Kigogo Bawacha apigwa na kujeruhiwa, Polisi yamsaka mlinzi 

Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linamsaka Noel Olevale anayedaiwa kuwa mlinzi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa tuhuma za shambulio la mwili dhidi ya Katibu Mwenezi wa Bawacha Taifa, Sigrada Mligo (34), mkazi wa Mtaa wa Mji Mwema, Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Machi 26,2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amesema tukio hilo limetokea jana Jumanne Machi 25, 2025 wakati viongozi wa Taifa wa Chadema walipokuwa kwenye kikao cha ndani kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche.

Kamanda Banga amesema miongoni mwa mambo waliyoyajadili ni pamoja na taarifa walizozipata kuhusu katibu huyo mwenezi kudaiwa kufanya mikutano kinyume na utaratibu wa chama hicho.

Kutokana na hili, Kamanda Banga amesema kuliibuka taharuki iliyosababisha Mligo kutolewa nje kwa lengo la kumpunguza munkari huku wajumbe wengine wakiendelea na kikao.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kamanda huyo, baadaye Mligo aliamriwa kurejea ukumbini.

“Alielekezwa kutolewa nje ya kikao ili kupunguza munkari aliokuwa nao na baada ya hali kutulia yalitoka maelekezo kuwa anaweza kurejea kuendelea na kikao hicho,” amesema Kamanda Banga.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa wakati Mligo anarejea ukumbini, inadaiwa alivamiwa na kushambuliwa na mmoja wa walinzi waliokuwapo mlangoni aliyefahamika kwa jina la Noel Olevale.

“Wakati vurugu hizo zinatokea, askari walikuwepo eneo hilo wakachukua hatua ya kumkamata mlinzi huyo, lakini baadaye akawaponyoka na kukimbia,” amesema kamanda huyo.

Kwa mujibu wa Kamanda Banga polisi walichukua hatua ya kumpatia huduma ya kwanza pamoja na PF3 kabla ya kupelekwa hospitali ya Kibena alikolazwa kwa ajili ya matibabu zaidi.

Tayari jadala kuhusu tukio hilo limefunguliwa kwa hatua zaidi.

Mwananchi limewatafuta baadhi ya viongozi wa Chadema kuzungunzia tukio hilo na kumpata mmoja wa viongozi wa Bawacha ngazi ya Taifa aliyekiri kutokea kwa tukio hilo. Hata hivyo, ameomba jina lake lihifadhiwe wakati anaendelea kufuatilia zaidi tukio hilo.

“Ni kweli, lakini kwa sasa siwezi kuzungumza zaidi mpaka hapo nitakapotulia na kupata taarifa kwa kina ndipo tutazungumza,” amesema.

Naye kada wa Chadema, Rose Mayemba alipoulizwa kuhusu mtifuano huo, amesema hakuna ugomvi uliotokea na kwamba wapo bize na kampeni ya ‘No reforms no election’

Pia, amesema kwa sasa hawawezi kufuatilia mambo ambayo hayahusiani na mikutano yao badala yake wanasonga mbele kufikia malengo yake.

“Sisi tuko bize na mikutano yetu, hakuna ugomvi wowote wala mwanachama kupigwa, hatuwezi kufuatilia yaliyo nje ya utaratibu wetu na tunazidi kusonga mbele,” amesema Rose, ambaye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *