Mbeya. Wakati mwili wa aliyekuwa Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Mkoa wa Mbeya, Lucia Sule (33), ukiagwa katika kiwanja cha Soko la Uhindini, wabunge waeleza kupata pigo kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.
Mwili wa Lucia umeagwa leo jijini hapa na umesafirishwa kwa mazishi yatakayofanyika nyumbani kwao Babati, Mkoa wa Manyara.
Marehemu, Lucia alifariki dunia usiku wa Machi 31, 2025 wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, akiwa miongoni mwa majeruhi watano waliolazwa hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu.
Lucia ni miongoni mwa waliopata ajali kwenye msafara wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Fadhil Rajab iliyotokea aliyekuwa kwenye ziara ya kichama mkoani Mbeya.
Ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Shamwengo Wilaya ya Mbeya Vijijini, Februari 25, mwaka huu ambapo kifo chake kinafikisha idadi ya watu sita waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo.
Watu watatu walipoteza maisha papo hapo na watatu walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu hospitalini.

Mbunge wa Lupa Wilaya ya Chunya, Masache Kasaka akitoa heshima za mwisho kwenye jeneza lenye mwili wa Katibu wa UWT, Lucia Sule kabla ya kusafirisha kwenda nyumbani kwako Babati Mkoa wa Manyara kwa Mazishi. Picha na Hawa Mathias
Lucia ambaye amekuwa hospitali tangu ilipotokea ajali Februari 25 mwaka huu, ndiye majeruhi wa mwisho aliyekuwa amebaki hospitali akipatiwa matibabu.
Wengine waliofariki dunia wakati wakipatiwa matibabu hospitali ni Thadei Focus ambaye ni dereva wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Seleman Ndelage ambaye ni mwandishi wa habari wa Dream Media na Lucia Sule ambaye ni Katibu wa UWT Mkoa wa Mbeya.
Kifo cha Lucia kimefikia idadi ya watu sita waliopoteza maisha kutoka na ajali hiyo huku majeruhi mwandishi wa Chanel Ten, Epimarcus Kalokola na Denis George waliokuwa kwenye matibabu katika hospitali hiyo wakiruhusiwa baada ya hali zao kuendelea vizuri.
Ajali hiyo ilihusisha gari la Serikali STM na basi la kampuni CRN ambapo watu saba walijeruhiwa na watatu walifariki papo hapo akiwepo mwandishi wa habari wa kujitegemea Furaha Simchimba.
Wengine waliofariki ni mjumbe wa kamati ya Utekelezaji (CC) Wilaya ya Mbeya, Daniel Mselewa na Utingo wa basi, Isaya Geuza ambao waliagwa Februari 27 mwaka huu jijini hapa.
Awali, akitoa salamu ya wabunge katika ibada ya kuaga mwili wa Lucia, Mbunge wa Lupa Wilaya ya Chunya, Masache Kasaka amesema wamepata pigo kwa maelezo kuwa enzi za uhai wake Lucia alikuwa mtenda haki na mwenye misimamo ya kweli.
“Kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Mbeya tulipokea taarifa za msiba kwa masikitiko mkubwa sana, awali tulipata taarifa njema za mwenendo wa afya yake kuimarika zilitupa matumaini,” amesema Masache.
Amesema kwa kipindi kifupi cha uwepo wake, wabunge wamenufaika kwa mazuri aliyo kuwa nayo na misimamo ya kusimamia haki na kutoa maamuzi sahihi pasipo upendeleo.

Baadhi ya wananachi walioshiriki ibada ya kuaga mwili wa Katibu wa UWT Mkoa wa Mbeya, Lucia Sule (katikati mwenye nguo nyeusi) aliyekuwa Mbunge viti maalum Dk Mary Mwanjelwa. Picha na Hawa Mathias
“Hakika tumepoteza jembe kweli kweli, wanasema pengo halizibiki sijui kama hili litazibika katika kipindi cha kuelekea mchakato wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025,”amesema Masache.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa CCM (Mnec), Ndele Mwaselela amesema wamepokea taarifa kwa uongozi wa Hosptali ya Gharama zote za matibabu za kiongozi huyo kabla ya umauti kumkuta zimetolewa Rais Samia Suluhu Hassan tangu ilipotokea ajali Februari 25 mwaka huu.
Historia ya marehemu
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Mbeya, Christopher Uhagile amesema kuwa marehemu Lucia Sule alihamishiwa kutoka Mkoa wa Iringa hadi Mkoa wa Mbeya na mpaka alipofariki dunia, alikuwa ametimiza miezi sita kituo chake kipya cha kazi.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa CCM (Mnec) Ndele Mwaselela akiwa miongoni mwa viongozi walioshiriki ibada ya kuaga mwili wa Katibu UWT Mkoa wa Mbeya. Picha na Hawa Mathias
Uhagile amesema kuwa Lucia alikuwa akiendelea kupata matibabu chini ya uangalizi wa madaktari katika chumba cha uangalizi wa karibu (ICU).
Amesema hali yake ilianza kuimarika na Machi 30, 2025, madaktari walipendekeza ahamishwe kwenye chumba cha kawaida ili kuanza mazoezi.
“Walipokuwa wanajiandaa kumhamisha kutoka ICU usiku wa Machi 31, 2025, Lucia alipoteza maisha,” amesema Uhagile.
Sababu za kifo
Uhagile alifafanua kuwa, baada ya hali ya Lucia kubadilika, madaktari walimfanyia uchunguzi wa kina na kugundua kuwa matatizo ya ini na figo yalikuwa chanzo cha kifo chake.
Aidha, Uhagile aliwahimiza wanachama wa CCM kuwa na akiba ya maneno na kuwaombea dua marehemu na wale walioshiriki katika kusindikiza mwili wake hadi nyumbani kwao Babati, Mkoa wa Manyara.