
Mjumbe wa zamani wa kamati ya utendaji ya Simba, Said Tulliy amefichua mbinu walizotumia hadi wakafanikiwa kutopoteza mechi ya ugenini ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2018 dhidi ya Al Masry ambayo ilimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Tulliy ametaja mikakati hiyo siku mbili baada ya Simba kupangwa kukutana na Al Masry katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu katika droo iliyofanyika Alhamisi, Februari 20, 2025 huko Doha, Qatar.
Tofauti na ilivyokuwa mwaka 2018 ambapo Simba ilianzia nyumbani na kumalizia ugenini ambapo ilitolewa kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya mechi mbili baina ya timu hizo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2, safari hii Simba itaanzia ugenini huko Misri kati ya Aprili Mosi hadi 2 mwaka huu na mechi ya marudiano itacheza nyumbani kati ya Aprili 8 hadi 9.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Tulliy amesema kuwa Al Masry ni timu yenye mbinu nyingi za kuvuruga kisaikolojia wapinzani pindi inapokuwa Misri hivyo walilazimika kupambana sana nje ya uwanja na wakaweza kupata sare ingawa haikutosha kuifanya Simba isonge mbele.
“Watu wanazungumzia timu za Tunisia, Algeria, Morocco au kwa pale Misri wanazitaja Al Ahly na Zamalek lakini wale Al Masry wana mashabiki bora na wanaojua sana kushangilia timu yao. Na wamekuwa wakitoa presha kwa timu pinzani uwanjani hadi sisi ambao tulikuwa nje tukawa tunaihisi ile presha yao na wanafaidika na uwanja wao kuwa na majukwaa yaliyo karibu na eneo la kuchezea.
“Lakini pia wana vurugu sana na sisi kabla ya kwenda uwanjani tulitumia kama dakika 20 kubishana nao. Walitupa basi ambalo walitaka tulitumie lakini sisi tulipanga tusilitumie na wachezaji wetu wakapanda basi ambalo lilikuwa la mashabiki wetu waliokuwa wametoka Cairo jambo ambalo liliwaudhi wale na wakawa wanalazimisha kwamba tulitumie hilo,” amesema Tulliy.
Tulliy alisema mbali na kutotumia basi waliloandaliwa na Al Masry, pia walichukua tahadhari kubwa katika vyakula na huduma za hoteli waliyofikia.
“Chakula cha pale hotelini hatukula, kiliandaliwa kwingine na wachezaji tukawa tunawapelekea wale. Pia siku ya mchezo, tulizuia vyumba vya wachezaji kusafishwa asubuhi na masuala yote kuhusu wachezaji yalimalizikia vyumbani, tukawa tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti mipango yao,” amesema Tulliy.
Tulliy alisema kuwa sababu kadhaa zilichangia kuifanya Simba isifuzu mbele ya Al Masry mwaka 2018 lakini ana imani kubwa kwamba safari hii itasonga mbele na kuingia nusu fainali.
“Wakati ule nadhani ni ugeni. Simba tulikuwa hatujashiriki mashindano ya kimataifa kwa miaka kadhaa lakini pia hatukuwa na dondoo za kutosha na teknolojia kipindi kile ilikuwa chini hivyo ugeni wa mechi ukatuangusha ingawa tulijitahidi kwa kadri ya uwezo wetu.
“Aina ya kikosi pia kwani tulitengeneza nafasi nyingi kule kwao na mechi ya hapa Dar es Salaam kulikuwa na makosa madogo madogo. Tulikuwa na kocha mzuri wakati ule Pierre Lechantre lakini wachezjai wengi hawakuwa na uzoefu lakini safari hii tuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri na nje ya uwanja tuna faida. Tuna walimu ambao wana uwezo mkubwa wa kusoma na kufuatilia wapinzani lakini pia hata wachezaji wengi ni bora na wana uzoefu.
“Pia Simba imeweka kambi ya maandalizi ya msimu pale hivyo naipa nafasi kubwa ya kusonga mbele. KIkubwa hatua hii inahitaji umakini maana inatumia akili zaidi kuliko nguvu,” amemalizia Tulliy.
Huu ni msimu wa sita kwa Simba kucheza robo fainali kati ya misimu saba mfululizo iliyoshiriki mashindano ya Caf tangu 2018-2019, japo mara zote imekuwa ikikwamia hatua hiyo kwa kutolewa na wapinzani waliokutana nao iwe katika Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.
Simba inajivunia nyota walioibeba tangu hatua ya raundi ya pili ilipokutana na Al Ahli Tripoli ya LIbya na kuing’oa kutinga makundi ambapo alikutana na timu mbili za Afrika Kaskazini za CS Sfaxien ya Tunisia na CS Constantine. Mechi dhidi ya Watunisia ilishinda nje ndani na ile ya Waalgeria ilishinda nyumbani wakati ugenini ilipoteza 2-1.
Klabu ya Al Masry ilianzishwa Machi 18, 1920 ikiwa ni moja kati ya timu tano bora kwa taifa la Misri ambapo Simba itatakiwa kujiandaa kupambana nayo kwa umakini kutokana na ubora wa kikosi chao.
Hata hivyo haina mafanikio makubwa kwa michuano ya CAF na hata nyumbani kulinganisha na vigogo vingine vya Misri.
Mafanikio makubwa ya Al Masry katika mashindano ya klabu Afrika miaka ya hivi karibuni ni kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2018 baada ya kuing’oa Simba raundi ya pili, ingawa pia imewahi kutinga hatua kama hiyo kwenye Kombe la Caf mwaka 2002.