Kibu, Hamza kuna siri nzito Simba

SIMBA imerejea kambini jana tayari kwa maandalizi ya mchezo ujao wa Dabi ya Kariakoo, huku kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Kibu Denis akifichua beki Abdulrazack  Hamza, amekuwa kipimo kizuri mazoezini kwa namna anavyomkaba na imemrahisishia kazi katika mechi za mashindano, anapokutana na mabeki wa aina yake.

Kibu alisema aina ya ukabaji wa Hamza sio rahisi kupenya eneo alilosimama, isipokuwa kwa kutumia akili, nguvu na kufanya maamuzi ya haraka na anachokifanya dhidi ya mabeki katika mechi kinaanzia mazoezini.

“Katika timu mkiwa na beki aina ya Hamza ni msaada mkubwa kwa washambuliaji na mawinga, kwani changamoto anayotupa  mazoezini inatujengea kutowahofia mabeki wa timu pinzani tunapokuwa katika mechi,” alisema Kibu ambaye hadi sasa hajafunga bao lolote la Ligi Kuu, japo ana asisti moja.

Kibu aliisema Hamza ni beki asiyependa mzaha wakati wa kazi na anapenda kuzingatia vitu muhimu vinavyomsaidia kuonekana bora uwanjani.

“Japo sijawahi kumwambia ni kati ya mabeki ninaowakubali, ni mshikaji wangu na nafahamu anavyoipenda kazi, ikifika wakati wa kupumzika, anapumzika kufanya mazoezi basi anafanya kweli kweli, akiendelea kupata uzoefu atafanya makubwa kwa Simba na Taifa Stars,” alisema.

Kibu kufunga mabao mengi ilikuwa msimu wa msimu wa 2021/22 mabao manane, msimu wa 22/23 mabao mawili, msimu wa 2023/24 bao moja na kuhusu ukame wa mabao mshambuliaji huyo wa zamani wa Geita Gold na Mbeya City alisema; “Ikifika wakati wa kufunga nitafunga, kikubwa nafanya kazi ambayo ina manufaa kwa klabu ndio maana kocha ananipa nafasi ya kucheza.”

Mara ya mwisho kwa Kibu kufunga katika Ligi Kuu Bara ilikuwa msimu uliopita katika Dabi ya Kariakoo ya Novemba 4, 2023 pale Simba ilipocharazwa mabao 5-1, japo katika mechi za kimataifa  msimu huu ameifungia Simba mabao matatu katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa upande wa Hamza aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea SuperSport United ya Afrika Kusini, alisema Kibu ni aina ya wachezaji wasiokata tamaa, ana nguvu na kasi.

“Nafurahi kucheza kiungo mshambuliaji wa aina yake, anafanya nifikirie zaidi jinsi ya kukabana naye, akija kwa kasi najua nifanye kitu gani, akitumia nguvu nijipangaje, hivyo uwepo wake unazidi kunipa maarifa zaidi ya kazi yangu,” alisema Hamza anayemiliki bao moja katika Ligi Kuu kwa sasa.