Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amevitaja vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Gaza na Lebanon kuwa ni vita kati ya haki na batili.
Hujjatul-Islam Walmuslimin Kazem Seddiqi, amesema kuwa: Leo hii vita vya utawala ghasibu wa Israel si vya Gaza na Lebanon pekee, bali ni vita kati ya dini na upagani, haki na batili, ubinadamu na uovu.
Akiashiria kikao cha hivi karibuni cha wakuu wa nchi za Kiislamu mjini Riyadh, Seddiqi amezikosoa nchi hizo kwa kutoiunga mkono Kambi ya Muqawama na kusema: Tunalaani matokeo ya aina hii, kwa sababu nchi za Kiislamu zinapaswa kuwajibika zaidi kwa Kambi ya Mapambano.

Imamu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amezungumzia suala la kuchaguliwa Donald Trump kuwa rais mpya wa Marekani na kusema: “Kuchaguliwa kwa Trump kuwa rais wa Marekani hakuna umuhimu kwetu. Marekani haina faida yoyote kwa mataifa mengine isipokuwa kupanua ubeberu, uporaji, kuunda magenge ya kigaidi, mapinduzi katika nchi nyingine na kuzusha na mifarakano katika mataifa mbalimbali.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran ameongeza kuwa: “Watu ambao Trump amewachagua kusimamia masuala ya Marekani wote wamekula kiapo cha kuihami Israel na kuwa na misimamo mikali dhidi ya Iran, hivyo hakuna tofauti kati ya huyu na yule.”