Kiduku, Mwakinyo wanavyopishana duniani

Dar es Salaam. Wakati Hassan Mwakinyo akihitaji nyota moja na nusu kuingia kwenye anga za mastaa wa ndondi duniani, jahazi linazidi kuzama kwa Twaha Kiduku ambaye wiki iliyopita alichapwa kwa pointi nchini Ujerumani.

Kiduku aliyezichapa kwenye uzani wa super middle, alipigwa na Juergen Doberstein kwa pointi za majaji 3-0, jaji Iwan Horn na Nikita Horn kila mmoja alimpa pointi 107-120 na jaji Ruslan Svider akimpa pointi 108-119.

Hata hivyo, Kiduku amefichua siri ya kipigo hicho akidai marefa wa nje wamekuwa na upendeleo kwa mabondia wa nchi zao akijitolea mfano katika pambano hilo lililochezeshwa na Mike Wissenbach.

“Nilipigwa lakini si kimchezo,”alisema Kiduku akibainisha pia kupata hali ya kizunguzungu raundi ya tatu na ya tisa.

“Raundi ya tatu nilikaza,m ya tisa nilikwenda chini, japo watu wansema ni ngumi, lakini haikuwa ngumi, mpinzani wangu alikuwa kwenye ‘motion’ ya kupiga, lakini kabla hajanigusa mimi nilidondoka kwa kizungu zungu,” alisema Kiduku jana.

Kipigo hicho kimeendelea kudidimiza renki ya Kiduku ndani na nje ya nchi ambako sasa ni wa 162 kati ya mabondia 1649 duniani na nchini ameporokoma kutoka namba moja hadi nafasi ya tatu kwenye uzani wa super middle.

Hata hivyo, Kiduku amesisitiza kujipanga upya ili kurudi kwenye renki yake ya awali na ikiwezekana zaidi ya hapo.

Katika uzani huo, Kiduku amempisha Selemani Kidunda ambaye sasa ndiye namba moja kwa mujibu wa Mtandao wa Ngumi za Kulipwa wa kimataifa (Boxrec) na nafasi ya pili inashikiliwa na bondia Joseph Maigwisya.

Bondia huyo aliyeingia kwenye ndondi 2021 amewachapa ‘wakali’ kadhaa akiwamo Said Mbelwa, Jacob Maganga, George Dimoso, Hussein Itaba na Ibrahim Tamba na kupanda hadi nafasi ya pili iliyokuwa ikisgikiliwa kwa muda mrefu na Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ ambaye ameporomoka hadi nafasi ya tano.

Mwakinyo anarudi

Wakati Kiduku akiporomoka, ‘hasimu’ wake Hassan Mwakinyo ni kama anarudi kwenye ubora wake akipanda hadi nafasi ya 19 duniani na sasa ametangaza pambano la kutetea mkanda wake.

Mwakinyo ambaye amepandisha uzani kutoka super welter (kg 69) na sasa anapigania middle (kg 70-75) ameendelea kung’ang’ania nafasi ya kwanza kati ya mabondia 43 kwenye uzani wake nchini na wa 19 duniani kati ya mabondia 1872.

Bondia huyo aliyepitia panda shuka tangu mwaka 2018 alipomchapa Sam Eggington kwa Technical Knock Out (TKO) na kupanda hadi nafasi ya 14, amewahi kuporomoka hadi nafsi ya 109 akipitia panda shuka kwa miaka kadhaa hadi yupo nafasi ya 19.

Mbabe wao huyu hapa

Licha ya renki hizo, Kiduku akiporomoka na Mwakinyo kupanda, bado ‘wababe’ hao hawajaifunika rekodi ya ‘mkali’ Fadhil Majiha ambaye ndiye kinara wa Tanzania kwenye kila uzani.

Katika orodha ya mabondia bora wa kila uzani (pound for pound), Majiha ambaye ni namba moja kwenye uzani wake wa bantam na wa 14 duniani, ndiye kinara wa Tanzania wa kila uzani akimiliki nyota tatu na nusu.

Bondia huyo aliyewahi kuzichapa pambano la utangulizi kusindikiza pambano la Manny Pacquiao nchini China anasema, kujituma na kiu ya kutaka mafanikio ndivyo vimemfikisha hapo.

“Huwa sichagui wala sichungulii bondia wa kupigana naye, napigana na yoyote atakayeletwa na mara nyingi nacheza na mabondia wakali zaidi yangu na kuwapiga, hii ndiyo siri ya kupanda kwenye renki,” anasema.

Ibrahim ‘Class’  anayeongoza kwenye uzani wa super feather anakamata nafasi ya pili akifuatiwa na Mwakinyo na Ibrahim Mafia anayepigania uzani wa super bantam ni wa nne na tano bora inahitimishwa na Abeid Zugo anayepigani uzani wa light.

Wengine waliongia 10 bora ni Juma Choki (super feather), Salmin Kassim (super bantam), Salimu Jengo (light), Selemani Kidunda (super middle) na Kalolo Amiri (super bantam) huku Tony Rashid (14), Nasibu Ramadhani (16), Loren Japhet (17) na Said Chino (20) wakimaliza kwenye top 20 ya kila uzani.

Mastaa wengine nao chali

Katika orodha hiyo, mastaa na nguli wa ndondi nchini wameshindwa kuingia kwenye top 20 ya Tanzania katika kila uzani akiwamo Kiduku aliyeporomoka kutoka nafasi ya tano hadi ya 21, Mbabe (61) na Mfaume Mfaume ambaye kwa sasa ni inactive.

Wengine ni Idd Pialari (67), Francis Miyeyusho (122), Awadh Tamim (137), Mada Maugo (219), Cosmas Cheka (220) , Habibu Pengo (247), Karim Mandonga (254) huku mkongwe Said Yazidu akiendelea kukomaa nafasi ya 294.