Kibwana afichua jambo kuhusu Aziz KI

MRATIBU wa Yanga Princess, Kibwana Matokeo amesema kiungo mshambuliaji wa Yanga, Aziz KI amekuwa mtu muhimu kwenye matokeo ya timu hiyo akiwapa sapoti wachezaji wa kike.

Aziz KI kwenye mechi mbalimbali za Ligi ya Wanawake amekuwa akionekana uwanjani, Yanga Princess inapocheza ikiwamo mchezo wa juzi wa dabi dhidi ya Simba Queens.

Akizungumza na Mwanaspoti, Matokeo alisema nyota huyo raia wa Burkina Faso amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi hicho akiwapa hamasa wachezaji wa kike kwenye mechi mbalimbali hasa za dabi.

“Aziz ni kama shabiki ama mdau mkubwa wa Yanga Princess tangu siku ya kwanza, katika misimu tofauti huwa anaongea nao na kuwapa uzoefu kwenye mpira, namna ya kuishi sio ajabu kumuona uwanjani amekuwa akifanya hivyo,” alisema na kuongeza:

“Tulipokwenda Arusha kwenye mashindano ya Samia alitupigia simu na kutuambia anahitaji kombe hilo lirudi nyumbani iwe kama zawadi ya harusi yake na tulifanikiwa na alisema nitakuja uwanjani kwenye mechi ya dabi natamani mfanye vizuri.”

Kwenye mechi 13 za ligi, Yanga imeshinda nane, sare tatu na kupoteza mbili dhidi ya JKT na Simba ikiruhusu mabao tisa na kufunga 29 ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na pointi 27.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *