
Dar es Salaam. Mastaa wa zamani waliocheza Ligi Kuu Bara wamemzungumzia aliyekuwa kipa wa Simba na Yanga, Doyi Moke (marehemu) kwamba watamkumbuka kwa ucheshi na uchapakazi wake.
Kipa huyo wa zamani wa Simba na Yanga, aliishi kwenye mitaa ya Kariakoo kuanzia 1999 hadi 2003.
Moke, raia wa DRC kutoka eneo la Bukavu ameripotiwa kuuawa asubuhi ya Machi 6, mwaka huu huko kwao ukiwa ni msiba ambao umewasikitisha wanasoka wengi wa zamani.
Sababu za kifo chake zinatajwa ni kuchomwa moto na wananchi waliojichukulia sheria mkononi wakidhani ni mhalifu. Katika siku za hivi karibuni matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi huko Bukavu nchini DRC yamekuwa mengi sana.
Sababu kubwa inatajwa kuwa ni kupambana na wimbi la uhalifu kufuatia wafungwa wote kutolewa jela na Waasi wa M23 baada ya kuliteka eneo hilo. Wafungwa hao sasa wamegeuka kuwa wahalifu mitaani na wananchi hawana namna zaidi ya kuwakamata na kuwachoma moto. Kwa hiyo wananchi walimkamata Doyi Moke kimakosa wakidhani mhalifu na kumchoma moto.
Akizungumza kwa masikitiko baada ya kupata taarifa ya kifo hicho, kipa wa zamani wa Simba na Yanga, Ivo Mapunda alisema Moke alikuwa mtu safi na alipenda kucheka na kila mtu, kuna wakati walikuwa wanashauriana mambo ya kazi, hivyo kifo chake kimemsikitisha.
“Sikucheza na Moke timu moja, isipokuwa ligi moja, wakati nipo Prisons alikuwa Majimaji ya Songea, nakumbuka wakati anakwenda timu kubwa Simba na Yanga aliniambia, hivyo tukawa tunashauriana kuhusu mazoezi na mechi, alikuwa mtu safi sana na mcheshi, hili ni pigo kubwa sana,” alisema Mapunda.
Kwa upande wa staa wa zamani wa Yanga, Ally Mayay Tembele, alisema kifo cha Moke kimemsikitisha na atamkumbuka uhamasishaji wake uwanjani na alipenda ushindani kwenye kila mechi.
“Nakumbuka wakati tunafanya mazoezi Uwanja wa Kaunda, tukimaliza ya kocha anatuambia naomba mnipigie mashuti, basi tulikuwa tunafanya hivyo hadi giza linaingia, alipenda kushangilia hata akikaa benchi, kuna kauli alikuwa anaongea kwa Kikongo ila kwa Kiswahili alimaanisha ushindani uendelee, apumzike kwa amani mwamba,” alisema Mayay ambaye aliwahi kugombea nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mbali na hao kipa na kocha wa zamani wa Yanga, Peter Manyika alisema, ni pigo kwa wanasoka wengi ambao walikuwa wanamfahamu kwa kuwa alikuwa mcheshi na mtu mwenye roho safi.
“Moke alikuwa mcheshi sehemu anapokuwepo muda wote ni kicheko, kifo chake kimeniumiza, lakini katangulia kila mtu ataondoka kwa wakati wake ambao Mungu kampangia, ingawa ni jambo la kuhuzunisha sana.”
Doyi Moke ni nani
Alikuja Tanzania mwaka 1997 kujiunga na timu ya Majimaji ya Songea. Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wa wakati ule, Anna Makinda, aliamua kuwekeza kwenye timu ili kurudisha heshima ya klabu ya Majimaji na Mkoa wa Ruvuma kwa jumla.
Akamleta kocha Nzoyisaba Tauzany kutoka Burundi, na nyota wengine wengi kama akina Godfrey Kikumbizi kutoka Mtibwa Sugar, Willy Martin ‘Gari Kubwa’ kutoka Yanga, John Alex Lwena, aliyerudi Majimaji kutoka Yanga na kadhalika.
Kwa hiyo Doyi Moke alijiunga nyota hawa na kutengeneza moja ya kikosi bora na kwa miaka hiyo. Usajili wa Doyi Moke kwenda Maiimaji ulipambwa sana wakati, ikisemekana alisajiliwa kwa kiasi cha shilingi laki saba.
Kikosi hiki kikatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Muungano mwaka 1998 na kushiriki klabu bingwa wa Afrika. Wakati ule Ligi Kuu ya Muungano ndiyo ilikuwa Ligi Kuu ya Tanzania na bingwa wake ndiye aliyetambuliwa na CAF na Fifa. Bingwa wa Bara alitambuliwa na CECAFA tu na aliishia kushiriki Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame).
Mwaka 1999, Doyi Moke na wenzake wawili, Steven Mapunda ‘Garrincha’ na Amri Said ‘Stam’ wakatimkia Simba. Moke akacheza Simba hadi 2000 na kuhamia Yanga mwaka 2001 hadi 2003 alipoondoka na kutimkia Vital’O ya Burundi, timu aliyoitumikia kabla ya kuja Tanzania.
Apata lawama kwenye Dabi
Moke alifanya mengi mazuri lakini atakumbukwa zaidi kwa kashikashi aliyoipata mwaka 2000 kwenye mechi ya watani. Mechi hii iliyofanyika Agosti 5, 2000 uwanja wa taifa (sasa Uhuru), inakaribia kufanana na mechi ya safari hii. Ni kwamba siku ile Yanga ilikuwa na mchezaji mmoja aliyetoka kufunga ndoa, Idd Moshi ‘Mnyamwezi’ na safari hii Yanga ina mchezaji aliyetoka kufunga ndoa, Stephanie Aziz Ki.
Katika mechi ile, bwana harusi Idd Moshi alitokea fungate moja kwa moja na kufunga mabao mawili yaliyoipa timu yake ushindi mnono wa 2-0.
Doyi Moke akiwa kwenye lango la Simba, alilaumiwa kwa kudaiwa kuihujumu timu. Yeye mwenyewe alinukuliwa akisema wakati ule kwamba sababu kuu ni kudai pesa zake hivyo anaangushiwa jumba bovu. Ushindi huo wa Yanga ulikuwa wa mwisho dhidi ya Simba, hadi Oktoba 26, 2008 kwenye mechi ya kwanza kabisa uwanja mpya wa taifa (sasa Mkapa).
Bao la Mkenya Ben Mwalala likafuta uteja wa Yanga wa miaka 7 mbele ya Simba. Basi Doke akaondoka Simba baada ya msimu ule wa 2000 na kujiunga na Yanga.
Moke atua Yanga
Jangwani Moke atakumbukwa zaidi kutokana usajili wa kikosi chao kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Chini ya Kocha Charles Boniface Mkwassa, Yanga ilifanya moja ya matukio yasiyotegemewa.
Walipangwa kucheza na Highlanders ya Zimbabwe (timu iliyomlea na kumkuza Prince Dube) na mechi ya kwanza Dar es Salaam iliisha kwa sare ya 2-2. Lakini wakiwa ugenini jjini Bulawayo, Yanga ilishinda 2-0 katika mechi iliyovunjika baada ya mashabiki wa Highlanders kuingia uwanjani kufanya fujo wakigomea penalti ambayo Yanga walipata.
Yanga wakavuka hatua hiyo na kukutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Wakapoteza 3-2 ugenini na kutoka sare ya 3-3 nyumbani, mechi iliyofanyika Mwanza. Doyi Moke alikuwa golini mechi zote hizi.