Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran: Israel imekwisha kimkakati

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema utawala wa Kizayuni wa Israel umeshindwa na kuangamizwa kistratijia.

Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Mohammad Hassan Abu Torabifard amesema: Baada ya kupata hasara kubwa ya kijeshi, Wazayuni hawakufikia malengo waliyoyaainisha katika uvamizi wao Ukanda wa Gaza,  na kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa wanasumbuliwa na vita vinavyoendelea kwa zaidi ya mwaka.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran ameongeza kuwa: Wataalamu wa Kimagharibi wameandika kuwa Israel imekwisha katika mtazamo wa kistratijia na inayumbayumba mno kijamii na kisiasa.

Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Mohammad Hassan Abu Torabifard ameashiria Operesheni Ahadi ya Kweli- 2 dhidi ya utawala wa Kizayuni na kusema kuwa: Operesheni hii ni shambulio kubwa na tata zaidi la makombora ya balistiki duniani na limetoa onyo kali kwa utawala huo na washirika wake juu ya uwezekano wa kuchukua hatua yoyote dhidi ya Iran.

Swala ya Ijumaa, Tehran

Imamu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran pia amezungumzia kushindwa mtawalia utawala ghasibu wa Israel mkabala wa harakati za mapambano za Lebanon na Palestina na kusema: Iwapo Wazayuni wataendelea uchokozi wao huko Gaza na Lebanon, wanapaswa  kungojea muujiza wa Muqawama huko Gaza na Hizbullah ya Lebanon ambao utaupondaponda utawala huo wa Kizayuni.