kupitia njia haramu.
Katika kufanikisha hilo, imebainika watu wenye ushawishi wanaofaidika na mianya iliyopo hufanikisha upitishaji wa bidhaa za magendo kupitia bandari bubu bila hatua madhubuti kuchukuliwa.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, baadhi ya bidhaa za magendo hupitia kwenye bandari hizo zilizopo Mbweni na Kigamboni, pia Bagamoyo mkoani Pwani.
Licha ya Mbweni na Kunduchi zilizokuwa miongoni mwa bandari bubu maarufu kurasimishwa, bado wanaojishughulisha na biashara ya magendo wametafuta maeneo mengine jirani wakiendelea na kazi hiyo isivyo halali.
Mkoani Lindi, maeneo yanayotumiwa kupitisha bidhaa za magendo ni Somanga na Safina, yaliyopo Kilwa Kivinje, yanayotumika kutokana na mazingira yake ya mikoko mingi.

Bidhaa nyingine ndogo ndogo ambazo zimesafirishwa kwa njia ya boti.
Ofisa Forodha Mfawidhi Mkoa wa Lindi, Flora Kijole, akizungumza na Mwananchi Machi 13, 2025, amesema mafuta ya kupikia, sukari, mchele na vifaa vya umeme ni bidhaa ambazo wamekuwa wakizikamata kwenye maeneo ya bandari bubu.
Ameyataja maeneo vinara kwa kupitisha biashara ya magendo kuwa ni Somanga na Safina yaliyopo Kilwa Kivinje, Rushungi na Mayungiyungi (Kilwa).
Bandari hizo zisizo rasmi ni milango ya uingizaji na usafirishaji bidhaa zikiwa hazijasajiliwa na wala hazidhibitiwi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) au taasisi nyingine za Serikali.
Miongoni mwa taasisi hizo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Sheria ya Bandari Na. 17 ya mwaka 2004, kifungu cha 5, kinaipa TPA mamlaka ya kuanzisha, kuendesha na kusimamia bandari zote zilizopo Bahari ya Hindi na maziwa nchini.

Mifuko ya mchele inayopitishwa kwenye bandari bubu ya Kilwa Kivinje na kuhifadhiwa kwenye nyumba iliyopo jirani na fukwe ya bahari ya Hindi.
Sheria hii pia inasimamia maendeleo ya miundombinu ya bandari na kuhakikisha huduma bora kwa wateja, inazuia uanzishaji wa bandari zisizo rasmi kwa kufafanua taratibu maalumu za kufuatwa kabla ya kuanzisha bandari yoyote na kuhakikisha shughuli za bandari zinasimamiwa kikamilifu na TPA.
Ofisa Habari wa TPA, Leonard Magomba, akizungumzia kuhusu usimamizi unaofanyika, amesema maeneo ya bandari bubu awali hayakuwa na udhibiti wa usalama, hivyo wengi walitumia mwanya huo kupitisha biashara za magendo.
Amesema baada ya kurasimishwa bandari bubu, kumekuwa na usalama, kazi wanayofanya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Magomba amesema kumekuwa na ulinzi kwa saa 24 kwa kushirikiana na askari wa TPA na vyombo vingine vya ulinzi.

Hata hivyo, amesema bado wapo wanaobuni mbinu mpya kwa kutafuta maeneo mengine kwa shughuli hizo.
“Baada ya kuona kuna ulinzi, wanachoweza kufanya ni kutafuta eneo jipya,” amesema.
Ukubwa wa tatizo
Mei 2021, katika hotuba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho, akiwasilisha bungeni mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2021/22, alisema wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), zinatambua changamoto na athari za uwepo wa bandari zisizo rasmi (bandari bubu) katika pwani ya Bahari ya Hindi na kwenye maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Alisema kwa wakati huo kulikuwa na jumla ya bandari zisizo rasmi 694 zilizotambuliwa, na kati ya hizo, 240 zilikuwa katika mwambao wa Bahari ya Hindi, huku 329 zikiwa Ziwa Victoria, 108 Ziwa Tanganyika na 17 Ziwa Nyasa.
“Athari za uwepo wa bandari hizi ni pamoja na hatari za kiulinzi, kiusalama na upotevu wa mapato ya Serikali. Aidha, kuna ushindani usio sawia baina ya bandari rasmi na zisizo rasmi na biashara inayofanywa baina ya hizo bandari mbili tofauti,” alisema.
Wizara hiyo ilieleza kuwa kwa kushirikiana na Tamisemi, imeshazielekeza taasisi zinazohusika na suala hilo kuendelea kutathmini bandari zisizo rasmi ili kuishauri Serikali kuzirasimisha kwa lengo la kuimarisha usalama, kuongeza fursa za ajira na mapato ya Serikali.
Alisema hadi Aprili 2021, bandari zisizo rasmi 119 zilikuwa zimeainishwa katika awamu ya kwanza kwa ajili ya kufanyiwa tathmini ya kina ya kuzirasimisha.
Kati ya hizo, alisema katika mwambao wa Bahari ya Hindi zilikuwa 31, Ziwa Victoria (79), Ziwa Tanganyika (6) na Ziwa Nyasa (3).
Ilivyo maeneo ya pwani
Baadhi ya wananchi waishio maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi wameeleza kuwa wamekuwa wakishuhudia mitumbwi na majahazi yakishusha bidhaa, zikiwamo za mafuta ya kupikia nyakati za usiku au alfajiri.
Kwa maelezo ya wananchi hao, bidhaa hizo huuzwa kwa bei nafuu kwa wafanyabiashara, hivyo kuathiri ushindani sokoni.
Mchuuzi wa bidhaa eneo la Mbweni, ambalo awali lilitumika kwa bandari bubu kabla ya kurasimishwa, amesema licha ya sasa kuwapo udhibiti, bado kuna vitendo vya rushwa miongoni mwa watumishi wa umma wanaoruhusu bidhaa za magendo kupitishwa.
Akiomba kutotajwa jina, amedai kwa utaratibu ulivyo, mafuta ya kula yakifuata utaratibu halali yanapaswa kutozwa ushuru wa jumla wa zaidi ya Sh10,000 kwa dumu, lakini baadhi wanayapitisha kwa magendo kwa malipo ya Sh6,000.
“Licha ya TPA, TRA na TBS kuwa na ofisi zao huku kwa ajili ya kudhibiti na kukagua bidhaa zinazoshushwa, bado kuna mianya ya rushwa. Wanaelewana katika utozaji ushuru na idadi ya madumu inapunguzwa ili isijulikane,” amedai.
Amesema wapo pia wanaokwepa kutumia bandari hiyo ambao wametafuta eneo lingine katikati ya Mbweni na Bagamoyo ambako huvusha kwa magendo bidhaa hasa za mafuta na vipodozi.
Mkazi wa Mbweni aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina amesema baada ya kurasimishwa bandari hiyo, sasa bidhaa za magendo hushushwa mbali na fukwe.
Amesema bidhaa hizo hupelekwa kuhifadhiwa nyumba za jirani kabla ya kusafirishwa kupelekwa maeneo mengine.
“Bidhaa zikishushwa usiku au alfajiri, zinapelekwa nyumba za jirani na fukwe, kisha husafirishwa kwa bodaboda na magari madogo,” amesema.
Mmiliki wa nyumba eneo la Mbweni (jina linahifadhiwa) amesema wanafanya hivyo kwa ajili ya ugumu wa maisha.
“Hii tunaifanya kwa sababu ya ugumu wa maisha. Kwangu, ukilaza mzigo siku moja, unanilipa Sh50,000 hadi Sh100,000, inategemea ukubwa wake,” amesema.
Kiongozi wa kampuni ya Azania Group, John Laizer, amesema mafuta ya kula yamekuwa yakiingizwa nchini kwa njia isiyo rasmi.
“Ukipita eneo la Bahari Beach kuanzia saa 12:00 jioni unaona majahazi yanashusha madumu yakiwa na mafuta na hawana wasiwasi, kama ni jambo la kawaida. Hii inaweza kuwa chanzo cha viwanda vya mafuta kufa,” amesema.
Laizer amesema mafuta hayo yakiingizwa kinyemela hayalipiwi kodi, hivyo hata bei yake mtaani inakuwa ya chini na wananchi wanayakimbilia.
Kauli ya wizara
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, Machi 20, 2025, kwenye mkutano na wenye viwanda nchini, alisema uwapo wa bandari bubu ni changamoto kubwa inayohitaji ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Fedha na TRA kukabiliana nayo.

Bidhaa ambazo hazikutambulika kwa haraka ambazo zimeshushwa kwenye bandari bubu ya Kilwa Kivinje na kisha kuhifadhiwa kwenye nyumba zilizopo katika mwambao wa bahari.
Alitaja bidhaa zinazopitishwa kwenye bandari ambazo si rasmi kuwa ni mafuta ya kupikia na vitenge, hivyo kusababisha Serikali kukosa mapato.
“Baadhi ya bidhaa kupitishwa nje ya utaratibu ni athari kubwa. Tusipohangaika, viwanda vya mafuta vinaweza kufa, hivyo tunatakiwa tushirikiane na sekta nyingine kama Wizara ya Mambo ya Ndani na watu wa TRA,” alisema.
Alisema kuna majahazi yanakesha usiku kucha yakishusha mizigo katika maeneo yasiyo rasmi, na hao wanakuwa chanzo cha upotevu wa mapato na watu kukimbilia kununua bidhaa zao ambazo hazijathibitishwa na TBS.
Hilo, amesema, linahusisha masuala ya usalama wa nchi, hivyo kuna haja ya kukaa kikao cha pamoja kujadiliana namna ya kukabiliana na changamoto hiyo inayotishia usalama wa wananchi kwa kuingizwa vitu kinyemela ambavyo vinaweza kuwadhuru.
Kauli ya DC Lindi
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, amesema mwambao mrefu wa bahari wilayani humo ni miongoni mwa vyanzo vya kuwapo bandari bubu zinazochangia biashara ya magendo.

Mifuko ya sukari ikiwa imekamatwa ambayo imepitishwa kwenye bandari bubu ya Kilwa Kivinje.
Alitoa kauli hiyo Februari 18, 2025, alipokutana na maofisa wa TRA waliomtembelea ofisini kwake wakiwa katika shughuli ya kutoa elimu ya kodi mlango kwa mlango wilayani humo.
Amesema wilaya hiyo ina mwambao mrefu wa bahari ambao baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakitumia mwanya huo kuingiza bidhaa kinyume cha utaratibu, hivyo elimu ya kodi itawasaidia kubadilika.
“Rai yangu kwenu TRA, endeleeni kutoa elimu ya kodi ili wafanyabiashara wajue, unapofanya biashara bila kulipa kodi au kutumia njia za magendo unadhulumu na kuhujumu Taifa,” amesema.
Kaimu Meneja wa TRA, Mkoa wa Lindi, Faraji Mkikima, amesema mamlaka hiyo itaendelea kutoa elimu ya kodi kuhakikisha wafanyabiashara wanafahamu athari za biashara ya magendo.
Alipotafutwa na Mwananchi, Kamishna wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema: “Ni kweli moja ya changamoto tulizonazo ni bandari bubu. Magendo yanapita kwenye bandari bubu, bandari ambazo si rasmi.
“Tunacho kikosi rasmi kwa ajili ya kusimamia sheria kwa wanaotaka kupitisha bidhaa ndani ya nchi, hili ni kosa na tunachukua hatua. Hata bandarini tuna kikosi na tunakiwezesha.”
Mwenda amesema katika kuhakikisha wanakomesha jambo hilo, wameshaweka vifaa, zikiwamo boti ambazo zilizinduliwa Mwanza.

Bidhaa zilizopelekwa wenye moja ya nyumba zilizopo jirani na mwambao wa bahari ya Hindi, eneo la Kilwa Kivinje wakiwepo na waliopo pembeni ni baadhi ya watu wanaoishi kwenye nyumba hiyo.
“Bidhaa nyingi zinazosafirishwa ni zile fast moving (zinazouzika haraka) zikiwamo mafuta na sukari, lakini watu wana ujasiri hata saruji wanaleta kama magendo. Tukikamata, tunataifisha mzigo pamoja na boti iliyobeba. Kuna kesi mbalimbali tunafungua,” amesema.