Kigogo… Pacome tatizo Aziz KI

JAMAA aliyemleta kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua nchini ametazama kiwango cha mchezaji huyo kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa na kusema kinachomzuia staa huyo kuonyesha makali yake zaidi ni nafasi anayocheza Stephanie Aziz Ki.

Pacome ambaye amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Yanga kuanzia amejiunga na kikosi hicho  alionyesha kiwango cha juu kwenye mechi iliyopita na kutoa pasi mbili za mabao, ukiwa ni mchezo wa kwanza anawika msimu huu.

Pamoja na kiwango hicho, Zambro Traore ambaye ni meneja wa mchezaji huyo ameliambia Mwanaspoti kwamba tangu amlete kiungo huyo nchini bado hajaona kiwango kile ambacho alikuwa anakitarajia kutoka kwake kutokana na nafasi anayochezesha.

Traore amefunguka kwamba kuna mambo yalimtingisha kiungo huyo na wamekubaliana kwamba kuanzia sasa auwashe moto kufikia kiwango ambacho anakijua ili mashabiki wa Yanga wafurahie zaidi.

“Mimi namjua Profesa, nadhani sihitaji kueleza sana juu ya ubora wake kila mtu ameona lakini watu wasishangae nikisema kwangu bado hajafanya kile ambacho nakijua kuhusu kiungo huyu kwa kuwa anapita kwenye kivuli cha Aziz Ki,”alisema Traore na kuongeza kuwa:

“Pacome nimemwambia anatakiwa sasa kuonyesha kiwango chake, kuna vitu ambavyo vilimzuia kufanya makubwa hapa kati, lakini vimekwisha naona ameanza kuongeza kitu kikubwa.

“Unajua alikuja hapa akamkuta Aziz Ki na kitu kibaya zaidi alikuwa na jina kubwa tayari timu nzima ilitengenezwa kumzunguka yeye.

“Hii ilisababisha Pacome awe anatumika sana pembeni kuliko kucheza namba 10, nafasi ambayo ndio anaiweza zaidi, sasa hapo wakati huu lazima acheze Aziz, shida kubwa inaanzia hapo.

“Siku Pacome akicheza namba 10, watu wanaufurahia uwezo wake kwani hapo ndio kama alizaliwa ili acheze eneo hilo,” alisema jamaa huyo raia wa Ivory Coast.

Msimu huu hadi sasa, Pacome amefunga mabao saba na kutoa asisti sita.

Aziz Ki hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara ameshafunga mabao matano akiwa amepiga asisti nne