Kibano taasisi za umma, binafasi zinazotumia mkaa, kuni mbioni

Dodoma. Serikali ya Tanzania imeanza kufuatilia utekelezaji wa katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi za umma na binafsi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumatano Februari 12, 2025 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis wakati akijibu swali la Mbunge wa Rungwe (CCM), Anton Mwantona.

Katika swali la msingi, mbunge huyo ameuliza Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha taasisi zinazohudumia watu wengi zinaweka mifumo ya majiko ya gesi ili kuokoa mazingira.

Naibu Waziri amesema jumla ya taasisi 551 zimeanza matumizi ya nishati safi ya kupikia; kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa nishati safi ya kupikia; na  kusaini  makubaliano ya awali na wawekezaji mbalimbali ikiwemo kampuni ya Oryx, Taifa Gas, Lake Gas na Manji’s gas.

Amesema kampuni zimeanza kutoa ruzuku ya Sh8.64 bilioni kwenye nishati safi ya kupikia ili kupunguza mzigo wa gharama kwa watumiaji wa nishati safi ambapo jumla ya majiko 452,455 yamepata ruzuku.

“Aidha, Serikali inaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuanzisha Mfuko wa Nishati safi ya kupikia ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi,” amesema Khamis.

Waziri huyo amesema, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha uandaaji wa Kanuni ya Katazo la Matumizi ya Kuni na Mkaa kwa Taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku. Kanuni hizo zitajumuisha taasisi za umma na binafsi.

Jumatano ya Mei 8, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia huku akiitaka Wizara ya Nishati ishirikiane na sekta binafsi kuona namna ya kuifanya bei ya gesi iwe himilivu.

Pamoja na hatua hiyo itakayoshinikiza matumizi ya nishati safi, mkuu huyo wa nchi alitoa marufuku ya matumizi ya kuni na mkaa kupikia kwa taasisi za umma na binafsi zinazohudumia watu zaidi ya 100.

Hatua hizo zote zililenga kuweka msisitizo wa utekelezaji wa mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, unaotaka kufikia mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi.

Mkakati huo ulizinduliwa katika kipindi ambacho, takwimu zinaonyesha asilimia 90 za kaya zote nchini zinatumia nishati ya kuni na mkaa. Hiyo ni sawa na kusema kati ya kaya 10, tisa zinatumia nishati isiyo safi kupikia.

“Kaeni na wizara muone wapi tubane, wapi tuongeze na wapi tupunguze ili tuweke bei himilivu na wananchi wengi zaidi watumie (Nishati safi),” alisema Rais Samia.

Katika msisitizo wake wa kupunguza bei ya nishati hiyo na nyingine safi za kupikia, aliibebesha Wizara ya Nishati jukumu hilo, huku Serikali kuu akisema itabeba jukumu la utoaji elimu na kutunga sera wezeshi.

“Jukumu la Serikali ni kutunga sera wezeshi kufikia malengo ya mkakati na kutoa elimu kwa wananchi, huku Wizara ya Nishati ikiwa na jukumu la kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa uhakika na bei himilivu,” amesema Rais Samia.