Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Benson Kigaila amesema baada ya kuwapokea vigogo 3,000 waliokihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wataanza kuweka mikakati rasmi ya kupambana na ‘adui’ yao wa kudumu ambaye ni Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kigaila amesema mipango yao ni kufunga ukurasa wa kuacha kukijadili Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kujikita kukijenga Chaumma)na kuwa chama kikuu cha upinzani kuzidi vyote 19 vilivyopo nchini.
Hayo ameyasema leo Jumatano, Mei 21, 2025 wakati wa mahojiano na Mwananchi kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza wakati wakiwapokea wanachama zaidi 3,000 waliohama Chadema, tayari kwa kujipanga na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Kigaila aliyeteuliwa kushika wadhifa huo muda mfupi baada ya kujiunga na chama hicho Mei 19, 2025, amesema wanafunga ukurasa wa kuwazungumza Chadema kwa kuwa hawakujiunga na Chaumma ili kushindana na chama walichotoka.
“Tunataka kufunga ukurasa rasmi wa kuizungumzia Chadema leo baada ya kuwapokea hawa makada 3,000 na kuanza kupambana na adui wetu wa kudumu CCM, tuliihama Chadema kwa sababu ambazo tulishasema hatuwezi kurudia tena kuzisema,” amesema Kigaila.
Amesema wamejiunga Chaumma ili kuendeleza malengo yao ambayo walishindwa kuyatimiza wakiwa Chadema.

“Sisi timu yetu ambayo imeingia Chaumma imefunga ukurasa wa kuijadili Chadema na tutaelekeza nguvu zetu kwenye malengo mapana ya kupigania haki za Watanzania na wale wanaotaka kutujadili. Wao tunawaacha waendelee kwa kuwa hawana ajenda, lakini kwetu tunataka kuonyesha tunajua kufanya kazi,” amesema Kigaila.
Amesema mipango yao ni kushindana na CCM, huku akisema hawawezi kupoteza muda kukabiliana na Chadema kwa sababu hawana madaraka yoyote.
“Chadema ana nini ili tukamnyang’anye, chama cha siasa malengo yake ni kushika dola na inashikiliwa na CCM, tunataka tuwafungie kazi, ingawa wanatuita siye madalali basi watuache kama tumenunuliwa tumewaacha wakae wao kama marafiki, tunaenda kuendeleza tulipoishia,” amesema.
Alama alizoacha Chadema
Kigaila aliyekuwa anashikilia wadhifa kama huo Chadema kabla ya kukoma Januari 2025 baada ya kufanyika uchaguzi mkuu, amesema amefanya mengi ambayo anaamini hata kuondoka kwake ataendelea kuwa mfano.

“Mtu aliyefiwa hasemi shida yake ya kufiwa, wanamsemea watu wengine, kwa hiyo mimi ukiwauliza Chadema wenyewe watasema wanajua hakuna aliyejenga Chadema kama mimi pamoja na wenzangu. Nimekaa porini miaka 21 kukijenga chama kuanzia ngazi ya msingi,” amesema Kigaila.
Alipoulizwa kama ni hivyo ilikuwaje akihame chama alichokijenga kwa miaka mingi katika majibu yake amesema; “Chama siyo gereza na wala si baba wala mama, sema huwa kinaanzishwa na watu wanajiunga na wanaweza kutoka kama kinaacha malengo yake ya kuanzishwa kwake,” amesema.
“Chaumma kitakuwa chama kikubwa hawa watu unaowaona hapa wako mikoa yote na majimbo yote Tanzania, waliokuja hapa ni viongozi tu baada ya kuwapokea wanachama tutaanza kwenda kuwapokea mikoani,” amesema.
Kigaila amesema baada ya kumaliza shughuli ya kuwapokea makada hao, Chadema itaendelea na kubaki na viongozi pekee lakini wanachama wote wanatarajia kuwakusanya wawafuate.
“Chama ni wanachama, nao wako hapa, viongozi waliopo hapa ni zaidi ya 4,000 na siwezi kujua waliko huko mtaani, tukimaliza mkutano wa leo tutazungumza, lakini mjue adui yetu mkubwa ni CCM na yajayo yanafurahisha,” amesema Kigaila.
Pia, amesema baada ya kuwapokea, watapanga ratiba na kuanzia Juni Mosi, 2025 wanaanza ziara mikoani kukijenga chama hicho.
Wakati akieleza hayo, Mwenyekiti wa Chama hicho, Hashimu Rungwe amesema shughuli inayofanyika katika ukumbi huo ni mwanzo na mafuriko yanakuja kuanzia mwezi ujao huko mikoani.